“Mei 30–Juni 5. Waamuzi 2–4; 6–8; 13–16: ‘Bwana Akawainulia Mwokozi’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Agano la Kale 2022 (2021)
“Mei 30–Juni 5. Waamuzi 2–4; 6–8; 13–16,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2022
Mei 30–Juni 5
Waamuzi 2–4; 6–8; 13–16
“Bwana Akawainulia Mwokozi”
Kuna hadithi nyingi za kuinua zinazopatikana katika Waamuzi 2–4; 6–8; 13–16. Tafakari jinsi unavyoweza kutumia hadithi hizi kuwasaidia watoto kuja karibu na Mwokozi na kutamani kumfuata Yeye.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Alika kila mtoto ashiriki hadithi kutoka kwenye maandiko ambayo walijifunza hivi karibuni. Kisha waombe washiriki kile walichojifunza kutoka katika hadithi hizi.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Yesu Kristo ni Mwokozi wangu.
Wakati Waisraeli walipomuomba Bwana, Yeye akawainulia mwokozi. Wasaidie watoto kuona kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi ambaye Mungu ametuinulia.
Shughuli Yamkini
-
Waelezee watoto kwamba wakati Waisraeli waliacha kutii amri za Mungu, walipoteza ulinzi Wake na wakashindwa na maadui zao. Soma kutoka katika Waamuzi 3:9 kifungu cha maneno “wana wa Israeli walipomlingana Bwana.” Waisraeli walifanya nini walipohitaji msaada? Shiriki uzoefu ambapo uliomba kwa ajili ya usaidizi na Mungu akajibu maombi yako.
-
Soma kutoka katika Waamuzi 3:9 kifungu cha maneno “Bwana akawainulia mwokozi,” na uwaalike watoto wakirudie pamoja na wewe mara chache. Elezea kwamba mkombozi ni mtu ambaye hutuokoa. Waonyeshe watoto picha kadhaa za watu, ikijumuisha picha ya Yesu Kristo, na ziweke picha zikiangalia chini sakafuni. Waache watoto wachukue zamu kugeuza picha, wakiipata picha Yesu, na wainyanyue juu. Shuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi ambaye Mungu alimuinua ili kutuokoa kutoka katika dhambi na kifo.
Bwana anaweza kutumia vitu vidogo kufanya kazi kubwa.
Gidioni alijifikiria kuwa maskini na duni, lakini Mungu alimwona kama “mtu shupavu na shujaa” (Waamuzi 6:12). Wasaidie watoto waone kwamba hata kama wanahisi kuwa wadogo, Mungu anaweza kufanya kazi kupitia wao kufanya mambo muhimu (ona Alma 37:6–7).
Shughuli Yamkini
-
Waambie watoto kwamba Bwana alihitaji mtu wa kumsaidia Yeye kuokoa Israeli kutoka kwa maadui wao, Wamidiani, na Alimchagua Gidioni. Wasomee watoto Waamuzi 6:15 na uwaulize kwa nini Gidioni hakuhisi anaweza kufanya kile Bwana alikuwa anataka. Soma mstari wa 16, na uwaulize ni nani Bwana alisema angemsaidia Gidioni. Waambie watoto kuhusu wakati ambao Bwana alikuomba ufanye kitu kigumu ili kumtumikia Yeye na ukahisi Yeye alikuwa pamoja nawe.
-
Onyesha picha za watoto au vijana wakifanya mambo makubwa katika huduma ya Mungu (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 19, 23, 90, 102), au waambie kuhusu mifano ambayo umeona. Wasaidie watoto kufikiria njia wanazoweza kushiriki katika kazi ya Mungu, na waombe wachore picha zao wenyewe wakifanya mambo haya.
-
Tumia ukurasa wa shughuli wa wiki hii kuwafundisha watoto kuhusu jinsi Bwana alivyolifanya jeshi la Israeli kuwa dogo ili Waisraeli waweze kujua kwamba nguvu Zake zilikuwa zimewaokoa kutoka kwa maadui wao. Shiriki mifano ya vitu vidogo ambavyo vinafanya mambo makubwa, kama vile nyuki wakikusanya nekta kutengeneza asali. Toa ushuhuda wako kwamba Mungu hutusaidia kufanya kazi kubwa, hata wakati tunapojihisi kuwa wadogo.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Yesu Kristo ni Mkombozi wangu.
Waamuzi 3 inaelezea mzunguko ambao unaweza kuutumia kuwafundisha watoto kwamba Mungu hutukomboa kutoka kwenye dhambi kupitia Mwokozi Yesu Kristo.
Shughuli Yamkini
-
Andika yafuatayo ubaoni: “walitenda uovu” “walimililia Bwana,” na “akawainulia mwokozi.” Waalike baadhi ya watoto watafute vifungu hivi katika Waamuzi 3:7–9, na uwalike wengine kuvitafuta katika Waamuzi 3:12–15. Waelezee watoto kwamba mara kwa mara katika kitabu cha Waamuzi, Waisraeli “walitenda uovu.” Kisha, wakati maadui zao walipowashambulia, “walimlilia Bwana,” na Bwana “akawainulia mwokozi” kuwasaidia. Je, tunajifunza nini kuhusu Bwana kutoka kwenye mzunguko huu?
-
Imbeni pamoja wimbo ambao huwasaidia watoto kuelewa kwamba Yesu Kristo ni Mkombozi na Mwokozi wao, kama vile “He Sent His Son” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 34–35). Waalike watoto washiriki hisia zao kuhusu kile Mwokozi amefanya kuwakomboa kutoka kwenye dhambi, majaribu, huzuni na kifo.
Ninaweza kuwa mwaminifu kwa Bwana hata kama wengine si waaminifu.
Ingawa wengi wa Waisraeli walianguka kutoka kwa Bwana, baadhi yao walibaki wakweli Kwake na waliweza kuwasaidia wengine wengi kurudi katika haki. Unawezaje kuhamasisha watoto kubaki wakweli kwa Bwana bila kujali wengine wanachofanya?
Shughuli Yamkini
-
Waambie watoto kwamba wakati Waisraeli walikuwa waovu, mwanamke mwema aliyeitwa Debora na amiri jeshi wa jeshi la Waisraeli, Baraka, walikomboa Israeli kutoka kwa maadui zao (ona Waamuzi 4:1–15). Someni pamoja Waamuzi 4:14, na waalike watoto watafute kitu ambacho Debora alisema ambacho kinaonyesha kwamba imani yake katika Bwana ilikuwa thabiti. Kisha waombe wasome Mafundisho na Maagano 84:88 kutafuta kanuni iliyopo pia katika Waamuzi 4:14. Wahimize washiriki kile ahadi ya Bwana “Nitakwenda mbele yenu” inavyomaanisha kwao.
-
Imbeni wimbo kuhusu kutii amri, kama vile “Choose the Right” (Nyimbo, no. 239) au “Choose the Right Way” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 160–61). Tunawezaje kusimama kwa ajili ya haki na kutii amri hata wakati wengine wanaotuzunguka hawafanyi hivyo?
Njia za Mungu ni tofauti na njia za ulimwengu.
Bwana alimtaka Gidioni kufanya mambo ambayo labda hakuyaelewa wakati huo. Ni nini kinakuvutia kuhusu hadithi yake? Unahisi inaweza kuwabariki vipi watoto unaowafundisha?
Shughuli Yamkini
-
Waombe watoto wafikirie kwamba walihitaji kukusanya jeshi pamoja kwenda vitani. Ni watu wangapi wangewataka katika jeshi lao? Ukitumia Waamuzi 7:4–7, waalike watoto waigize jinsi Bwana alivyomsaidia Gidioni kuchagua jeshi ambalo lingewakomboa Waisraeli kutoka kwa Wamidiani. Kwa nini Bwana alitaka jeshi la Gidioni kuwa dogo sana? (ona Waamuzi 7:2). Kwa nini kufuata amri ya Bwana kumekuwa kugumu kwa Gidioni na jeshi lake? Waombe watoto kushiriki uzoefu wakati walipojifunza kumwamini Bwana hata ingawa kufanya hivyo ilikuwa vigumu.
-
Waalike watoto wachore picha za upanga, ngao, tarumbeta, taa, na jagi. Waulize watoto kitu gani kati ya hivi wangependa kwenda nacho vitani. Waalike wasome Waamuzi 7:16 ili kujifunza kile jeshi la Gidioni lilibeba. Kwa nini ingekuwa ni ujasiri kufanya hivi? Someni pamoja Waamuzi 7:19–21 ili kujifunza jinsi jeshi lilivyotumia tarumbeta na jagi kuwashinda Wamidiani. Je, tunajifunza nini kuhusu Bwana kutoka kwenye mistari hii?
Himiza Kujifunza Nyumbani
Waalike watoto washiriki na mwanafamilia wao kitu fulani walichojifunza leo ambacho huwafanya watake kutii amri.