“Novemba 20–26. 1 na 2 Petro: ‘Furahini kwa Shangwe isiyoelezeka Yenye Utukufu’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Agano Jipya 2023 (2021)
“Novemba 20–26. 1 na 2 Petro,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2023
Novemba 20–26
1 na 2 Petro
“Furahini kwa Shangwe Isiyoelezeka na kwa Utimilifu wa Utukufu”
Anza kujifunza kwako 1 na 2 Petro kwa sala. Kumbuka kwamba maandalizi bora ya kufundisha yatakuja kwa njia ya uzoefu wako wa kujifunza wewe binafsi na kifamilia.
Alika Kushiriki
Onyesha picha ya Petro katika muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia, na waalike watoto wakusimulie kitu wanachojua kuhusu Petro. Wakumbushe kwamba Petro alikuwa kiongozi wa Kanisa baada ya Yesu kufufuka, na eleza kwamba 1 Petro na 2 Petro ni barua kutoka kwake kwenda kwa waumini wa Kanisa katika siku yake.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Ninaweza kuwa na furaha hata wakati wa shida.
Fikiria jinsi unavyoweza kufundisha mistari hii katika njia ambazo zitawasaidia watoto kumgeukia Mwokozi wakati wanapokabiliwa na shida.
Shughuli Yamkini
-
Wasaidie watoto kufikiria mifano ya mambo magumu ambayo Yesu aliyapitia, kama vile kukejeliwa au kufanyiwa mzaha. Elezea kwamba sisi tutakuwa na nyakati ngumu katika maisha yetu. Someni 1 Petro 1:6–7; 3:14 kwa pamoja, na shiriki uzoefu ambapo wewe ulikabiliwa na “jaribu la imani yako” na Mwokozi alikusaidia kupata shangwe. Au unaweza kusimulia sala ya Nabii Joseph Smith katika Jela la Liberty na faraja ambayo Mungu alimpa (ona Mafundisho na Maagano 121:1–8; 123:17).
-
Onyesha picha ambayo inamwonyesha Yesu na watu wengine ( Kitabu cha Sanaa ya Injili kinazo picha nyingi; vivyo hivyo Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia). Waombe watoto wamtafute Yesu katika hiyo picha. Shuhudia kwamba kama tutamtegemea Mwokozi, Yeye anaweza kutusaidia kupata shangwe katika maisha yetu.
Baba wa Mbinguni ananitaka mimi niwe mfano kwa wengine.
Petro alifundisha kwamba sisi ni “watu wa Mungu” na kwamba kazi zetu njema zinaweza “kumtukuza Mungu.”
Shughuli Yamkini
-
Elezea vitu ambavyo vinajitokeza kutoka kwenye mazingira yao, au onyesha picha za vitu hivyo. Kwa mfano, hekalu limejitokeza kutoka kwenye majengo yaliyolizunguka au mlima unainuka juu ya bonde. Eleza kwamba tunapotii amri, tunajitokeza na watu wengine wanaweza kuona mifano yetu. Ongelea kuhusu baadhi ya “kazi njema” ambazo umewaona watoto wakifanya. Eleza kwamba kazi njema kama hizi “zinamtukuza Mungu”—zinawasaidia wengine kuhisi upendo zaidi kwa Mungu na kutamani kumhudumia Yeye.
-
Kamilisha ukurasa wa shughuli pamoja na watoto. Je, ni kwa jinsi gani watu waliowaona katika picha wanamtukuza Mungu?
Roho katika ulimwengu wa roho wanajifunza kuhusu injili.
Baada ya kufa, Yesu alikwenda ulimwengu wa roho na aliwatuma roho wenye haki kuwafundisha roho wengine ambao walikuwa bado hawajaikubali injili.
Shughuli Yamkini
-
Waeleze watoto kuhusu mtu fulani unayemjua kuwa amefariki dunia. Eleza kuwa watu wanapokufa, roho zao zinaacha miili yao na kwenda ulimwengu wa roho. Soma 1 Petro 3:19 na uelezee kwamba wakati Yesu alipokufa, alikwenda kutembelea ulimwengu wa roho. Huko, aliwaomba roho wenye haki kufundisha injili kwa roho wengine ambao walikuwa bado hawajaikubali injili (ona Mafundisho na Maagano 138:30).
-
Onyesha picha ya hekalu. Elezea watoto kwamba watakapo kuwa wakubwa vya kutosha, wataweza kwenda hekaluni na kubatizwa kwa niaba ya mababu zao ambao hawakubatizwa wakati walipokuwa duniani. Wasaidie watoto kujaza chati ya mti wa familia (ona mfano kwenye “Kurasa za Kupaka Rangi za Historia ya Familia,” ChurchofJesusChrist.org).
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Ninaweza kupata furaha na amani hata katika wakati mgumu.
Watoto unaowafundisha yawezekana wamewahi kupatwa na tukio la kutaniwa au kukejeliwa kwa sababu ya kile wanachoamini. Mistari hii inaweza kuwasaidia nyakati hizo.
Shughuli Yamkini
-
Fanya muhtasari wa hadithi chache kuhusu Yesu akiwa anateswa, au waalike watoto wazisome—ona, kwa mfano, Mathayo 12:9–14 au Luka 22:47–54. Waulize watoto kama wamewahi wakati wowote kutaniwa au kukejeliwa kwa sababu wanaishi mafundisho ya Yesu Kristo. Iliwafanya wajisikie vipi? Kisha someni pamoja 1 Petro 3:12–14; 4:13–14, 16, na waombe watoto kutafuta kile Petro alichosema kuhusu mateso “kwa ajili ya haki.” Je, ni kwa nini bado tunaweza kuwa na furaha wakati watu wengine wanatukejeli kwa ajili ya kufanya kile kilicho sahihi?
-
Elezea uzoefu wako wakati alipopata furaha au amani wakati wa majaribu, au elezea jinsi gani Nabii Joseph Smith alipata amani wakati akiwa katika Jela la Liberty (ona Mafundisha na Maagano 121:1–8; 123:17). Je, ni kwa jinsi gani tunaweza kupata shangwe na amani wakati wa majaribu yetu?
Ninaweza daima kuwa tayari kushiriki injili.
Watoto unaowafundisha watakuwa na fursa nyingi katika maisha yao yote za kujibu maswali kutoka kwa watu wengine kuhusu imani yao. Tafakari kile unachoweza kufanya ili kuwasaidia “kuwa tayari wakati wote kutoa jibu.”
Shughuli Yamkini
-
Simulia kuhusu wakati ambapo mtu fulani alikuuliza swali kuhusu Kanisa, na eleza kama ulijisikia upo tayari kujibu. Waombe watoto kuzungumza kuhusu wakati wo wote watu walipowauliza maswali kuhusu Kanisa. Someni pamoja 1 Petro 3:15. Tunawezaje kufuata ushauri wa Petro katika mstari huu?
-
Wasaidie watoto kufikiria juu ya maswali machache watu wanayoweza kuuliza kuhusu Yesu Kristo au Kanisa Lake. Waache watoto wafanye zamu kuelezea jinsi ambavyo wangeweza kujibu maswali haya ili waweze “daima kuwa tayari.” Makala ya Imani yanatoa kweli zilizo rahisi ambazo watoto wanaweza kutumia kujibu maswali kuhusu Kanisa.
Roho katika ulimwengu wa roho wanajifunza kuhusu injili.
Wenye haki wanapokufa, wanakwenda ulimwengu wa roho kufundisha injili kwa wale ambao hawakuipokea wakati wakiwa duniani.
Shughuli Yamkini
-
Chora ubaoni duara na mstari ukipita katikati. Andika Paradiso ya Roho nusu moja ya duara na Gereza la Roho upande mwingine. Mwalike mmoja wa watoto kusoma 1 Petro 3:18–20; 4:6 (ona 1 Petro 4:6, tanbihi a, kwa marejeleo kutoka Tafsiri ya Joseph Smith). Elezea kwamba Yesu Alipokufa, alikwenda paradiso ya roho. Aliwafundisha roho wenye haki kule ili kufundisha injili kwa roho walio katika gereza la roho.
-
Mwalike mzazi au ndugu mkubwa wa mmoja wa watoto kusimulia kuhusu kwenda hekaluni na kupokea ibada kwa niaba ya mmoja wa mababu zao.
-
Waalike watoto kujaza chati ya mti rahisi wa familia (ona mfano kwenye “Kurasa za Kupaka Rangi za Historia ya Familia,” ChurchofJesusChrist.org).
Himiza Kujifunza Nyumbani
Waalike watoto kushiriki mti wao wa familia pamoja na wanafamilia wao na waombe kusaidiwa kuongeza majina kwenye mti huo.