Sura ya 56 Matatizo Zaidi kwa Watakatifu 1843–1844 Watu wengi walioishi karibu na Nauvoo hawakuwa waumini wa Kanisa. Wengi wao hawakuwapenda Watakatifu na walianza kuwasababishia matatizo. Baadhi ya watu walikusanyika pamoja katika magenge ya watu wenye fujo. Waliiba mifugo ya Watakatifu na kuchoma moto maghala yao na makazi yao. Walijaribu kuwafanya Watakatifu waondoke Nauvoo. Polisi na askari hawakuweza kuyazuia magenge hayo. Gavana asingeweza kuwasaidia Watakatifu. Joseph Smith alikuwa amewaambia Watakatifu katika Nauvoo kwamba wangepata matatizo. Alijua kwamba siku moja wangepaswa kuondoka Nauvoo na kwenda mbali ambapo hakuna yeyote ambaye angeweza kuwasumbua. Joseph Smith alikuwa na mkutano na Mitume na baadhi ya watu wengine. Aliwaambia kutafuta mahali ambapo Watakatifu wangeweza kuishi kama ingewabidi kuondoka Nauvoo. Joseph aliangalia ramani za nchi. Ramani zilionyesha mahali ambapo kulikuwa na milima mirefu na mabonde makubwa. Joseph alijua kuwa hapa pangekuwa mahali pazuri kwa ajili ya Watakatifu. Baadhi ya watu katika Nauvoo waliokuwa waumini wa Kanisa waligeuka dhidi ya Kanisa. Walimchukia Joseph Smith na walitaka kumuua. Walianzisha gazeti na kuandika mambo mabaya juu ya Joseph na Watakatifu. Viongozi wa mji huko Nauvoo walikarishwa kuhusu gazeti hilo. Kwa sababu lilichapisha uongo, viongozi hawa walihisi walikuwa na mamlaka ya kisheria ya kulisitisha. Baadhi ya wanaume walikwenda kwenye jengo la gazeti na kuchoma magazeti na kuharibu mtambo wa uchapishaji. Hii ilisababisha maadui wa Kanisa kuwa na hasira zaidi.