Sura ya 32 Kanisa la Yesu Kristo katika Kirtland 1833–1834 Bwana alisema ya kwamba Joseph Smith anapaswa kuwa na wanaume wa kumsaidia kuongoza Kanisa. Wanaume hawa wangekuwa washauri wa Joseph. Bwana alifunua kuwa Sidney Rigdon na Frederick G. Williams wanapaswa kuwa washauri hawa. Mafundisho na Maagano 90:6 Mnamo Machi 1833, Joseph Smith aliwatawaza washauri wake katika mkutano mtakatifu huko Kirtland, Ohio. Joseph na washauri wake walikuwa Urais wa Kwanza wa Kanisa. Leo nabii aliye hai ndiye kiongozi wa Kanisa. Yeye na washauri wake ndio Urais wa Kwanza wa Kanisa. Yesu alimwambia Joseph Smith kwamba Watakatifu wanapaswa kujenga majengo mengi ya Kanisa. Jengo muhimu zaidi lingekuwa hekalu katika Kirtland. Watakatifu pia walihitajika kujenga kiwanda cha uchapishaji na mahali pa Urais wa Kwanza kufanya kazi. Mafundisho na Maagano 94; 95 Watakatifu walimtii Bwana na kuanza kujenga Hekalu la Kirtland. Ilikuwa kazi ngumu, na Watakatifu wote walihitajika kusaidia. Kadiri watu zaidi walivyojiunga na Kanisa, Yesu alimwambia Joseph Smith kuchagua viongozi zaidi. Alisema baba yake Joseph alipaswa kuwa patriaki wa Kanisa. Patriaki hutoa baraka maalum kwa Watakatifu. Leo kuna mapatriaki katika vigingi vingi vya Kanisa. Yesu pia alimwambia Joseph kuchagua wanaume kumi na wawili kutumikia katika baraza kuu. Wajumbe wa baraza kuu wanashikilia ofisi ya kuhani mkuu katika Ukuhani wa Melkizedeki. Mojawapo ya kazi zao ni kusaidia kutatua matatizo yanayoweza kutokea katika Kanisa. Mafundisho na Maagano 102 Mnamo Februari 1834, Joseph Smith alianzisha kigingi cha kwanza cha Kanisa. Kigingi ni waumini wengi wa Kanisa wanaoishi katika eneo moja. Watakatifu wote katika Kirtland walikuwa katika kigingi cha kwanza. Leo Kanisa lina maelfu ya vigingi.