Sura ya 61 Kikosi cha Mormoni Juni 1846–Julai 1847 Wakati Watakatifu walipokuwa Iowa, Kapteni James Allen wa Jeshi la Marekani alikuja kumwona Brigham Young. Kapteni Allen alisema rais wa Marekani alitaka wanaume 500 kutoka Kanisani kujiunga na jeshi ili kusaidia katika vita na Mexico. Ingawa huu ulikuwa ni wakati mgumu kwa Watakatifu na wanaume walihitajika kwa ajili ya safari ya magharibi, Brigham Young aliwahimiza waende. Fedha ambazo wangelipwa zingesaidia familia zao, Watakatifu ambao walikuwa masikini, na wamisionari. Kutumikia jeshini pia kungeonyesha utiifu wa waumini wa Kanisa kwa nchi yao. Kapteni Allen alizungumza na wanaume, na 541 kati yao walijiunga na jeshi. Waliitwa Kikosi cha Mormoni. Brigham Young aliwaambia wanaume wawe askari bora katika jeshi. Walipaswa kuchukua Biblia na Kitabu cha Mormoni pamoja nao. Walipaswa kuwa nadhifu, wasafi, na wapole. Hawakupaswa kuapa au kucheza karata. Brigham Young aliwaambia wanaume hao watii amri za Mungu. Kama wangefanya hivyo, wasingelazimika kupigana. Mnamo Julai 1846 wanaume wa Kikosi cha Mormoni walienda pamoja na Kapteni Allen. Ilikuwa ni vigumu kwao kuwaacha wake zao na watoto katika wakati mgumu kama ule. Lakini Brigham Young alisema familia zao zingehudumiwa wakati watakapokuwa wameondoka. Kikosi cha Mormoni kilienda Fort Leavenworth, ambapo walipokea vifaa. Kisha walisafiri kusini magharibi kuelekea California. Familia za askari wachache zilikwenda pamoja nao. Ilikuwa vigumu sana kwa kikosi kusafiri. Barabara zilikuwa mbaya sana, na wakati mwingine magari ya kukokotwa na maksai yalikwama. Ilikuwa vigumu kupata maji ya kunywa. Wakati mwingine hapakuwa na miti ambapo wanaume wangeweza kupumzika katika kivuli. Baadhi ya watu walikuwa wagonjwa. Kapteni aliamua kwamba wanawake na watoto, pamoja na askari waliokuwa wagonjwa, walipaswa kwenda Colorado na kukaa katika mji wa Pueblo. Walikaa huko majira ya baridi. Majira ya joto yaliyofuata walikutana na waanzilishi ambao walikuwa wakivuka nyanda tambarare. Wengi wa askari katika kikosi waliendelea kusonga mbele. Wakati mwingine ilibidi wachimbe chini kwenye mchanga ili kupata maji. Hawakuwa na chakula cha kutosha. Mara nyingi hapakuwa na kuni za kuwasha moto, hivyo iliwabidi wanaume hao kuchoma magugu. Askari walikutana na Wahindi na watu wengine ambao walikuwa na chakula. Askari hawakuwa na fedha za kununua chakula, hivyo walibadilishana na Wahindi baadhi ya nguo zao kwa ajili ya chakula. Hatimaye Kikosi cha Mormoni kilifika kwenye milima yenye mwinuko mkali. Iliwabidi wanaume wafunge kamba kwenye magari ya kukokotwa na maksai na kuyavuta juu ya milima. Kisha wakaachilia magari ya kukokotwa na maksai chini upande wa pili. Siku moja baadhi ya mafahali mwitu waliwashambulia askari. Watu walipigana na mafahali na hatimaye kuwafukuzia mbali. Watatu kati ya askari waliumizwa. Hatimaye, baada ya kusonga mbele kwa zaidi ya maili 2,000, Kikosi cha Mormoni kilifika Bahari ya Pasifiki tarehe 29 Januari 1847. Wanaume walikuwa wamechoka sana, na nguo zao zilikuwa zimetatuka. Walikuwa na furaha safari yao ndefu ilikuwa imekwisha. Wanaume walifanya kazi California ili kumaliza mwaka wao wa huduma katika jeshi. Kisha waliruhusiwa kwenda kujiunga tena na familia zao. Kama vile Brigham Young alivyoahidi, wanaume wa Kikosi cha Mormoni hawakulazimika kupigana. Baadhi ya wanaume walibaki California. Wengi wao walikwenda kwenye Milima ya Miamba ili kuwa pamoja na familia zao na Watakatifu wengine ambao walikuwa wakiwasili huko. (Ona ramani kwenye ukurasa wa 234 kwa ajili ya safari za Kikosi cha Mormoni.)