Sura ya 6 Joseph na Oliver Wanapewa Ukuhani Mei1 829 Joseph Smith na Oliver Cowdery walikuwa wakitafsiri Kitabu cha Mormoni. Walisoma juu ya ubatizo na walitaka kujua mengi zaidi kuhusu hilo. Joseph Smith—Historia ya 1:68 Joseph na Oliver waliamua kumwomba Mungu. Walikuwa na imani kwamba Yeye angewasaidia kujifunza ukweli. Mnamo 15 Mei 1829, walikwenda msituni na kuomba. Joseph Smith—Historia ya 1:68 Mjumbe wa mbinguni alikuja kwa Joseph na Oliver. Alikuwa ni Yohana Mbatizaji, aliyembatiza Yesu zamani. Mwanga mkali ulimzunguka kote. Joseph Smith—Historia ya 1:68, 72 Yohana Mbatizaji alikuwa amekuja kuwatunukia Joseph na Oliver Ukuhani wa Haruni. Ukuhani ni uwezo wa Mungu. Ukuhani wa Haruni unajumuisha mamlaka ya kubatiza watu. Mafundisho na Maagano 13; Joseph Smith—Historia ya 1:68–69 Yohana Mbatizaji aliwaambia Joseph na Oliver wabatizane. Joseph alimbatiza Oliver, na kisha Oliver akambatiza Joseph. Walishuka chini ya maji walipobatizwa. Joseph Smith—Historia ya 1:70–71 Zamani, Yohana Mbatizaji alikuwa amembatiza Yesu kwa njia hiyo hiyo. Yesu alikuwa ameshuka chini ya maji pale alipobatizwa. Mathayo 3:16 Joseph na Oliver walijawa na Roho Mtakatifu baada ya kubatizwa. Roho Mtakatifu aliwaambia Kanisa la kweli la Yesu Kristo punde lingekuwepo duniani tena. Joseph Smith—Historia ya 1:73 Joseph na Oliver waliwaambia marafiki zao wema kuwa walikuwa wamebatizwa. Pia waliwaambia kuhusu ukuhani. Lakini Joseph na Oliver hawakuwaambia watu wengine mara moja. Walijua kwamba baadhi ya watu wasingewaamini na wangewaletea matatizo. Joseph Smith—Historia ya 1:74–75 Baadaye, wajumbe wengine watatu wa mbinguni walikuja. Walikuwa Petro, Yakobo na Yohana, ambao walikuwa Mitume watatu wa mwanzo wa Yesu. Petro, Yakobo na Yohana waliwapa Joseph Smith na Oliver Cowdery Ukuhani wa Melkizedeki. Huu pia unaitwa ukuhani “mkubwa.” Mafundisho na Maagano 27:12; 84:19 Mara baada ya ukuhani kurejeshwa, wanaume waadilifu wangeweza kupewa mamlaka ya kusaidia kufanya kazi ya Mungu duniani. Wanaume wenye Ukuhani wa Melkizedeki wanaweza kuwa viongozi wa Kanisa. Wanaweza kutoa baraka kwa watu. Wanaweza pia kuwapa watu kipawa cha Roho Mtakatifu. Urejesho wa ukuhani ni baraka kubwa.