“Novemba 15–21. Mafundisho na Maagano 133–134: ‘Jitayarisheni Kwa Ajili ya Ujio wa Bwana Harusi,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)
“Novemba 15–21. Mafundisho na Maagano 133–134,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2021
Novemba 15–21
Mafundisho na Maagano 133–134
“Jitayarisheni Kwa Ajili ya Ujio wa Bwana Harusi”
Fikiria mahitaji ya watoto unaowafundisha—wote wale wanaosoma na kujifunza nyumbani na wale ambao pengine hawafanyi hivyo. Je, ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia kufundishana kuhusu mambo wanayojifunza?
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Onesha picha uliyoitumia hivi karibuni katika somo la Msingi, na waalike watoto kusimulia kile wanachokumbuka kutokana na somo hilo.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Mafundisho na Maagano 133:19–21, 25
Yesu Kristo atakuja tena.
Katika sehemu ya 133, Bwana anaelezea Ujio Wake wa Pili na kuwaalika watu Wake kujitayarisha kwa ajili ya tukio hili tukufu. Je, utawezaje kuwasaidia watoto kutazamia kurudi kwa Mwokozi?
Shughuli Yamkini
-
Ficha picha ya Ujio wa Pili wa Mwokozi nyuma ya nguo, kama vile nguo hiyo ni pazia (unaweza kutumia picha katika muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia au Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 66). Waalike watoto kufanya zamu kusogeza “pazia” pembeni na kujifanya wanaangalia nje ya dirisha. Waombe waelezee namna ambavyo wangejisikia kama wangeangalia nje ya dirisha na kumwona Yesu akishuka chini kutoka mbinguni. Soma kifungu cha maneno “nendeni nje kumlaki” (mstari wa 19), na wasaidie watoto kurudia kifungu hicho cha maneno.
-
Chini ya kiti cha kila mtoto, ficha picha inayoonesha kitu fulani tunachoweza kufanya ili kujitayarisha kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Yesu Kristo (kama vile kusoma maandiko, kushiriki injili, au kuhudumia familia zetu). Acha watoto wazitafute picha hizo, na kuzungumzia kuhusu namna gani kufanya vitu hivi kunatusaidia sisi kuwa tayari kumlaki Mwokozi wakati Atakaporudi.
-
Imbeni pamoja wimbo kuhusu Ujio wa Pili, kama vile “When He Comes Again” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 82–83). Shiriki upendo wako kwa ajili ya Mwokozi na hisia zako kuhusu kurudi Kwake duniani. Waalike watoto kushiriki hisia zao pia.
Mafundisho na Magano 133:52–53
Yesu Kristo ni mwenye upendo na mkarimu.
Mistari hii inaelezea baadhi ya njia nyingi Bwana alizoonesha “upendo wa ukarimu” Wake kwa watu Wake. Je, ni kitu gani unaweza kufanya ili kuwasaidia watoto kuhisi upendo kwa Mwokozi kwao?
Shughuli Yamkini
-
Onesha picha ambayo inaonesha kwamba Yesu ni mwenye upendo na ni mkarimu (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 42, 47). Waombe watoto kueleza mambo mengine ambayo Yesu alifanya ili kuonesha upendo na ukarimu Wake. Soma kifungu cha maneno “watataja ukarimu wa Bwana wao” (mstari wa 52), na wasaidie watoto kufikiria njia wanazoweza kuwaambia wenzao kuhusu upendo wa Mwokozi.
-
Imbeni pamoja wimbo kuhusu upendo wa Mwokozi, kama vile “Jesu is Our Loving Friend” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 58). Toa ushuhuda wako wa jinsi ambavyo Mwokozi ameonesha upendo Wake kwako.
Bwana ananitaka nitii sheria.
Watoto wadogo mara nyingi wanazo kanuni za kufuata nyumbani, shuleni, na popote penginepo. Unaweza kuwasaidia kuelewa kwamba Bwana anategemea sisi tufuate masharti na sheria katika jumuiya zetu na taifa letu.
Shughuli Yamkini
-
Waalike watoto kucheza mchezo rahisi pasipo kufuata masharti yoyote, na kisha wacheze kwa kufuata masharti. Je, masharti yanatusaidiaje sisi? Elezea shukrani yako kwa ajili ya sheria za nchi?
-
Wasaidie watoto kurudia makala ya kumi na mbili ya imani. Sisitiza maneno muhimu, kama “kutii, kuheshimu, na kuzishika,” na zungumza na watoto kuhusu maneno hayo yanamaanisha nini. Waelezee kwa nini ni muhimu kutii sheria.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Mafundisho na Maagano 133:4–5, 14–15
Bwana ananitaka niwe safi.
Mafundisho na Maagano 133 inaweza kuwasaidia watoto kuelewa namna ya kujiweka safi kutokana na ushawishi wa ulimwengu unaowazunguka.
Shughuli Yamkini
-
Waalike watoto kusoma “Babeli, Babilonia” katika Mwongozo kwenye Maandiko (scriptures.ChurchofJesusChrist.org) ili kutafuta Babilonia ni nini na inawakilisha kitu gani. Kisha someni pamoja Mafundisho na Maagano 133:4–5, 14–15. Je, inamaanisha nini “tokeni katika Babilonia”? (mstari wa 5). Je, ni baadhi ya maeneo na hali gani Bwana anataka tukae mbali nazo? Je, tunaweza kufanya nini ili kuziepuka?
-
Weka alama kwenye upande mmoja wa chumba ambayo inasema “Sayuni,” na weka alama nyingine upande mwingine wa chumba ambayo inasema “Babilonia.” Andika kwenye kipande cha karatasi maneno kutoka Mafundisho na Maagano 133:4–5, 14–15 ambayo yanaelezea ama Sayuni au Babilonia (kama vile “uovu,” “safi,” au “angamizo”), na waalike watoto kuweka kila karatasi chini ya alama sahihi.
Mafundisho na Maagano 133:19–25, 46–52
Yesu atatawala juu ya dunia.
Mzee D. Todd alisema, “Ni muhimu sana kuuandaa ulimwengu kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Bwana Yesu Kristo” (“Kujiandaa kwa ajili ya Kurudi kwa Bwana,” Ensign au Liahona, Mei 2019, 81). Je, utawasaidiaje watoto kuelewa jinsi wanavyoweza kushiriki katika kazi hii muhimu sana ?
Shughuli Yamkini
-
Onesha picha kutoka muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia, na waalike watoto kutengeneza orodha ya mambo wanayojua kuhusu Ujio wa Pili wa Yesu Kristo. Kisha, kwa kutumia Mafundisho na Maagano 133:19–25, 46–52, waalike kuongeza mambo kwenye orodha yao. Toa ushuhuda wako kwamba Ujio wa Pili utakuwa siku ya shangwe kwa walio waadilifu.
-
Ili kuwasaidia watoto kuelewa mstari wa 19, zungumza nao kuhusu jinsi bibi harusi anavyoweza kujiandaa kwa ajili ya harusi yake (pengine mtu aliyeolewa au kuoa siku za hivi karibuni angeweza kusaidia katika mazungumzo haya). Je, ni kwa jinsi gani sisi ni kama bibi harusi anayejitayarisha “kwa ajili ya ujio wa Bwana harusi,” Yesu Kristo? Kama unafikiri ingekuwa yenye msaada, rejea pamoja na watoto mfano wa wale wanawali kumi (ona Mathayo 25:1–13). Kwa nini ni muhimu kujitayarisha kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Mwokozi? Je, tunaweza kufanya nini sasa ili kujitayarisha?
Bwana ananitaka nitii sheria.
Ingawa kuna miundo tofauti ya serikali kote ulimwenguni, Bwana anatutaka sisi “tuzikubali na kuziunga mkono … serikali ambamo ndani yake [sisi] tunaishi” (Mafundisho na Maagano 134:5).
Shughuli Yamkini
-
Waalike watoto kuorodhesha masharti au sheria wanazotii. Je, maisha yangekuwaje kama kusingekuwa na mtu anayetii sheria? Soma Mafundisho na Maagano 134:1–2 pamoja na watoto, ukiwasaidia kuelewa neno lolote au kifungu cha maneno wasichokielewa. Je, ni kwa nini Bwana anatutaka kuwa na serikali na sheria?
-
Andika kila neno au kifungu cha maneno kutoka makala ya kumi na moja na kumi na mbili ya imani kwenye vipande viwili tofauti vya karatasi. Changanya karatasi hizo, na waombe watoto kufanya kazi pamoja ya kuziweka katika mpangilio sahihi. Tunawezaje kuonesha kwamba tunaamini kile makala hizi za imani zinachotufundisha?
Himiza Kujifunza Nyumbani
Mpe kila mtoto swali la kumwuliza mwanafamilia afikapo nyumbani. Kwa mfano, kama mmejifunza kuhusu Ujio wa Pili wa Mwokozi, mtoto anaweza kuuliza, “Tunaweza kufanya nini ili kujitayarisha kwa kuja tena kwa Yesu?”