Sura ya 31 Neno la Hekima Februari 1833 Joseph Smith alianzisha shule kwa ajili ya wanaume wa Kanisa. Ilikuwa ikiitwa Shule ya Manabii. Shule ilifanyika katika chumba ndani ya ghala ya Newel Whitney huko Kirtland, Ohio. Katika shule hii, Joseph na viongozi wengine wa Kanisa walifundishana kuhusu ukuhani, maandiko, na mambo mengine. Shule ilipaswa kuwasaidia wanaume kujiandaa kwa ajili ya uongozi wa Kanisa na huduma ya umisionari. Wengi wa wanaume walivuta kiko au biri, ambavyo vilijaza chumba kwa moshi. Baadhi ya wanaume walitafuna tumbaku na kutema mate juu ya sakafu, na kuifanya kuwa chafu sana. Emma Smith, mke wa Joseph, alisafisha chumba baada ya kila mkutano. Yeye na Joseph walisikitishwa kuhusu matumizi ya akina kaka ya tumbaku. Joseph alijiuliza ikiwa watu wanapaswa kuvuta sigara au kutafuna tumbaku. Joseph aliomba ili kujua kile kilichokuwa sahihi. Yesu alimpa ufunuo ulioitwa Neno la Hekima. Yesu alisema kwamba baadhi ya watu wanataka wengine wafanye mambo ambayo ni mabaya kwa miili yao. Katika Neno la Hekima, Yesu aliwaambia Watakatifu kuhusu vitu ambavyo ni vibaya kwa miili yao. Pia aliwaambia kuhusu vitu ambavyo ni vizuri kwa miili yao. Mafundisho na Maagano 89:1, 4 Yesu alisema kileo si kizuri kwa watu. Hawapaswi kunywa vinywaji vyenye kileo ndani yake. Kileo kinapaswa kutumika tu nje ya mwili. Mafundisho na Maagano 89:5–7 Yesu alisema tumbaku si nzuri kwa watu. Hawapaswi kuvuta sigara, biri, au kiko. Hawapaswi kutafuna tumbaku. Mafundisho na Maagano 89:8 Yesu alisema Watakatifu hawapaswi kunywa vinywaji vya moto kama vile chai na kahawa. Vinywaji hivi si vizuri kwa mwili. Mafundisho na Maagano 89:9 Yesu alisema mimea mingi na wanyama ni vizuri kwa watu kula. Watu wanapaswa kumshukuru Baba wa Mbinguni kwa chakula bora. Mafundisho na Maagano 89:11–12 Yesu alisema watu hawapaswi kula nyama kwa wingi. Mafundisho na Maagano 89:12 Bwana alisema nafaka ni nzuri kwa ajili ya mwili. Baadhi ya nafaka ni ngano, mchele, mahindi, na shayiri. Matunda na mboga pia ni nzuri kwa mwili. Mafundisho na Maagano 89:11, 14–17 Yesu aliahidi baraka kuu kwa wale ambao wanatii Neno la Hekima. Miili yao itakuwa na nguvu na afya njema kuliko kama hawakulitii. Akili zao pia zitakuwa zenye afya, na watapata hekima na hazina ya maarifa. Mafundisho na maagano 89:18–21