“Kukidhi Mahitaji ya Watoto Wadogo,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)
“Kukidhi Mahitaji ya Watoto Wadogo,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2021
Kukidhi Mahitaji ya Watoto Wadogo
Watoto wako tayari na wana nia ya kujifunza injili ikiwa itawasilishwa katika njia wanayoweza kuelewa. Hususani kama unafundisha watoto wadogo, fikiria kutumia aina zifuatazo za shughuli ili kuwasaidia kujifunza.
-
Imba. Nyimbo za Kanisa na nyimbo kutoka Kitabu cha Nyimbo za Watoto hufundisha mafundisho kwa nguvu zaidi. Tumia kielezo cha mada kilicho nyuma ya Kitabu cha Nyimbo za Watoto ili kutafuta nyimbo ambazo zinahusiana na kanuni za injili unazofundisha. Wasaidie watoto kuhusisha ujumbe wa nyimbo na maisha yao. Kwa mfano, unaweza kuuliza maswali kuhusu maneno au vipengele katika maneno ya wimbo. Mbali na kuimba, watoto wanaweza kufanya vitendo vinavyoendana na nyimbo au kusikiliza tu nyimbo kama muziki wa chinichini wakati wanafanya shughuli nyingine kwenye ukurasa wa shughuli.
-
Sikiliza au igiza hadithi. Watoto wadogo wanapenda hadithi, zote za kuhadithia na kusikiliza. Simulia hadithi kutoka kwenye maandiko, kutoka katika maisha yako, kutoka kwenye historia ya Kanisa, au kutoka kwenye magazeti ya Kanisa, na acha watoto wasimulie hadithi kutoka katika maisha yao. Tafuta njia za kuwashirikisha katika kusimulia hadithi. Wanaweza kushika picha au vitu, kuchora picha ya kile wanachosikia, kuigiza hadithi, au kusaidia kusimulia hadithi. Wasaidie watoto kutambua kweli za injili katika hadithi unazowasimulia.
-
Soma andiko. Watoto wadogo wanaweza kushindwa kusoma vizuri, lakini bado unaweza kuwahusisha katika kujifunza kutoka kwenye maandiko. Unaweza kuhitaji kuzingatia mstari mmoja, kifungu cha maneno muhimu, au neno. Unaposoma maandiko kwa sauti, unaweza kuwaalika watoto kusimama au kuinua mikono yao wakati wanaposikia neno fulani au kifungu cha maneno unachotaka kukizingatia. Wanaweza hata kukariri vifungu vifupi vya maneno kutoka katika maandiko ikiwa watavirudia mara kadhaa. Wanaposikia neno la Mungu, watamsikia Roho.
-
Changamka. Kwa sababu watoto wadogo mara nyingi wana nguvu, panga njia ya kuwawezesha kuzunguka zunguka—kuandamana, kurukaruka, kuinama, kutembea, na vitendo vingine vinavyohusiana na kanuni au hadithi unayofundisha. Matendo haya yanaweza pia kuwa ya ufanisi wakati mnaimba pamoja.
-
Tazama picha au angalia video. Unapowaonesha watoto picha au video zinazohusiana na kanuni ya injili au hadithi ya maandiko, waulize maswali ambayo yanawasaidia kujifunza kutoka kwenye kile wanachokiona. Kwa mfano, ungeweza kuuliza, “Je, ni nini kinatokea katika picha au video hii?” au “kinakufanya ujisikie namna gani?” The Gospel Library app, medialibrary.ChurchofJesusChrist.org, na children.ChurchofJesusChrist.org ni maeneo mazuri ya kutafutia video.
-
Elezea uzoefu na ushuhuda. Watoto wadogo wanaweza wasiwe na mengi ya kuelezea kama watoto wakubwa wanavyofanya, lakini ikiwa utawapa mwongozo maalum, wanaweza kuelezea uzoefu wao na shuhuda zao kuhusu kile wanachojifunza.
-
Buni. Watoto wanaweza kujenga, kuchora, au kupaka rangi kitu kinachohusiana na hadithi au kanuni wanayojifunza. Wahimize kupeleka ubunifu wao nyumbani na kushirikiana na wanafamilia ili kuwasaidia watoto kukumbuka yale waliyojifunza.
-
Shiriki katika masomo ya vitendo. Somo rahisi la kitendo linaweza kuwasaidia watoto kuelewa kanuni ya injili ambayo ni ngumu kwao kuielewa. Wakati unapotumia masomo ya vitendo, tafuta njia za kuwafanya watoto kushiriki. Watajifunza zaidi kutokana na tukio la kuchangamana kuliko kuangalia onyesho tu.
-
Igiza‑Nafasi. Watoto wanapoigiza-nafasi ya aina fulani watakayokutana nayo katika maisha halisi, wanaelewa vizuri zaidi jinsi kanuni ya injili inavyohusika kwenye maisha yao.
-
Rudia shughuli. Watoto wadogo wanaweza kuhitaji kusikia mawazo mara nyingi ili kuyaelewa. Usiogope kurudia hadithi au shughuli mara nyingi, hata wakati wa somo hilo hilo. Kwa mfano, unaweza kusimulia hadithi ya maandiko mara kadhaa kwa njia tofauti wakati wa somo—kwa kusoma kutoka kwenye maandiko, kufupisha kwa maneno yako mwenyewe, kuonesha video, kuwaruhusu watoto wakusaidie kusimulia hadithi hiyo, kuwaalika kuigiza hadithi hiyo, na kadhalika. Ikiwa shughuli iliyotumiwa katika darasa inarudiwa nyumbani pia, marudio yatawasaidia watoto kujifunza na kukumbuka.
-
Changamana na wengine. Watoto wanajenga stadi za kijamii na mara nyingi wanafurahia kujifunza na kucheza na rika lao. Watengenezee fursa za kuelezea, kupeana zamu, na kushirikiana wakati wanajifunza.
-
Shiriki katika shughuli tofauti tofauti. Watoto wadogo kwa kufanana sana huwa na usikivu wa muda mfupi, na wana mitindo tofauti ya kujifunza. Tumia shughuli mbalimbali, na uwe makini na ishara zinazoonesha kuwa watoto wanahitaji mabadiliko ya mwendo. Kwa mfano, huenda ukahitaji kubadilisha mara kwa mara kati ya shughuli za ukimya na za kuchangamka.
Sehemu ya jukumu lako kama mwalimu wa watoto wadogo—katika nyongeza ya kufundisha kanuni za injili—ni kuwasaidia watoto kujifunza jinsi ya kushiriki kwa namna inayofaa katika darasa la Kanisa. Kwa mfano, wanaweza kuhitaji kujifunza kuhusu kupeana zamu, kuelezea, kuwaheshimu wengine, na kadhalika. Walimu wengine hutengeneza chati zenye majukumu kwa kila mtoto kushiriki katika darasa kwa namna fulani (kama vile kusema sala, kushikilia picha, au kupitisha karatasi). Majukumu yanaweza kubadilika kila wiki. Hii huwasaidia watoto kupeana zamu na kuzingatia tabia sahihi ya darasa.
Watoto—hasa watoto wadogo—mara nyingi hufaidika na utaratibu wa kawaida, unaotabirika. Kwa sababu watoto wadogo wana kiwango cha chini cha usikivu na wakati mwingine hupata shida kufokasi kwa kipindi chote cha darasa, ni vizuri zaidi ikiwa utaratibu huu unahusisha mabadiliko ya mara kwa mara kutoka kwenye aina moja ya shughuli hadi nyingine. Kwa mfano, utaratibu wako wa darasa unaweza kujumuisha mapumziko ya mara kwa mara ili kucheza mchezo, kupaka rangi picha, kuimba wimbo, na kadhalika.