“Septemba 19–25. Isaya 40–49: ‘Wafarijini Watu Wangu’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Agano la Kale 2022 (2021)
“Septemba 19–25. Isaya 40–49,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2022
Septemba 19–25
Isaya 40–49
“Wafarijini Watu Wangu”
Vifungu vingi vya maneno katika Isaya 40–49 vinaweza kuwasaidia watoto kuongeza upendo wao kwa Bwana na imani yao Kwake. Tafuta mwongozo wa Roho ili kupata vifungu hivyo vya maneno pale unapojifunza.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Soma Isaya 40:9 pamoja na watoto na waalike wajifanye wanapanda juu ya “mlima mrefu” na kisha wafanye zamu kupaza sauti zao kushiriki jambo walilojifunza kutoka kwenye maandiko hivi karibuni—labda nyumbani au kanisani.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Ninaweza kuwa shahidi wa Bwana.
Bwana aliwakumbusha Waisraeli kwamba walikuwa wameshuhudia mambo mengi ambayo Yeye alikuwa ametenda kwa ajili yao. Aliwataka wao (na sisi sote) kuwa mashahidi wake, ili kuwasaidia wengine kujua juu ya nguvu na wema Wake.
Shughuli Yamkini
-
Waambie watoto kuhusu jambo ambalo wewe umeshuhudia. Wasaidie wafikirie mambo ambayo wamepitia ambayo wanaweza kuambiana kuhusu au kuwa “shahidi”—kwa mfano, chakula kitamu walichowahi kula, mahali walipozuru au mtu wanayemfahamu. Wasomee watoto kutoka katika Isaya 43:10: “Ninyi ni mashahidi wangu, asema Bwana, na mtumishi niliyemchagua.” Waambie watoto kwamba tunapobatizwa tunaahidi kuwa mashahidi wa Yesu Kristo (ona Mosia 18:9). Je, ina maana gani kuwa shahidi wa Bwana?
-
Waombe watoto kushiriki kile wanachokijua kuhusu Yesu Kristo na injili Yake. Waoneshe picha ili kuwapa mawazo (kwa mfano, picha ya Ufufuko wa Mwokozi, Kitabu cha Mormoni, hekalu na nabii aliye hai). Waalike wazungumze kuhusu kile ambacho wangeweza kushiriki pamoja na wengine kama mashahidi wa Bwana.
“Zaidi yangu mimi hapana mwokozi.”
Yesu Kristo ndiye pekee anayeweza kutuokoa kutoka katika dhambi na kifo. Tafakari jinsi utakavyowashawishi watoto kuweka tumaini lao Kwake.
Shughuli Yamkini
-
Waalike watoto wavute taswira ya hali ambapo wanaweza kuhitaji msaada (kama vile kuwa mgonjwa au kukumbwa na dhoruba). Onesha vitu kadhaa (au picha za vitu), ambavyo vitawasaidia katika hali fulani na vingine ambavyo havitawasaidia. Kwa mfano, mwamvuli ungesaidia katika mvua, lakini glasi ya maji na penseli havingesaidia. Waombe watoto wachukue kitu ambacho kingesaidia katika hali hiyo. Onesha picha ya Mwokozi ili kuwasaidia watoto kuzungumza kuhusu jinsi Yeye anavyotusaidia sisi.
-
Wasomee watoto Isaya 43:11, na waombe waoneshe kwa kidole picha ya Yesu wakati wanaposikia neno “Mwokozi.” Shuhudia kwamba kwa sababu Yesu Kristo aliteseka na kufa kwa ajili yetu na akafufuka, Yeye ni mtu pekee anayeweza kutuokoa kutokana na dhambi zetu na kutokana na kifo.
Kutii amri za Mungu kunaleta amani.
Bwana anaahidi amani kama “mto wa maji” na haki kama “mawimbi ya bahari” kwa wale wanaotii amri Zake.
Shughuli Yamkini
-
Wasomee watoto Isaya 48:18. Waalike kuchezesha viganja na mikono yao kama mto wa maji na mawimbi. Zungumza kuhusu jinsi kutii amri za Mungu kulivyokusaidia kuhisi amani kama mto wa maji au imara kama mawimbi.
-
Chora mto ubaoni. Wasaidie watoto wafikirie juu ya amri ambazo Mungu ametupatia. Andika amri hizo juu ya kipande cha karatasi (au chora picha rahisi ya amri hizo), na waruhusu watoto wafanye zamu kupachika amri kwenye mto ubaoni. Wasaidie watoto wajifunze jinsi kutii amri za Mungu kunavyoleta amani.
-
Imbeni pamoja wimbo kuhusu amri, kama vile “Keep the Commandments” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 146–47). Wimbo huu unafundisha nini kuhusu kwa nini tunapaswa kutii amri za Mungu?
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Ninaweza kusaidia kutengeneza “njia ya Bwana.”
Tunasaidia kutimiza unabii katika Isaya 40:3–5 kwa kuwasaidia wengine kumpokea Bwana katika maisha yao.
Shughuli Yamkini
-
Muombe mtoto mmoja asome Isaya 40:3 wakati watoto wengine kila mmoja akisoma moja ya vifungu vifuatavyo na kutafuta maneno na vifungu vya maneno vinavyofanana: Marko 1:3–4 (Yohana Mbatizaji); Alma 7:9 (Alma); Mafundisho na Maagano 33:10–11 (wamisionari wa siku za mwisho). Wasaidie watambue nani anaitengeneza “njia ya Bwana” katika kila kifungu. Je, watu hawa wanaitengenezaje njia ya Bwana? Tunaweza kufanya nini ili kusaidia?
-
Chora njia ubaoni na soma pamoja na watoto Isaya 40:3–5. Waombe watoto waorodheshe vikwazo vinavyoweza kuwazuia watu kumfuata Mwokozi na waalike wachore vikwazo kwenye njia. Acha wafute vikwazo hivyo wakati unapozungumza kuhusu jinsi tunavyoweza kuwasaidia watu kuvishinda.
Bwana yu pamoja nami katika majaribu yangu.
Tunapofanya maagano na Bwana, Yeye anaweka ahadi ya kuwa pamoja nasi—hata wakati wa majaribu yetu. Wasaidie watoto wajione wenyewe kama sehemu ya watu wa Bwana wa agano na kama wapokeaji wa ahadi Zake.
Shughuli Yamkini
-
Andika ubaoni Mimi ni… na nita… waalike watoto wasome Isaya 41:10 na Isaya 43:1–5 ili kutafuta Bwana amesema Yeye ni nani na nini amesema Yeye atafanya. Ni virai gani vingine vimerudiwa katika mistari hii? Je, ni kwa jinsi gani ujumbe huu unatupatia sisi faraja na matumaini kipindi cha nyakati ngumu?
-
Someni pamoja Isaya 48:10, na zungumzeni kuhusu tanuru ni nini na njia tofauti za tanuru linavyotumika. Eleza kwamba vyuma husafishwa katika tanuru. Kwa nini tanuru ni njia nzuri ya kufafanua mateso? Ni kwa jinsi gani mateso yetu yanaweza kutufanya tuwe wasafi? (ona Alma 62:41).
Bwana kamwe hatanisahau mimi.
Wakati tunapohisi kuwa mbali na Bwana kwa sababu ya dhambi, majaribu au sababu nyingine yoyote, ujumbe wa Isaya 49:14–16 unaweza kuleta faraja.
Shughuli Yamkini
-
Waombe watoto wasome Isaya 49:14. Nini kinaweza kuwafanya watu wahisi kusahaulika au kuachwa? Ni kwa jinsi gani tunaweza kuwasaidia wengine kujua kwamba Bwana hajawasahau? Je, tunajuaje kuwa Yeye hajatusahau?
-
Waalike watoto wazungumze kuhusu mtu wanayemjua ambaye kamwe hawatamsahau, kama vile mwanafamilia au rafiki. Jadilini jinsi mama mwenye upendo anavyojisikia kuhusu watoto wake na jinsi Bwana anavyojisikia kuhusu sisi. Kisha waombe watoto wasome Isaya 49:15–16. Kulingana na mistari hii, kwa nini Bwana hatatusahau sisi? Waalike watoto kushiriki hisia zao kuhusu Yesu Kristo.
Himiza Kujifunza Nyumbani
Waalike watoto wafikirie kuhusu jambo walilojifunza leo ambalo wanataka kujifunza zaidi kulihusu. Wasaidie waandike swali kuhusu jambo hilo ambalo wanaweza kumwuliza mzazi au mwanafamilia mwingine.