“Oktoba 17–23. Yeremia 30–33; 36; Maombolezo1; 3: ‘Nitageuza Masikitiko Yao kuwa Furaha,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Agano la Kale 2022 (2021)
“Oktoba 17–23. Yeremia 30–33; 36; Maombolezo1; 3,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2022
Oktoba 17–23
Yeremia 30–33; 36; Maombolezo1; 3
“Nitageuza Masikitiko Yao kuwa Furaha”
Vitabu vya Yeremia na Maombolezo vinaweza kuwa vigumu kwa watoto kuelewa, lakini darasa lako bado linaweza kujifunza masomo kutokana na kanuni zilizofundishwa katika vitabu hivi. Je, unasukumwa kushiriki kitu gani?
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Pitisha nakala ya Biblia. Watoto wanaposhika kitabu, waombe kushiriki jambo wanalolipenda kuhusu Agano la Kale—pengine kanuni au hadithi pendwa waliyojifunza kutoka Agano la Kale nyumbani au kanisani.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Baba wa Mbinguni na Yesu Wananipenda mimi.
Kuhisi “upendo usio na mwisho” wa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo kutawasaidia watoto unaowafundisha kusogea karibu zaidi Nao.
Shughuli Yamkini
-
Waoneshe watoto baadhi ya vitu (au picha za vitu) ambavyo hudumu muda mrefu na baadhi ambavyo havidumu, kama vile sarafu na kipande cha tunda. Waulize watoto kipi kitadumu muda mrefu zaidi, na jadilini kwa nini baadhi ya vitu hudumu kwa muda mrefu zaidi ya vingine. Soma Yeremia 31:3, na wasaidie watoto waelewe kwamba upendo ambao Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanao kwao “hauna mwisho.”
-
Waombe watoto kushiriki jinsi Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanavyoonesha “fadhili” Zao kwao (Yeremia 31:3). Ili kuwapa watoto mawazo, imbeni wimbo kuhusu upendo Wao kwetu, kama vile “I Feel My Savior’s Love” au “My Heavenly Father Loves Me” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 74–75, 228–29). Kama inawezekana, onesha picha za vitu vilivyotajwa katika wimbo. Tunajisikiaje tunapofikiria kuhusu upendo wa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo?
Maandiko ni neno la Mungu.
Bwana alimwambia Yeremia aandike maneno Yake na maandishi ya Yeremia yamehifadhiwa kwa ajili yetu katika kitabu cha Yeremia. Wasaidie watoto waongeze upendo wao wa maandiko, ambapo tunapata neno la Mungu.
Shughuli Yamkini
-
Mwalike mtoto mmoja ajifanye kuwa Yeremia na waalike watoto wengine kuwa Baruku. Msaidie mtoto anayeigiza kama Yeremia kusema maneno kutoka Yeremia 36:3 wakati watoto wengine wakijifanya kuyaandika, kama vile Baruku alivyofanya. Shuhudia kwamba maandiko leo ni “maneno ya Bwana” (Yeremia 36:4) ambayo aliwaagiza manabii wayaandike.
-
Onesha kitabu cha watoto na nakala ya maandiko na waombe watoto wazungumzie tofauti wanayogundua kati ya vitabu hivyo. Je, ni kitu gani kinafanya maandiko kuwa ya kipekee? Wasaidie watoto waelewe kwamba maandiko ni maneno ya Mungu yaliyoandikwa na manabii, kama vile kitabu cha Yeremia ni yale ambayo Mungu alimwambia Yeremia ayaandike.
Ninaweza kushiriki kile ninachojifunza kutoka kwenye maandiko.
Watoto wanaweza kuwa na ushawishi mkubwa juu ya wale wanaowazunguka. Kama vile Baruku, wanaweza kushiriki na wengine kile wanachojifunza kwenye maandiko.
Shughuli Yamkini
-
Waalike watoto wafanye matendo yanayoendana na maneno pale unaposoma (au kufanyia ufupisho) Yeremia 36:4–10, kama vile kujifanya kuandika ndani ya kitabu (ona mstari wa 4), kushikilia nondo za jela (ona mstari wa 5), na kuwasomea watu maandiko (ona mistari 8,10). Sisitiza kwamba Baruku alikuwa na ujasiri wa kuwasomea watu maneno ya Yeremia licha ya viongozi wa Yerusalemu kutotaka afanye hivyo. Wasaidie watoto wakumbuke jambo walilojifunza kutoka Agano la Kale na kufikiria jinsi wanavyoweza kulishiriki na wengine.
-
Imbeni wimbo kuhusu maandiko, kama vile “Search, Ponder, and Pray” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto,109). Toa ushuhuda wako juu ya maandiko, na waalike watoto kutoa shuhuda zao pia.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Ninaweza kushika maagano yangu na Mungu.
Mafundisho ya Yeremia kuhusu agano jipya na lisilo na mwisho la Bwana yanaweza kuwasaidia watoto unaowafundisha kuimarisha hamu yao ya kushika maagano yao.
Shughuli Yamkini
-
Chora moyo ubaoni na waalike nusu ya watoto wasome Yeremia 31:31–34 na nusu nyingine wasome Yeremia 32:38–41. Yaalike makundi kuandika ndani ya moyo pale ubaoni mambo wanayojifunza kutoka kwenye mistari yao kuhusu maagano yetu na Mungu. Ni kwa jinsi gani kuwa na sheria ya Mungu imeandikwa katika mioyo yetu (ona Yeremia 31:33) ni tofauti na kuisoma tu katika maandiko? Kwa nini tunataka kufanya maagano na Bwana? Kwa nini Yeye anataka kufanya maagano na sisi?
-
Ili kurejelea maagano tunayofanya wakati tunapobatizwa, waalike watoto watengeneze chati yenye pande mbili kwenye kipande cha karatasi zenye kichwa cha habari Ahadi Zangu na Ahadi za Mungu. Waombe wajaze chati kwa kutumia sehemu yenye kichwa cha habari “Agano la Ubatizo” kwenye makala ya Mada za Injili “Ubatizo” (topics.ChurchofJesusChrist.org) au Mosia 18:10,13; Mafundisho na Maagano 20:37. Waalike watoto waiweke karatasi hiyo nyumbani ili iwasaidie kukumbuka kushika maagano yao.
Maandiko ni neno la Mungu.
Hadithi katika Yeremia 36 inaweza kuwasaidia watoto kujifunza kutokana na mifano ya watu ambao walikubali neno la Bwana katika maandiko.
Shughuli Yamkini
-
Andika maswali haya ubaoni: Kwa nini? Je, ni nani alithamini maandiko? Je, ni nani hakuthamini? Someni pamoja Yeremia 36:1–3, na waulize watoto kwa nini Bwana alimtaka Yeremia aandike maneno Yake. Kisha waombe watoto wafanye kazi katika jozi ya kusoma Yeremia 36:5–8, 20–25 na kubainisha ni akina nani walionesha kwamba waliyathamini maandiko na nani hawakuyathamini. Zungumza kuhusu kwa nini wewe unayathamini maandiko. Shiriki kifungu cha maandiko au hadithi ambayo ina maana ya kipekee kwako. Waalike watoto kushiriki pia.
-
Waalike watoto watumie ukurasa wa shughuli ya wiki hii kufanya mazoezi ya kuelezana wao kwa wao hadithi iliyoko katika Yeremia 36. Waalike kutoa shuhuda zao juu ya maandiko.
Mwokozi alifanya iwezekane kwangu kusamehewa dhambi zangu.
Kama jinsi ambavyo kitabu cha Maombolezo kinavyofafanua kishairi, mara nyingi tunajisikia huzuni wakati tunapotenda dhambi. Hisia hizi zinaweza kutuhamasisha kubadilika na kumwomba Baba wa Mbinguni msamaha.
Shughuli Yamkini
-
Eleza kwa watoto kwamba kwa sababu Waisraeli hawakutubu, Yerusalemu na hekalu viliharibiwa. Waombe watoto wazungumze kuhusu jinsi ambavyo wangeweza kuhisi kama wangeliishi Yerusalemu katika kipindi hicho. Someni pamoja Maombolezo 1:1–2,16. Ni maneno na vifungu gani vya maneno katika mistari hii vinatusaidia sisi kuelewa jinsi ambavyo Waisraeli yawezekana walihisi? Je, ni kwa jinsi gani ujumbe katika Maombolezo 3:22–26 uliwapa wao matumaini?
-
Waombe watoto wafikirie kuhusu wakati ambapo wamehisi huzuni kwa uchaguzi mbaya waliofanya. Wanapata nini katika Maombolezo 3:22–26 ambacho kinawasaidia kujua Bwana yu tayari kuwasamehe?
Himiza Kujifunza Nyumbani
Waalike watoto wawaombe wanafamilia zao kushiriki uzoefu unaohusiana na kanuni mliyojifunza darasani. Kwa mfano, ikiwa mlijadili maandiko, watoto wangeweza kumwomba mwanafamilia kushiriki jinsi anavyojua kwamba maandiko ni ya kweli.