Hadithi za Maandiko
Sura ya 4: Martin Harris na Kurasa Zilizopotea: 1827–1828


Sura ya 4

Martin Harris na Kurasa Zilizopotea

1827–1828

mabamba ya dhahabu
Joseph akitafsiri

Huko Pennsylvania, Joseph alianza kutafsiri maandishi yaliyokuwa kwenye mabamba ya dhahabu. Hakujua maandishi yalimaanisha nini, lakini alipotumia Urimu na Thumimu, Mungu alimsaidia kuelewa maneno.

Martin Harris akinakili

Martin Harris alienda Pennsylvania na kumsaidia Joseph kutafsiri. Wakati Joseph akitafsiri maneno kutoka kwenye mabamba ya dhahabu, Martin aliyaandika kwenye karatasi. Joseph na Martin walitafsiri kurasa 116 za Kitabu cha Mormoni.

Martin Harris akiomba muswada

Martin Harris alitaka kupeleka kurasa 116 nyumbani ili familia yake iweze kuziona. Joseph alimwuliza Bwana ikiwa Martin angeweza kuchukua kurasa hizo, lakini Bwana alisema hapana. Joseph aliuliza tena, lakini Bwana alisema tena hapana.

Joseph na Martin Harris

Martin bado alitaka kuzipeleka kurasa hizo nyumbani. Alimsihi Joseph amuulize Bwana kwa mara nyingine. Wakati huu Bwana alisema kwamba Martin angeweza kuchukua kurasa ikiwa angekubali kuzionyesha tu kwa mke wake na baadhi ya wanafamilia wengine wa familia yake.

Martin Harris akiwa na kurasa

Martin aliahidi kumtii Bwana. Alipeleka zile kurasa nyumbani na kuzionyesha kwa familia yake. Lakini kisha alivunja ahadi yake na kuzionyesha kurasa kwa watu wengine kadhaa.

Martin Harris

Baadaye Martin alikwenda kuchukua zile kurasa. Alitafuta kila mahali lakini hakuweza kuzipata. Kurasa zilikuwa zimepotea.

Joseph akitafakari

Baada ya wiki chache, Martin Harris alipokosa kurejea na zile kurasa, Joseph akawa na wasiwasi. Alikwenda New York ili kumtafuta Martin, ambaye alimwambia kwamba zile kurasa zilikuwa zimepotea. Joseph na Martin wote walijisikia vibaya sana.

Moroni akichukua mabamba

Joseph alirudi Pennsylvania, ambako aliomba kwa ajili ya kusamehewa. Moroni alitokea na kuchukua mabamba ya dhahabu.

Joseph akipokea mwongozo wa kiungu

Katika ufunuo, Bwana alimwambia Joseph kwamba hataweza kuruhusiwa kutafsiri kwa muda kwa sababu hakutii. Bwana pia alimfariji Joseph, akisema kazi Yake ingeendelea mbele na kwamba Joseph alikuwa bado amechaguliwa kufanya kazi kama atatubu.

watu waovu wakipanga njama

Yesu alimwambia Joseph kwamba Shetani alikuwa amewashawishi baadhi ya watu waovu kuchukua zile kurasa 116. Watu hawa walikuwa wanakwenda kubadilisha maneno ili watu wengine wasiamini Kitabu cha Mormoni. Yesu alisema Shetani na watu waovu wasingeweza kusimamisha kazi ya Mungu.

Joseph akiona taswira ya watu wakisoma kitabu

Joseph alitubu. Punde Moroni alirudisha mabamba ya dhahabu, na Bwana alimsamehe Joseph na kurejesha kipawa cha kutafsiri. Yesu alimwambia Joseph asiwe na wasiwasi kuhusu kurasa zilizopotea kwa sababu hadithi sawa na hizo ziliandikwa katika sehemu nyingine ya mabamba hayo ya dhahabu. Yesu alisema Joseph alipaswa kutafsiri sehemu nyingine ya mabamba. Yesu pia alisema watu wengi wangesoma Kitabu cha Mormoni na kujifunza kuhusu injili Yake.