Sura ya 12 Misheni ya Samuel Smith Juni 1830 Samuel Smith alikuwa kaka mdogo wa Joseph Smith. Yesu alitaka Samuel aende misheni. Samuel Smith alikuwa mmisionari wa kwanza wa Kanisa. Samuel alikwenda kuwafundisha watu injili na kuwaambia kuhusu Kitabu cha Mormoni. Mnamo siku ya kwanza alisafiri maili 25, lakini watu walikuwa wakatili kwake na hawakutaka kumsikiliza. Wakati usiku ulipofika, Samuel alisimama kwenye hoteli. Alimwuliza mmiliki kama angependa kununua Kitabu cha Mormoni. Mmiliki aliuliza ni wapi Samuel alikipata kitabu hicho. Samuel alisema ndugu yake alikuwa amekitafsiri kutoka kwenye mabamba ya dhahabu. mmiliki alikuwa na hasira. Alisema Samuel alikuwa akidanganya na akamwambia atoke nje ya hoteli. Samuel Smith alikufa moyo. Usiku huo alilala chini ya mti wa tufaa. Asubuhi iliyofuata Samuel alikwenda kumuona John Greene, aliyekuwa kiongozi wa kanisa lingine. Bw. Greene hakutaka Kitabu cha Mormoni, lakini alikubali kuwauliza watu katika kanisa lake kama wangependa kununua nakala. Wakati Samuel aliporudi wiki tatu baadaye, hapakuwa na mauzo. Hata hivyo, mke wa Bw. Greene alisema alikuwa amekisoma kitabu. Misheni ya Samuel Smith ilikuwa ngumu. Aliporudi nyumbani, hakudhani kuwa alikuwa na mafanikio. Samwel hakujua kwa wakati huo kwamba kazi yake hatimaye ingesababisha watu wengi kujiunga na Kanisa, ikiwa ni pamoja na Bw. na Bi. Greene. Samuel pia alikuwa ameuza Kitabu cha Mormoni kwa mtu mmoja aliyeitwa Phineas Young. Phineas alisoma kitabu na akampa kaka yake, ambaye jina lake lilikuwa Brigham Young. Brigham Young alisoma Kitabu cha Mormoni na kuamini kilikuwa cha kweli. Phineas na Brigham Young waliwaambia baadhi ya marafiki kuhusu Kitabu cha Mormoni, na wao pia walikisoma na kuamini ni cha kweli. Baadaye, Phineas na Brigham Young na marafiki zao walijiunga na Kanisa. Ndani ya miaka michache, Brigham Young aliitwa kuwa Mtume. Miaka mingi baadaye alikuwa Rais wa Kanisa. Yeye pamoja na wengine walioongoka kupitia juhudi za Samuel Smith wakawa viongozi wakuu katika Kanisa.