Sura ya 27 Nabii Anaendelea na Kazi Yake Licha ya Mateso Machi 1832 Joseph Smith na Sidney Rigdon waliendelea kufanya marekebisho yenye mwongozo wa kiungu kwenye Biblia. Yesu alimfunulia Joseph Smith masahihisho yaliyopaswa kufanywa, na Sidney Rigdon aliyaandika (ona sura ya 16). Joseph Smith hakuelewa baadhi ya sehemu za Biblia. Aliomba kwa ajili ya uelewa, na Bwana alijibu. Mengi ya mafunuo katika Mafundisho na Maagano yalikuja kama majibu ya maswali ambayo Nabii alimwuliza Bwana wakati akitafsiri Biblia (ona, kwa mfano, Mafundisho na Maagano 76, 77, na 113). Yesu alikuwa na furaha kwa kazi ya Joseph. Joseph alikuwa nabii mkuu. Wakati huu, Joseph na Emma Smith walikuwa na watoto mapacha ambao waliishi kwa masaa machache tu. Marafiki wa Joseph na Emma pia walikuwa na watoto mapacha. Mama wa mapacha hawa alifariki, na baba yao aliwaruhusu Joseph na Emma kuwaasili. Usiku mmoja genge la watu wenye hasira walikwenda nyumbani kwa Joseph. Walivunja mlango na kuingia ndani. Joseph alikuwa amemshikilia mmoja wa watoto wadogo, ambaye alikuwa mgonjwa sana. Wanaume walimkamata Joseph na kumburuta hadi nje katika usiku wenye baridi. Mtoto alibaki peke yake, na siku tano baadaye alifariki. Watu walimsonga Joseph na kujaribu kummwagia sumu katika kinywa chake. Chupa ilivunja moja ya meno yake, na sumu ilimwunguza. Watu walirarua mavazi ya Joseph na kupaka lami kwenye ngozi yake. Walifunika lami kwa manyoya na kumpiga. Genge liliondoka, wakifikiri Joseph angekufa. Joseph alijaribu kusimama, lakini hakuweza. Alipumzika kwa muda, kisha akapata nguvu ya kutosha kutambaa kurudi ndani. Marafiki wa Joseph walisafisha lami kutoka kwenye mwili wake. Ilikuwa ni vigumu kuitoa lami. Ngozi yake ilikuwa imeungua na kuvimba. Siku iliyofuata ilikuwa Jumapili. Katika maumivu makali, Joseph alikwenda kanisani na kutoa hotuba. Baadhi ya watu katika genge walikuja kwenye mkutano na walishangaa kumwona Joseph. Nabii hakuwaruhusu kumzuia kufanya kazi ya Bwana.