“Novemba 20–26. 1 na 2 Petro: ‘Kufurahi Sana, kwa Furaha Isiyoneneka na Yenye Utukufu’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023 (2022)
“Novemba 20–26. 1 na 2 Petro,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2023
Novemba 20–26
1 na 2 Petro
“Kufurahi Sana kwa Furaha Isiyoneneka na Yenye Utukufu”
Unaposoma Waraka wa Petro, unaweza kupokea misukumo ya kiroho. Andika ushawishi huo wakati ungali “bado katika Roho” (Mafundisho na Maagano 76:80) ili uweze kwa usahihi kupata kile Mungu anachokufundisha.
Andika Misukumo Yako
Muda mfupi baada ya Ufufuko Wake, Mwokozi alitoa unabii ambao yaweza kuwa ulikuwa wa kutaabisha kwa Petro. Yeye alitabiri kwamba wakati Petro atakapouawa kifo cha kishahidi kwa ajili ya imani yake, angechukuliwa “asikotaka [yeye] …, akiashiria ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu” (Yohana 21:18–19). Miaka kadhaa baadaye, Petro alipoandika nyaraka zake, alijua kwamba kifo chake kilichotabiriwa kilikuwa kimekaribia: “Kule kuwekea mbali maskani yangu kwaja upesi, kama Bwana wetu Yesu Kristo alivyonionyesha” (2 Petro 1:14). Na bado maneno ya Petro hayakujawa na woga au kukosa rajua. Badala yake, aliwafundisha Watakatifu “kufurahi sana,” japokuwa walikuwa “wamehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali.” Aliwashauri kukumbuka kwamba “kujaribiwa kwa imani [yao]” kungewaongoza kwenye “sifa na utukufu na heshima katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo” na kwenye wokovu wa roho [zao]” (1 Petro 1:6–7,9). Imani ya Petro lazima ilikuwa ya kutia faraja kwa wale Watakatifu wa mwanzo, kama ilivyo ya kutia moyo kwa Watakatifu leo, ambao pia ni “washiriki wa mateso ya Kristo; ili, na katika ufunuo wa utukufu wake tufurahi kwa shangwe” (1 Petro 4:13).
Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko
1 Petro 1:3–9; 2:19–24; 3:14–17; 4:12–19
Ninaweza kupata furaha katika nyakati za majaribu na mateso.
Kipindi baada ya Kusulubiwa kwa Kristo haukuwa wakati rahisi kuwa Mkristo, na waraka wa kwanza wa Petro ulithibitisha hilo. Katika sura nne za kwanza, utaona maneno na virai vinavyoelezea magumu: huzunishwa, majaribu, huzuni, majaribu kama moto, na mateso (ona 1 Petro 1:6; 2:19; 4:12–13). Lakini pia utaona maneno ambayo yanaonekana kuwa furaha—ungetaka kutengeneza orodha ya kile unachopata. Kwa mfano, unaposoma 1 Petro 1:3–9; 2:19–24; 3:14–17; na 4:12–19, ni kitu gani hukupa tumaini kwamba unaweza kupata shangwe hata katikati ya nyakati ngumu?
Ungeweza pia kusoma ujumbe wa Rais Russell M. Nelson “Furaha na Kuendelea Kuishi Kiroho” (Liahona, Nov. 2016, 81–84) na utafute mifanano kati ya kile Petro alichofundisha na kile Rais Nelson alichofundisha. Je, ni nini katika mpango wa wokovu na injili ya Yesu Kristo ambacho hukupa shangwe?
Ona pia Ricardo P. Giménez, “Kupata Kimbilio kutoka Kwenye Dhoruba za Maisha,” Liahona, Mei 2020, 101–3
Injili inahubiriwa kwa wafu ili kwamba waweze kuhukumiwa kwa haki.
Siku moja, kila mtu atasimama mbele ya kiti cha hukumu na “kutoa hesabu kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na walio kufa” (1 Petro 4:5). Ni kwa jinsi gani Mungu anaweza kuhukumu watu wote kwa usawa wakati fursa zao za kuelewa na kuishi injili ni tofauti sana. Gundua mafundisho ambayo Petro alifundisha katika 1 Petro 3:18–20; 4:6 husaidia kujibu swali hili. Je, ni kwa jinsi gani mistari hii huimarisha imani yako katika usawa na haki ya Mungu?
Ili kuchungza mafundisho haya zaidi, jifunze Mafundisho na Maagano 138, ufunuo ambao Rais Joseph F. Smith alipokea alipokuwa akitafakari haya maandishi ya Petro. Ni kweli zipi za ziada Rais Smith alijifunza?
Ona pia Mada za Injili, “Ubatizo wa Wafu,” topics.ChurchofJesusChrist.org.
Kupitia nguvu ya Yesu Kristo, ninaweza kuukuza utu wangu mtakatifu.
Je, umewahi kuhisi kwamba kuwa kama Yesu Kristo na kukuza sifa Zake haiwezekani? Mzee Robert D. Hales alitoa wazo hili la kutia moyo kuhusu jinsi tunavyoweza kukuza sifa kama za Kristo: “Sifa za Mwokozi … ni sifa zinazojifuma, moja ikiiongeza nyingine, ambazo hukua ndani yetu katika njia za muingiliano. Kwa maneno mengine, hatuwezi kupata sifa moja ya Kristo bila pia kupata na kuzishawishi zingine. Pale sifa moja inapokuwa na nguvu, ndivyo zinavyokuwa na zingine zaidi” (“Kuwa Mfuasi wa Bwana Wetu Yesu Kristo,” Liahona, Mei 2017, 46).
Unaposoma 2 Petro 1:1–11, tafakari sifa “za asili ya kiungu” katika mistari hii. Katika uzoefu wako, ni kwa jinsi gani “zimefumwa,” kama Mzee Hales alivyoelezea? Je, zinajenganaje moja juu ya nyingine? Unajifunza nini kingine kutoka kwenye mistari hii kuhusu mchakato wa kuwa zaidi kama Kristo?
Ungeweza pia kutafakari “ahadi kubwa mno za thamani” ambazo Mungu hutoa kwa watakatifu Wake—ikijumuisha wewe (2 Petro 1:4). Ujumbe wa Mzee David A. Bednar “Ahadi Kubwa Mno, za Thamani” (Liahona, Nov. 2017, 90–93) unaweza kukusaidia kuelewa ahadi hizo ni nini na jinsi ya kuzipokea.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani
-
1 Petro 2:5–10.Unaposoma mistari hii na familia yako, fikiria kutumia mawe ili kuwasaidia wanafamilia kupata taswira ya mafundisho ya Petro kwamba Mwokozi ni jiwe letu “kuu la pembeni.” Je, ni kwa jinsi gani sisi ni kama “mawe yaliyo [hai]” ambayo Mungu anatumia ili kujenga ufalme Wake? Je, tunajifunza nini kutoka kwa Petro kuhusu Mwokozi na nafasi yetu katika ufalme Wake? Je, ujumbe wa Petro kwa familia yako ni upi?
-
1 Petro 3:8–17.Je, ni kwa jinsi gani tunaweza “kuwa tayari kutoa jibu” kwa wale wanaotuuliza kuhusu imani yetu? Familia yako inaweza kufurahia kuigiza nyakati ambapo mtu huwajia na maswali kuhusu injili.
-
1 Petro 3:18–20; 4:6.Je, familia yako inaweza kufanya nini ili kuhisi kuwa wameunganishwa na mababu zako? Pengine mngeweza kusherehekea siku za kuzaliwa za mababu waliofariki kwa kuandaa mlo pendwa, mkitazama picha, au mkisimulia hadithi kutoka katika maisha yao. Ikiwezekana, mnaweza pia kupanga kupokea ibada kwa ajili ya mababu zenu hekaluni (kwa ajili ya msaada, tembelea FamilySearch.org).
-
2 Petro 1:16–21.Katika mistari hii, Petro anawakumbusha Watakatifu juu ya uzoefu wake katika Mlima wa Kugeuka sura (ona pia Mathayo 17:1–9). Je, tunajifunza nini kutoka kwenye mistari hii kuhusu mafundisho ya manabii? (Ona pia Mafundisho na Maagano 1:38). Je, ni kitu gani hutupatia ujasiri wa kuwafuata manabii wetu walio hai leo?
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.
Wimbo uliopendekezwa: “Family History—I Am Doing It,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 94.