Sura ya 2 Ono la Kwanza la Joseph Smith 1820 Joseph Smith na familia yake walimwamini Mungu. Walisoma Biblia pamoja. Wazazi wa Joseph waliwafundisha watoto wao kuwa wema. Kulikuwa na makanisa mengi sehemu aliyoishi Joseph. Watu wote walitofautiana juu ya kanisa gani lilikuwa sahihi. Joseph hakujua ni kanisa gani la kujiunga nalo. Alitaka kujua ni Kanisa gani lilikuwa la kweli la Yesu Kristo. Joseph Smith—Historia ya 1:5–10 Siku moja wakati Joseph alipokuwa na umri wa miaka 14, alisoma katika Biblia kwamba tunapaswa kumwomba Mungu wakati tunapotaka kujua kitu. Joseph aliamua kuomba na kumwuliza Mungu ni kanisa gani angejiunga nalo. Joseph Smith—Historia ya 1:11–13; Yakobo 1:5 Katika siku nzuri ya majira ya kuchipua, Joseph alikwenda msituni karibu na nyumba yake. Alipiga magoti na kuomba kwa sauti. Alikuwa na imani ya kwamba Baba wa Mbinguni angejibu maombi yake. Joseph Smith—Historia ya 1:14–15 Shetani hakutaka Joseph aombe. Alijaribu kumzuia Joseph na kufanya giza kumzunguka. Joseph alikuwa na hofu na hakuweza kuzungumza. Joseph Smith—Historia ya 1:15 Lakini Joseph hakukoma kuomba. Shetani asingeweza kumzuia. Joseph Smith—Historia ya 1:16 Kisha Joseph alipata ono. Aliona mwanga wenye mng’aro mzuri, uliomzunguka kote. Aliwaona Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wakisimama juu yake angani. Baba wa Mbinguni alimwonyesha Yesu na akasema, “Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!” Joseph Smith—Historia ya 1:16–17. Joseph alimwuliza Yesu ni kanisa gani angejiunga nalo. Yesu alimwambia Joseph asijiunge na kanisa lolote kwani yote yalikuwa si sahihi. Hakuna hata moja lililokuwa kanisa Lake. Alimwambia Joseph mambo mengine mengi. Kisha ono likamalizika. Joseph Smith—Historia ya 1:18–20 Wakati Joseph aliporudi nyumbani, mama yake alimuuliza kama alikuwa sawa. Joseph alisema alikuwa sawa. Kisha akamwambia mama yake kuwa alikuwa ameona ono. Alimwambia kile alichojifunza katika ono lake. Joseph Smith—Historia ya 1:20 Joseph pia aliwaambia baadhi ya watu katika mji kuhusu ono lake. Watu hawakumwamini. Walisema alikuwa anasema uongo, na wakawa na hasira na wakawa wakatili kwake. Joseph Smith—Historia ya 1:21–23 Joseph daima alisema ukweli kuhusu ono lake. Alijua alikuwa amewaona Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Alijua kwamba hakuna kanisa lolote duniani lililokuwa la kweli. Joseph Smith—Historia ya 1:24–26