Agano Jipya 2023
Novemba 13–19. Yakobo: “Iweni Watendaji wa Neno na Si Wasikiaji Tu”


“Novemba 13–19. Yakobo ‘Iweni Watendaji wa Neno, wala Si Wasikiaji Tu’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Agano Jipya 2023 (2021)

“Novemba 13–19. Yakobo,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2023

kijana akisafisha ukuta

Novemba 13–19

Yakobo

“Iweni Watendaji wa Neno, Wala Si Wasikiaji Tu”

Waraka wa Yakobo una kweli nyingi ambazo zinaweza kuwabariki watoto unaowafundisha. Mfuate Roho ili kuamua kweli zipi utashiriki nao. Mawazo yaliyoko katika muhtasari huu yanaweza kusaidia.

ikoni ya kushiriki

Alika Kushiriki

Waalike watoto kushiriki kanuni ya injili wanayokumbuka kujifunza pamoja na familia zao wakati wa wiki iliyopita au kutoka darasa lao la Msingi Jumapili iliyopita. Baada ya kila mtoto kushiriki, muombe mtoto mwingine katika darasa kufanya muhtasari wa yale waliyoshiriki.

ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo

Yakobo 1:5–6

Ninaweza kumwomba Baba wa Mbinguni kunisaidia kujifunza kile kilicho cha kweli.

Wasaidie watoto unaowafundisha kuelewa kwamba wanaweza kumgeukia Baba wa Mbinguni kwa ajili ya kupata hekima. Kufanya hivyo kutawabariki sana wanapokabiliwa na maswali magumu.

Shughuli Yamkini

  • Wasaidie watoto kurudia kirai “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu”(Yakobo 1:5). Je, tunamwulizaje Mungu maswali? Je, Yeye hutujibu kwa namna gani?

  • Onesha picha ya Ono la Kwanza (Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 90), au onesha video ya “Joseph Smith’s First Vision” (ChurchofJesusChrist.org). Elezea jinsi kusoma Yakobo 1:5 kulimshawishi Joseph Smith kumwomba Baba wa Mbinguni ili amsaidie na swali hilo (ona Joseph Smith—Historia ya 1:1–20). Toa ushuhuda wako kwamba Mungu hujibu maombi, na ushuhudie kwamba watoto wanaweza kuomba Kwake wanapokuwa na maswali. Waache watoto wachore picha zao wenyewe za Joseph Smith akisoma Yakobo 1:5 na akiomba kwa Baba wa Mbinguni.

Yakobo 3:1–13

Ninaweza kusema kwa ukarimu.

Kama Yakobo alivyoshuhudia, kujifunza kusema maneno ya ukarimu tu kwa wengine kutatusaidia sisi kuwa kama Yesu Kristo (ona Yakobo 3:2).

Shughuli Yamkini

  • Onyesha picha za kitu kitamu na kitu kichachu. Wasaidie watoto kuelewa kwamba Baba wa Mbinguni ametuomba tutumie ndimi zetu kusema mambo matamu (au ya ukarimu) na siyo mambo machachu (au yasiyo ya ukarimu) (ona Yakobo 3:10). Wasaidie kufikiria juu ya mifano ya mambo mazuri tunayoweza kusema kwa wengine.

  • Mpe kila mtoto mchoro rahisi wa mtu akizungumza. Waalike watoto wauinue juu unaposema jambo zuri tunaloweza kufanya kwa ndimi zetu (kama vile kusema ukweli, tunaposifia na kutoa msaada kwa mtu) na kuushusha chini unaposema kitu ambacho hatupaswi kufanya na ndimi zetu (kama vile kusema uongo, kuwaita watu majina mabaya na kukataa kutii mzazi).

  • Wekea mkazo ujumbe wa Yakobo 3:1–13 kwa kuimba pamoja wimbo kuhusu kuwa mkarimu, kama vile “Kindness Begins with Me” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 145).

Yakobo 5:7–11.

Kupokea baraka za Baba wa Mbinguni kunahitaji subira.

Subira siku zote haiji yenyewe, hususani kwa watoto. Fikiria jinsi unavyoweza kuutumia ushauri wa Yakobo ili kuwasaidia watoto unaowafundisha kujifunza subira.

Shughuli Yamkini

  • Wasaidie watoto kufikiria nyakati walipokuwa hawana budi kusubiria kitu ambacho kwa hakika walikitaka. Shiriki uzoefu wako wakati ulipotakiwa kusubiri. Waeleze kwamba kusubiri kitu fulani tunachokitaka bila kulalamika huitwa kuwa na subira.

  • Fanya muhtasari wa Yakobo 5:7 kwa maneno yako, na onyesha picha ya mbegu au mche. Kwa nini tunahitaji subira tunapopanda mmea? Ni nini kingetokea kama tungejaribu kuuvuta mche kuufanya ukue haraka? Ungetaka pia kuzungumza na watoto kuhusu kile inachomaanisha kuwa na subira na wengine na kwetu wenyewe. Shuhudia kwamba Mungu anaweza kutusaidia kuwa wenye subira.

  • Elezea hadithi ya Ayubu, ambaye ametajwa katika Yakobo 5:11 kama mfano wa subira (ona “Ayubu,” katika Hadithi za Agano la Kale, au video inayofanana nayo katika ChurchofJesusChrist.org). Ni kwa jinsi gani Ayubu alibarikiwa kwa kuwa na subira?

ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa

Yakobo 1:5–6

Baba wa Mbinguni atanisaidia kujifunza ukweli kama nitatafuta msaada Wake.

Watoto unaowafundisha wana miaka michache tu kufikia ule wa Joseph Smith aliposoma Yakobo 1:5 na alipata mwongozo wa kiungu wa kumwendea Baba wa Mbinguni katika sala. Fikiria jinsi unavyoweza kuwasaidia watoto unaowafundisha kujenga imani yao kwamba Mungu atawasaidia wanapopungukiwa na hekima.

Shughuli Yamkini

  • Waombe watoto kukusimulia hadithi ya Ono la Kwanza la Joseph Smith kwa maneno yao wenyewe (ona Joseph Smith—Historia ya 1:5-20; ona pia video “Joseph Smith’s First Vision” kwenye ChurchofJesusChrist.org). Je, ni kwa jinsi gani kusoma Yakobo 1:5 kulimsaidia Joseph? Wasaidie watoto kufikiria mifano mingine ya watu katika maandiko waliopokea jibu kwa sala zao, kama vile Nefi (ona 1 Nefi 11:1–6] na kaka wa Yaredi (ona Etheri 2:18–3:9). Je, ni mambo gani tunaweza kumwuliza Baba wa Mbinguni katika sala?

  • Soma pamoja na watoto Joseph Smith—Historia ya 1:10-14. Waalike watoto kutafuta vitu Joseph Smith alifanya ili kupokea majibu kwa maswali yake. Tunawezaje kufuata mfano wa Joseph wakati tunapokuwa na maswali?

Yakobo 1:22–27; 2:14–26

“Imani pasipo matendo imekufa.”

Utawezaje kuwasaidia watoto kuona uhusiano kati ya kile wanachoamini na kile wanachofanya?

Shughuli Yamkini

  • Waonyeshe watoto tochi bila betri, penseli bila risasi au kitu kingine ambacho hakifai au “kimekufa.” Waombe watoto kusoma Yakobo 2:14–17. Ni kwa jinsi gani vitu hivi vinafafanua kwa mfano ukweli wa mistari hii?

  • Waalike baadhi ya watoto wasome kimya kimya Yakobo 1:22–27 na wengine wasome 2:14–18. Kisha waombe kushiriki kile wanachoweza kufanya kuonyesha kwamba wao ni watendaji wa neno. Kwa mfano, ni kwa jinsi gani wao wanalishika agano lao la ubatizo? Je, wanamjua mtu aliye mgonjwa au mpweke ambaye wanaweza kumtembelea? Ni jinsi gani wanaweza kuhudumia familia zao zaidi? Ungeweza pia kuwakumbusha juu ya maneno ambayo yawezekana wameyasikia katika mkutano wa sakramenti leo. Tunawezaje kuwa watendaji wa maneno haya?

Ibrahimu akisali nje ya hema lake

“Ibrahimu alimwamini Mungu” (Yakobo 2:23). Ibrahimu katika Nyanda za Mamre, na Grant Romney Clawson

Yakobo 3:1–13

Ninaweza kuchagua kuongea kwa ukarimu.

Maneno tunayosemezana mmoja kwa mwingine yanaweza kuonekana sio muhimu, lakini kama Yakobo alivyoshuhudia, yanaweza kuwa na ushawishi mkubwa, kwa mema au ubaya.

Shughuli Yamkini

  • Je, kuna mtu yoyote katika kata, pengine mmoja wa watoto unaowafundisha, aliyewahi kufanya kazi na farasi au anafahamu chochote kuhusu boti? Ungeweza kumwalika aje kutoa utambuzi kuhusu mafundisho ya Yakobo katika Yakobo 3:3–4 kuhusu kutumia maneno ya ukarimu. Au toa ufahamu wako mwenyewe. Tunajifunza nini kuhusu kudhibiti ndimi zetu kutokana na mifano hii?

  • Waalike watoto wasome Yakobo 3:1–13 na kuchora picha ya kitu wanachokipata kinachofundisha kuhusu kudhibiti ndimi zetu. Wape muda wa kushiriki picha zao na kile walichojifunza. Imbeni pamoja wimbo kuhusu kutumia maneno ya ukarimu, kama vile “Let Us All Speak Kind Words” (Nyimbo za Kanisa, na. 232).

  • Baada ya kurejelea Yakobo 3:1–13 kwa pamoja, rejelea viwango kwa ajili ya lugha katika Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana ([kijitabu, 2022], 12). Wasaidie watoto kuweka lengo la kuboresha njia wanayoongea na wengine, na wahimize kumwomba Baba wa Mbinguni awasaidie kufikia lengo hili.

ikoni ya kujifunza

Himiza Kujifunza Nyumbani

Waalike watoto kufanya kitu fulani wiki hii ili kufanyia kazi kile walichojifunza darasani, kama kumwomba Baba wa Mbinguni wakiwa na swali au wanapojaribu kuwa na subira zaidi. Waombe kushiriki uzoefu wao katika darasa lijalo.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Wasaidie watoto kujishughulisha. “Unapowafundisha watoto, waruhusu kujenga, kuchora, kupaka rangi, kuandika na kubuni. Vitu hivi ni zaidi ya shughuli za kufurahisha—ni vya muhimu katika kujifunza” (Kufundisha katika Njia ya Mwokozi25).