“Wewe ni Mwalimu wa Watoto,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)
“Wewe ni Mwalimu wa Watoto,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2021
Wewe ni Mwalimu wa Watoto
Umeitwa na Mungu ili kuwapenda na kuwafundisha watoto Wake katika njia ya Mwokozi. Umesimikwa katika wito huu kwa mamlaka ya ukuhani Wake mtakatifu. Hata kama wewe si mwalimu mwenye uzoefu, unapoishi kwa kustahili, kusali kila siku, na kujifunza maandiko, Baba wa Mbinguni atakupatia ushawishi na nguvu ya Roho Mtakatifu ili kukusaidia kufanikiwa (ona 2 Nefi 33:1).
Wale waliowekwa chini ya uangalizi wako ni watoto wa Baba wa Mbinguni, na Yeye anajua kile wanachohitaji na jinsi ya kuwafikia vizuri zaidi. Kupitia Roho Mtakatifu, Mungu atakuongoza wakati wa maandalizi yako na wakati unapofundisha. Atakufunulia kile unachopaswa kusema na kile unachopaswa kufanya (ona 2 Nefi 32:5).
Katika nyanja zote za maisha yao, watoto hawa wa thamani wanaendelea kufyonza habari, kutengeneza na kusafisha maoni yao, na kufanya na kushiriki uvumbuzi. Hii ni kweli hasa kwa injili, kwani watoto wapo tayari na wana nia ya kujifunza kweli zake rahisi. Imani yao katika mambo ya kiroho ni imara na safi, na wanaona kila wakati kama fursa ya kujifunza. Kwa hiyari wako tayari kutenda juu ya yale waliyojifunza, hata kama ufahamu wao bado haujakamilika. Hivi ndivyo jinsi sote tunavyopaswa kupokea injili. Kama Mwokozi alivyofundisha, “Mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hauingii kamwe” (Luka 18:17).
Mwito wa kufundisha watoto ni wajibu mtakatifu, na ni kawaida kuhisi kuzidiwa wakati mwingine. Lakini kumbuka kwamba Baba yako wa Mbinguni amekuita, na Yeye hatakuacha kamwe. Hii ni kazi ya Bwana, na unapohudumu “kwa moyo wako wote, uwezo, akili na nguvu” (Mafundisho na Maagano 4:2), Atakuza uwezo wako, vipawa, na vipaji, na huduma yako itabariki maisha ya watoto unaowafundisha.