“Julai 22–28. Matendo ya Mitume 16–21: ‘Bwana Alituita kwa ajili ya Kuhubiri Injili’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: Agano Jipya 2019 (2019)
“Julai 22–28. Matendo ya Mitume 16–21,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: 2019
Julai 22–28
Matendo ya Mitume 16–21
“Bwana Alituita kwa ajili ya Kuhubiri Injili”
Kabla ya kuangalia muhtasari huu, kwa maombi soma Matendo ya Mitume 16–21 ukiwa na washiriki wa darasa lako akilini mwako. Mawazo yafuatayo yanaweza kuchangia katika mwongozo wa kiungu uliopokea kutoka kwa Roho.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Fikiria kuwaalika washiriki wa darasa kuelezea kifungu kutoka Matendo ya Mitume 16–21 ambacho kiliwakumbusha uzoefu ambao walikuwa nao wa kushiriki injili.
Fundisha Mafundisho
Kama waumini wa Kanisa, tunashuhudia juu ya Yesu Kristo na kushiriki na wengine injili Yake.
-
Kwa sababu Matendo ya Mitume 16–21 inaelezea safari mbili za kimisionari za Paulo, washiriki wa darasa wanaweza kujifunza kutoka sura hizi jinsi ya kushuhudia juu ya Yesu Kristo na kushiriki na wengine injili Yake kikamilifu. Ili kuhamasisha majadiliano juu ya mada hii, labda ungeweza kuwaalika washiriki wachache kuja darasani wakiwa wamejiandaa kuelezea umaizi walioupata toka Matendo ya Mitume 16–21 kuhusu kufundisha injili. Ili kujadili kwa kina, wangeweza pia kushiriki kauli kutoka kwenye hotuba za mkutano mkuu wa hivi karibuni kuhusu kazi ya umisionari. Wangeweza kutafuta hotuba moja wao wenyewe, au wewe unaweza kupendekeza ujumbe mmoja katika “Nyenzo za Zaida.”
-
Ujumbe mmoja maarufu toka sura hizi ni umuhimu wa nafasi ya Roho Mtakatifu katika kushiriki injili na wengine. Kwa mfano, washiriki wa darasa wangeweza kugundua ni kwa namna gani Roho Mtakatifu aliwasaidia Paulo na Sila katika Matendo ya Mitume 16:6–15. Wangeweza pia kusoma 2 Nefi 33:1 na Mafundisho na Maagano 42:14 na kuelezea juu ya kweli wanazozipata kuhusu umuhimu wa kuwa na Roho wakati wa kushiriki injili (ona pia kauli toka Mzee Dallin H. Oaks katika “Nyenzo za Ziada”). Labda washiriki wa darasa wangeweza kushiriki uzoefu wao wakati Roho Mtakatifu aliongoza jitihada zao za kushiriki injili. Ni uzoefu upi tumewahi kuwa nao wa kushiriki injili na mtu mwingine ambaye Bwana amemuweka katika njia yetu? (Ona pia Hubiri Injili Yangu, 3–4).
-
Ni kwa namna gani unaweza kutumia uzoefu wa Paulo kuwasaidia washiriki wa darasa lako kuwa na ujasiri wanapopata ushawishi wa kutoa shuhuda zao? Fikiria kupitia upya kwa pamoja hadithi za maandiko ambazo zinamuelezea Paulo akishuhudia, kama vile matukio yake akiwa Makedonia (ona Matendo ya Mitume 16:19–34), akiwa Athene (ona Matendo ya Mitume 17:16–34), na akiwa Korintho (ona Matendo ya Mitume 18:1–11). Ni ushahidi gani tunapata juu ya uimara na ujasiri wa Paulo? Ni mafundisho gani Paulo alifundisha (na kuelewa) ambayo yalimpa kujiamini katika ujumbe wake? Je, ni kwa nini wakati mwingine tunaogopa kushiriki injili na wengine, na ni kwa namna gani tunaweza kuushinda woga huu? Labda wamisionari wangeweza kutembelea darasa lako na kuelezea jinsi ambavyo wao wamepokea ujasiri wa kushuhudia. Wahamasishe washiriki wa darasa kufikiria njia mojawapo wanayoweza kufuata mfano wa Paulo na kuwa wajasiri zaidi katika kushiriki ushuhuda wao juu ya Kristo na wengine.
Sisi ni uzao wa Mungu.
-
Katika kilima cha Maazi, Paulo alifundisha kuhusu Baba wa Mbinguni kwa kundi la watu ambao walikuwa na ufahamu mdogo kuhusu asili ya kweli ya Mungu. Ili kuchunguza zaidi mafundisho haya, washiriki wa darasa wangeweza kusoma Matendo ya Mitume 17:24–31 na kuandika ubaoni kweli ambazo wanapata kuhusu Baba wa Mbinguni, uhusiano wetu na Yeye, na uhusiano baina yetu sisi kwa sisi. Ni uzoefu gani washiriki wa darasa wanaweza kushiriki ambapo walihisi ukweli wa kauli ya Paulo kwamba Mungu “hayuko mbali na kila mmoja wetu”? (mstari wa 27).
-
Wakati mnapoangalia mistari hii kwa pamoja, fikiria kujadili ukweli uliofundishwa katika mstari wa 29, “Sisi tu wazao wa Mungu,” ikimaanisha kwamba Baba wa Mbinguni ni Baba yetu halisi wa roho zetu. Kufanya hivi, ungeweza kuandika kwenye ubao Kwa kuwa sisi tu watoto wa Mungu na Kama tusingejua kuwa tu watoto wa Mungu. Alika washiriki wa darasa kupendekeza njia za kukamilisha sentensi hizi. Kwa mfano, ukweli kuwa sisi tu watoto wa Mungu unatufundisha nini kuhusu Mungu? Kuhusu sisi wenyewe? Kuhusu jinsi gani tunavyotakiwa kuchukuliana sisi kwa sisi? Je, ni kwa jinsi gani maisha yetu yangekuwa tofauti kama tusingejua kuhusu uhusiano wetu wa kweli na Mungu? Hii inaweza kupelekea kwenye mjadala wa jinsi gani tunaweza kuwasaidia wengine kuelewa kwamba wao ni watoto wa Mungu. Kauli ya Mzee Dallin H. Oaks katika “Nyenzo za Ziada” inaweza kuongezea katika mjadala huu.
Ubatizo lazima ufuatiwe na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu
-
Matendo ya Mitume 19 ni sehemu nzuri ya kusisitiza jinsi gani ilivyo muhimu kuthibitishwa baada ya kubatizwa. Fikiria kuelezea kauli hii kutoka kwa nabii Joseph Smith: “Ubatizo wa maji ni nusu ya ubatizo, na hauna faida yoyote bila nusu nyingine—ambayo ni ubatizo kwa Roho Mtakatifu” (Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith, 95). Ni kwa namna gani mafundisho ya Paulo katika Matendo ya Mitume 19:1–7 yanathibitisha kauli iliyotolewa na Joseph Smith? Washiriki wa darasa wanaweza pia kunufaika kutokana na kutafuta “Roho Mtakatifu, Ubatizo kwa” katika Mwongozo wa Maandiko ili kujifunza zaidi kuhusu baraka zitokanazo na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
Himiza Kujifunza Nyumbani
Ili kuwahimiza washiriki wa darasa kusoma Matendo ya Mitume 22–28 ndani ya wiki ijayo, waulize kitu kama, “kama ungekuwa na nafasi ya kumweleza kiongozi wa taifa kuhusu injili ungesema nini?” Waambie kwamba katika Matendo ya Mitume 22–28, watagundua kile Paulo alichosema kwa baadhi ya viongozi wenye nguvu wa siku zake.
Nyenzo za Ziada
Ujumbe kuhusu kazi ya umisionari.
-
Dallin H. Oaks, “Kushiriki Injili ya Urejesho,” Ensign au Liahona, Nov. 2016, 57–60.
-
David A. Bednar, “Njoo na Uone” Ensign au Liahona, Nov. 2014, 107-10
-
Neil L. Andersen, “Shahidi wa Mungu,” Ensign au Liahona, Nov. 2016, 35–38.
-
Mervyn B. Arnold, “Kuokoa: tunaweza kufanya,” Ensign au Liahona, Mei 2016, 53–55.
-
S. Gifford Nielsen, “Kuharakisha mpango mwaminifu wa Bwana!” Ensign au Liahona, Nov. 2013, 33–35.
Sisi sote tu watoto wa Mungu.
“Familia: Tangazo kwa Ulimwengu” huelezea ukweli wa milele kuhusu uhusiano wetu na Mungu: “Binadamu wote—wa kiume na wa kike—wameumbwa kwa mfano wa Mungu. Kila moja ni mwana au binti mpendwa wa kiroho wa wazazi wa mbinguni, na, kama hivyo, kila moja ana asili na hatima takatifu” (Ensign au Liahona, Nov. 2010, 129).
Mzee Dallin H. Oaks wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alizungumzia kuhusu umuhimu wa sisi wenyewe kujiona kwanza na zaidi ya yote kama watoto wa kiroho wa Mungu:
“Kuwa makini na jinsi gani unavyojichukulia. Usijichukulie au kujipambanua mwenyewe kwa sifa za kupita. Sifa moja pekee ambayo ni lazima iwe kwetu ni kwamba sisi tu wana na mabinti wa Mungu. Ukweli huu unazidi sifa zingine zote, ikijumuisha asili yetu, kazi, sifa za kimaumbile, heshima au hata ushirikishwaji wa kidini. …
“Tunayo haki yetu ya kujiamulia, na tunaweza kuchagua sifa yoyote ile kutuelezea. Lakini tunahitaji kujua kwamba tunapochagua kujipambanua au kujitambulisha kwa baadhi ya sifa ambazo ni za muda au zisizo halisi katika muktadha wa umilele, tunaacha kusisitiza kile ambacho ni muhimu juu yetu, na tunasisitiza zaidi kile ambacho si cha muhimu. Hii inaweza kutupeleka chini kwenye njia isiyo sahihi na kuzuia ukuaji wetu wa milele” (“Kuwa Mwerevu” [Brigham Young University–Idaho devotional, Nov. 7, 2006], byui.edu).