Sura ya 60 Watakatifu Wanaondoka Nauvoo Septemba 1845–Septemba 1846 Baada ya kifo cha Joseph Smith, magenge ya watu wenye fujo yalidhani Kanisa lingepotea. Lakini lilibakia imara chini ya uongozi wa Mitume, na Nauvoo iliendelea kukua. Hii ilisababisha magenge ya watu wenye fujo yajaribu hata kwa nguvu nyingi zaidi kuharibu Kanisa na kuwafukuza Watakatifu. Magenge ya watu wenye fujo yalichapisha uongo juu ya Watakatifu katika magazeti. Gavana wa Illinois hakuweza kuyazuia magenge ya watu wenye fujo. Watakatifu punde walitambua kwamba wasingekuwa na amani isipokuwa waondoke Nauvoo. Gavana alipendekeza waelekee mbali upande wa magharibi, ambapo wangekuwa mbali na maadui zao na wangeweza kuanzisha serikali yao wenyewe. Hatimaye Watakatifu walikubali kuondoka, lakini walihitaji muda ili kujitayarisha. Watakatifu walihitaji kupata chakula na mavazi kwa ajili ya safari. Pia walihitaji kutengeneza magari yaliyokokotwa na maksai, kununua ng’ombe dume na wanyama wengine, na kuuza makazi yao. Watakatifu walifanya kazi kwa bidii ili kujitayarisha kuondoka Nauvoo. Magenge ya watu wenye fujo hayakutaka kuwapa muda Watakatifu ili kujitayarisha. Waliiba vitu na kuchoma baadhi ya makazi. Watakatifu walipanga kuondoka mnamo Aprili 1846, lakini vitisho kutoka kwa maadui zao viliwasababisha kuanza kuondoka mnamo Februari, wakati ilipokuwa baridi kali. Watakatifu wanaweka vitu vyao kwenye magari ya kukokotwa na maksai. Kisha waliendesha magari ya kukokotwa na maksai kwenye mashua bapa na kuvuka Mto Mississippi. Karibu wiki mbili baada ya Watakatifu kuondoka Nauvoo, ilikuwa baridi sana kiasi kwamba mto uliganda. Baadhi ya Watakatifu waliendesha magari yao ya kukokotwa na maksai kuvuka mto juu ya barafu. Watakatifu walipiga kambi karibu na mto kwa siku chache. Baadhi yao hawakuwa na nguo za kutosha na walikuwa na baridi sana. Baadhi yao hawakuwa na chakula cha kutosha. Wale ambao walikuwa na chakula cha kutosha na nguo waligawana na watu wengine. Punde Watakatifu walisonga mbele na kutengeneza kambi nyingine. Brigham Young alichagua viongozi ambao waliwasaidia watu kujipanga na kujitayarisha kwa safari ya magharibi. Watakatifu waliokuwa wakisafiri kwenda magharibi waliitwa waanzilishi. Mnamo Machi 1846 waanzilishi walianza kusafiri magharibi kupitia Iowa. Maendeleo yao yalikuwa kidogo kwa sababu ya hali mbaya ya hewa, njia mbaya, na matatizo mengine. Brigham Young aliwatuma wanaume mbele ili kutafuta sehemu nzuri kwa ajili ya kambi zingine. Hawa watu walikata miti na kujenga nyumba za magogo. Pia walipanda mazao na kujenga madaraja katika mito. Walifanya iwe rahisi kwa waanzilishi kusafiri. Mnamo Juni 1846, karibu miezi minne baada ya kuondoka Nauvoo, kundi la kwanza la waanzilishi lilifanikiwa kusafiri kutoka Iowa mpaka Mto Missouri. Walisimama katika sehemu iliyoitwa Council Bluffs na kujenga kivuko cha mashua kwa ajili ya kuvuka mto. Watakatifu wengine punde walijiunga nao (ona ramani kwenye ukurasa wa 190). Wakati Watakatifu wengi walipoondoka Nauvoo mnamo Februari 1846, wengine wengi walibakia nyuma kwa muda mrefu kidogo. Baadhi yao walikuwa wameteuliwa kumalizia hekalu. Wengine walijaribu kuuza baadhi ya mali. Ilipofika mwezi Septemba, wengi wa Watakatifu walikuwa wameondoka katika mji huo. Watakatifu walipokuwa wakitoka Nauvoo, waliangalia nyuma ng’ambo ya mto na kuona mji wao mzuri, na hekalu juu ya mlima. Walihuzunika kuondoka, lakini walikuwa na furaha kwamba walikamilisha hekalu la Bwana. Wengi wa Watakatifu ambao waliondoka Nauvoo katika miezi ya baadaye walikuwa wagonjwa sana, masikini, au hawakuwa wamejiandaa kusafiri. Mamia yao walitawanyika kando ya ufuo wa mto na hawakuwa na makazi au walikuwa na chakula kidogo. Lakini Bwana aliwasaidia kwa kutuma makundi ya ndege wadogo walioitwa kware, ambao Watakatifu waliweza kuwakamata na kula. Wakati Brigham Young aliposikia juu ya matatizo ya Watakatifu hawa, aliwatuma baadhi ya wanaume kwenda kuwaokoa. Wanaume hawa waliwaokoa kutokana na njaa na kuwasaidia kusafiri kwenda Council Bluffs na maeneo mengine katika Iowa ambapo Watakatifu walikuwa wamepiga kambi.