Agano Jipya 2023
Novemba 6–12. Waebrania 7–13: “Kuhani Mkuu wa Mambo Mema Yatakayokuwapo”


“Novemba 6–12. Waebrania 7–13: ‘Kuhani Mkuu wa Mambo Mema Yatakayokuwapo’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023 (2022)

“Novemba 6–12. Waebrania 7–13,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2023

Melkizedeki akimbariki Abramu

Melkizedeki Akimbariki Abramu, na Walter Rane Karama ya msanii

Novemba 6–12

Waebrania 7–13

“Kuhani Mkuu wa Mambo Mema Yatakayokuwapo”

Unaposoma Waebrania 7–13, unaweza kupokea misukumo kupitia Roho Mtakatifu. Fikiria njia unazoweza kuiandika; kwa mfano, unaweza kuiandika ndani ya muhtasari huu, kwenye nafasi ya pembeni ya maandiko yako, au katika daftari, au katika shajara.

Andika Misukumo Yako

Hata Watakatifu waaminifu kuna wakati wanapata “mashutumu na dhiki” ambayo yanaweza kutikisa kujiamini kwao (ona Waebrania 10:32–38). Paulo alijua kwamba waongofu wa Kiyahudi kwenye Ukristo walikuwa wakipitia mateso makali kwa sababu ya imani yao mpya. Ili kuwatia moyo wa kubaki wakweli kwenye shuhuda zao, aliwakumbusha juu ya utamaduni wa muda mrefu wa wafuasi waaminifu kutoka katika historia yao wenyewe: Habili, Henoko, Nuhu, Ibrahimu, Sara, Yusufu, Musa—“wingu kubwa la mashahidi” kwamba ahadi za Mungu ni za kweli na zinastahili kusubiriwa (ona Waebrania 11; 12:1). Utamaduni huu ni wako pia. Urithi huu wa imani unatolewa kwa wote wale wanaomtazamia “Yesu [kama] mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu” (Waebrania 12:2). Kwa sababu Yake, wakati wowote dhiki inapotufanya “tusite-site,” sisi badala yake tunaweza “kukaribia kwa moyo wa kweli katika hakikisho timilifu la imani”(Waebrania 10:22, 38). Kwetu sisi, kama vile kwa Watakatifu wa kale, Yesu Kristo ni “kuhani wetu mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo” (Waebrania 9:11).

ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko

Waebrania 7

Ukuhani wa Melkidezeki unanielekeza kwa Yesu Kristo.

Kwa karne nyingi, Wayahudi walikuwa wakitumia Ukuhani wa Lawi, ambao unajulikana pia kama Ukuhani wa Haruni. Lakini kwa utimilifu wa injili ya Yesu Kristo ulikuja urejesho wa Ukuhani mkuu wa Melkizedeki, ambao ulitoa baraka kubwa zaidi. Je, unajifunza nini kuhusu Ukuhani wa Melkizedeki kutoka Waebrania 7? Ukiweka hili akili kwamba madhumuni ya waraka huu—kama vile maandiko yote—ni kujenga imani katika Yesu Kristo, ungeweza kuandika vifungu ambavyo vinamshuhudia Yeye.

Hapa kuna baadhi ya mifano mingine ya kweli unazoweza kuzipata:

Ni baraka zipi umezipokea kutoka kwenye Ukuhani wa Melkizedeki na “ibada zake”? (Mafundisho na Maagano 84:20). Ni kwa jinsi gani Ukuhani wa Melkidezeki umekusaidia kuja kwa Kristo?

Ona pia Alma 13:1–13; Mafundisho na Maagano 121:36–46; Mada za Injili, “Ukuhani wa Melkizedeki,” topics.ChurchofJesusChrist.org; Mwongozo wa Maandiko, “Melkizedeki,” scriptures.ChurchofJesusChrist.org; Russell M. Nelson, “Hazina za Kiroho,” Liahona, Nov. 2019, 76–79; Dallin H. Oaks, “Ukuhani wa Melkizedeki na Funguo,” Liahona, Mei 2020, 69–72.

Waebrania 9; 10: 1–22

Ibada za kale na za sasa huelekeza kwa Yesu Kristo.

Wasomaji wa asili ya Kiebrania wa waraka huu wangeweza kuwa na ufahamu wa maskani ya kale na ibada ambazo Paulo ameelezea. Lakini baadhi hawakutambua kikamilifu kwamba lengo la ibada hizi lilikuwa ni kuelekeza kwenye dhabihu ya Yesu Kristo ya upatanisho.

Katika nyakati za biblia, katika sikukuu ya kila mwaka iliyoitwa Siku ya Upatanisho, kuhani mkuu aliingia mahali patakatifu (au Patakatifu pa Patakatifu) ndani ya hekalu la Yerusalemu na kutoa dhabihu ya mbuzi au kondoo kulipia dhambi za Israeli.

Unaposoma maelezo ya Paulo ya ibada hizi, tafuta ishara na mafundisho ambayo yanaweza kukusaidia kuelewa vyema misheni ya Mwokozi ya upatanisho.

Ibada tunazoshiriki leo ni tofauti na zile za wakati wa Paulo, lakini madhumuni yake ni sawa sawa. Je, ni kwa jinsi gani ibada za leo zinakushuhudia wewe juu ya Yesu Kristo?

Ili kujifunza zaidi kuhusu sherehe za Wayahudi wa kale na ishara zake, angalia video “The Tabernacle” na “Sacrifice and Sacrament” (ChurchofJesusChrist.org).

Waebrania 11

Imani huhitaji kutegemea katika ahadi za Mungu.

Kama mtu angekutaka kuelezea maana ya imani, ungesema nini? Dada Anne C. Pingree alitumia lugha kutoka Waebrania 11 kutupatia maelezo haya ya imani: “Uwezo wa kiroho wa kushawishiwa juu ya ahadi ambazo zinaonekana kuwa ‘mbali lakini ambazo yawezekana zisipatikane katika maisha haya” (“Kuziona Ahadi kwa Mbali,” Liahona, Nov. 2003, 14).

Fikiria kutengeneza maana yako mwenyewe ya imani unapotafakari mawazo yaliyomo katika Waebrania 11. Je, mifano ya watu waliotajwa katika sura hii hukufundisha nini kuhusu imani? (Ona pia Etheri 12:6–22.)

Ni ahadi zipi unaziona kwa “mbali”? Je, ni kwa jinsi gani unaweza kumuonyesha Bwana kwamba wewe “umeshawishika nazo, na umezikumbatia”? (Waebrania 11:13).

Ona pia Alma 32:21, 26–43; Jeffrey R. Holland, “Kuhani Mkuu wa Mambo Mema Yatakayokuwapo,” Ensign, Nov. 1999, 36–38; Mada za Injili, “Imani katika Yesu Kristo,” topics.ChurchofJesusChrist.org.

ikoni ya kujifunza kama familia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani

Waebrania 10:32–36.Unaweza kuwaalika wanafamilia kuelezea uzoefu wa kiroho wakati walipohisi “kuangazwa” na kweli. Je, ni jinsi gani uzoefu huu hutusadia “kutotupilia mbali kujiamini [kwetu]” katika nyakati za majaribu au shaka?

Waebrania 11.Je, ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia wanafamilia wajifunze kutoka kwenye mifano ya uaminifu iliyotajwa katika Waebrania 11? Inaweza kuwa ya kufurahisha kuigiza hadithi za baadhi ya mifano hii. Unaweza kupitia tena baadhi ya hadithi hizi katika Hadithi za Agano la Kale. Au pengine familia yako inaweza kujadili mifano ya watu wengine waaminifu mnaowajua—ikijumuisha mababu, viongozi wa Kanisa, na watu wa jumuiya yako. Mnaweza pia kuimba wimbo kuhusu imani, kama vile “Faith” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 96).

Waebrania 12:2.Kulingana na mstari huu, kwa nini Yesu alikuwa tayari kuvumilia maumivu na mateso ya msalaba? Hii inatufundisha nini kuhusu jinsi tunavyoweza kuvumilia majaribu yetu? Rais Russell M. Nelson alitoa umaizi wenye msaada juu ya mstari huu katika ujumbe wake “Furaha na Kuendelea Kuishi Kiroho” (Liahona, Nov. 2016, 81–84).

Waebrania 12:5–11.Je, ni kwa nini Bwana huturudi na kutusahihisha? Tunaona nini kutoka kwenye mistari hii kuhusu vile Bwana anavyochukulia marudia? Je, ni kwa jinsi gani mistari hii huathiri jinsi unavyotoa au kupokea marudia?

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.

Wimbo uliopendekezwa: “Faith,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 96.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Tumia muziki ili umwalike Roho Mtakatifu na kujifunza mafundisho. Urais wa Kwanza umesema, “Muziki unazo nguvu zisizo na kipimo katika kutusogeza [sisi] kuelekea kuwa watu wa kiroho zaidi” (“Dibaji ya Urais wa Kwanza,” Nyimbo za Kanisa, x). Pengine wimbo kuhusu imani, kama vile “True to the Faith” (Nyimbo za Kanisa, na. 254), unaweza kuwa nyongeza kwenye mjadala wa familia kutoka Waebrania 11.

mfano wa Yerusalemu ya kale

Ishara na ibada za hekalu la kale zilifundisha kuhusu kazi ya Yesu Kristo.