Sura ya 16 Joseph Smith na Sidney Rigdon Wanajifunza kuhusu Sayuni 1830 Wakati Oliver Cowdery na marafiki zake walipokuwa katika misheni yao, walisimama karibu na Kirtland, Ohio. Walikutana na mtu mmoja aliyeitwa Sidney Rigdon, ambaye alikuwa kiongozi katika kanisa lingine. Wamisionari walimpa Sidney Rigdon nakala ya Kitabu cha Mormoni na kumfundisha injili. Sidney alisoma Kitabu cha Mormoni na kuomba kuhusu kitabu hicho. Baba wa Mbinguni alimwambia injili ilikuwa ya kweli, na Sidney alibatizwa. Sidney Rigdon aliwaambia waumini wa kanisa lake kuwasikiliza wamisionari, na wengi wao walifanya hivyo. Punde watu 1,000 walibatizwa katika Kirtland. Sidney Rigdon alitaka kukutana na Joseph Smith, hivyo alikwenda New York. Baada ya Sidney kuwasili, Joseph Smith alipokea ufunuo kwa ajili yake. Katika ufunuo, Yesu alisema Sidney Rigdon angefanya mambo makubwa. Angefundisha injili kwa watu wengi. Angewabatiza na kuwapa kipawa cha Roho Mtakatifu. Mafundisho na Maagano 35:4–6 Yesu pia alimwambia Joseph na Sidney kwamba baadhi ya sehemu za Biblia zilikuwa zimebadilishwa miaka mingi iliyopita. Sehemu zingine muhimu zilikuwa zimeondolewa. Yesu alisema Yeye angemfunulia Joseph Smith ni sehemu zipi za Biblia zingepaswa kurekebishwa. Sidney alipaswa kuandika marekebisho wakati Joseph akiyazungumza. Mafundisho na Maagano 35:20 Hadithi moja ambayo haijakamilika katika Biblia ni kuhusu Henoko, ambaye alikuwa nabii mkuu. Watu wake walikuwa wenye haki sana kiasi kwamba Bwana aliwaita Sayuni. Watu wa Henoko pia walijenga mji ulioitwa Sayuni. Katika Sayuni, watu walipendana na kujaliana. Hakuna mtu aliyekuwa masikini au aliyekuwa na huzuni. Musa 7:18–19 Kila mtu katika Sayuni alitii amri za Baba wa Mbinguni. Watu walikuwa wenye haki sana kiasi kwamba Bwana alikaa pamoja nao. Kisha akawatwaa watu wa Sayuni mbinguni ili waishi pamoja Naye. Musa 7:16, 69 Yesu alimwambia Joseph Smith kwamba Watakatifu walipaswa kujenga mji mwingine uitwao Sayuni. Mji ungekuwa mzuri. Hakuna watu wabaya ambao wangeishi huko. Wale ambao wangeishi katika mji huo wangependana na kuwa na furaha. Yesu alisema Yeye angekuja na kuishi pamoja nao. Mafundisho na Maagano 45:64–71; ona pia Musa 7:62–64