Siku tatu baadaye, Brigham Young na wengine waliosalia wa kundi lake wakatokeza juu ya milima na kutazama chini bondeni. Wakati Brigham Young alipoliona, alijua hapo ndipo mahali ambapo Bwana alitaka Watakatifu waishi. Alisema, “Hapa ni mahali sahihi. Songa mbele.” Watakatifu waliendesha magari yao ya kukokotwa na maksai kushuka bondeni. Ilikuwa tarehe 24 Julai 1847. Baada ya kusafiri maili 1,000 kuvuka tambarare na milima, Watakatifu hatimaye walikuwa wamepata mahali ambapo wangeweza kuishi. Walishukuru kwamba Mungu alikuwa amewaongoza mahali penye amani na usalama, ingawaje walijua kungekuwa na changamoto nyingi zaidi za kuzishinda.