“Julai 29–Agosti 4. Matendo ya Mitume 22–28: ‘Mtumishi na Shahidi’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: Agano Jipya 2019 (2019)
“Julai 29–Agosti 4. Matendo ya Mitume 22–28,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: 2019
Julai 29–Agosti 4
Matendo ya Mitume 22–28
“Mtumishi na Shahidi”
Soma Matendo ya Mitume 22–28 kwa maombi moyoni mwako kwamba Roho Mtakatifu akupe mwongozo wa kiungu ili kujua kile unachotakiwa kuzingatia juu yake ambacho kitawasaidia washiriki wa darasa lako. Andika mawazo yoyote yanayokuja akilini; haya yanaweza kuwa mwanzo wa mpango wako wa kufundisha
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Waombe washiriki wa darasa kuandika andiko la rejeo kutoka Matendo ya Mitume 22–28 ambalo limewavutia wiki hii. Kusanya majibu yao na usome baadhi ya mistari. Alika washiriki kadhaa wa darasa kuelezea ni kwa nini mistari hii ni ya maana kwao.
Fundisha Mafundisho
Matendo ya Mitume 22:1–21; 26:1–29
Ushuhuda ni tangazo kuhusu ukweli kulingana na uelewa au imani ya mtu binafsi.
-
Ushuhuda wa Paulo kwa Festo na Mfalme Agripa unaweza kuwa ni nafasi ya kujadili kutoa ushuhuda humaanisha nini. Unaweza kuanza kwa kuwaomba washiriki wa darasa kurejea Matendo ya Mitume 22:1–21 na 26:1–29. Tunajifunza nini kutokana na mfano wa Paulo kuhusu kutoa ushuhuda? Ni kanuni zipi za ziada tunajifunza kuhusu kutoa ushuhuda kutoka kwenye kauli ya Mzee M. Russell Ballard katika “Nyezo za Ziada”? Kuimba au kucheza wimbo “Testimony” (wimbo, namba. 137) kunaweza kusaidia kumwalika Roho katika majadiliano yenu.
-
Washiriki wa darasa wanaweza kuwa wamepata umaizi binafsi wakati wakisoma ushuhuda wa Paulo kwa Festo na Mfalme Agripa. Waalike kushiriki uzoefu wao. Jibu la Mfalme Agripa kwa ushuhuda wa Paulo lina maonyo gani kwetu leo? (ona Matendo ya Mitume 26:28). Washiriki wa darasa wangeweza pia kufikiri juu ya shuhuda zingine kutoka kwenye maandiko ambazo zimewapa mwongozo wa kiungu. (Baadhi ya mifano hujumuisha Ayubu 19:25–27; 2 Nefi 33:10–15; Alma 5:45–48; na M&M 76:22–24.) Au pengine wangeweza kuelezea matukio ambapo walishawishiwa na ushuhuda wa mtu fulani.
-
Nabii Joseph Smith alilinganisha uzoefu wake wa kushuhudia Ono la Kwanza na uzoefu wa Paulo mbele ya Mfalme Agripa (ona Joseph Smith—Historia 1:24–25). Labda washiriki wa darasa wangefanya kazi katika majozi kutengeneza orodha ya kuonyesha usawa kati ya hawa watumishi wawili wa Mungu. Ni kwa namna gani shughuli hii hutusaidia kuelewa jinsi ya kutoa ushuhuda wetu hata kama kufanya hivyo ni vigumu?
-
Ingawa Paulo hakuwa akitafuta ushahidi wa kiroho alioupokea akiwa njiani kwenda Dameski, alitumia maisha yake yote yaliyobakia akifanya kazi kuutunza na kuulinda ushuhuda wake (ona Matendo ya Mitume 22:10, 14–16; 26:19). Mfano wa Paulo unaweza kuwasaidia washiriki wa darasa lako kuelewa kwamba ushuhuda huhitaji matendo na dhabihu. Ili kuanza majadiliano kuhusu hili, pengine mshiriki wa darasa angeweza kuelezea jitihada zake katika kuwa mwanamuziki hodari, mwana sanaa au mwana riadha. Ni kwa namna gani kukuza ujuzi wa jinsi hii ni sawa na kupata na kuimarisha ushuhuda? Ni juhudi gani lazima tufanye ili kupata na kuimarisha ushuhuda? (Ona pia Alma 5:46).
Tunao wajibu wa kuwahudumia wengine.
-
Bwana alimwita Paulo kuwa “mtumishi” (Matendo ya Mitume 26:16), lakini neno hili linamaanisha nini? Ili kuwasaidia washiriki wa darasa kuchunguza ni kwa jinsi gani wanaweza kuwatumikia wengine, ungeweza kuandika kwenye ubao swali kama Kutumikia kunamaanisha nini? Alika washiriki wa darasa kutafuta majibu katika nyezo zifuatazo: Mathayo 20:25–28; Matendo ya Mitume 26:16–18; 3 Nefi 18:29–32; Mwongozo wa Maandiko, “kuhudumu,” scriptures.lds.org. Wakati wakielezea walichokipata, wahimize kujadili jinsi ambavyo tunaweza kuwatumikia wengine, ikijumuisha katika miito yetu kanisani.
-
Ndugu David L. Beck alizungumzia kuhusu majukumu ya akina kaka wa ukuhani kuhudumia wengine, na utambuzi wake mwingi unaoweza kutumiwa na wale wote wanaotumikia Kanisani (ona “Your Sacred Duty to Minister,” Ensign au Liahona, Mei 2013, 55–57). Kwa mfano, ni kwa namna gani hadithi ya Chy Johnson hutufundisha kuhusu kuwahudumia wengine? Video “The Miracle of the Roof” (LDS.org) ni mfano mzuri pia wa kuhudumia. Ni mifano gani mingine washiriki wa darasa wanaweza kuelezea? Wape washiriki wa darasa muda wa kumfikiria mtu ambaye wanaweza kumhudumia wiki hii na ni kwa namna gani watafanya hivyo.
Kama tutawatii manabii wa Bwana, Yeye atatuongoza na kutulinda dhidi ya uovu.
-
Yawezekana washiriki wa darasa lako wanao uzoefu wakati walipofuata mwongozo wa manabii hata wakati ulipopingana na ushauri wa wataalam waliobobea wa kidunia na mawazo ya watu wanaowazunguka. Waalike baadhi ya washiriki wa darasa waje wakiwa wamejiandaa kuelezea uzoefu huo. Kisha waalike washiriki wa darasa kuelezea ni kwa namna gani watu kwenye meli walimjibu Paulo wakati alipotoa unabii kuwa meli ingepata “madhara na hasara nyingi” (Matendo ya Mitume 27:10). Ni kwa namna gani majibu ya baadhi ya watu kwa ushauri wa kinabii ni sawa katika siku yetu?
-
Tunajifunza nini kutoka Matendo ya Mitume 27 Kuhusu kuwafuata manabii wa Bwana? Nukuu toka kwa Mzee Ronald A. Rasband katika “Nyenzo za Ziada” inajumuisha maswali ya kutafakari na orodha ya hatari ambazo manabii wa sasa wametuonya dhidi yake. Ni kwa namna gani tumeweza kubarikiwa kwa kufuata ushauri wa manabii wanaoishi?
Himiza Kujifunza Nyumbani
Ili kusaidia kuwapa msukumo washiriki wa darasa kuanza kusoma nyaraka za Paulo, waombe wavute taswira kwamba mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili aliandika barua binafsi katika kata yako. Je, tungehisi vipi kuhusu barua hiyo? Je, angeweza kusema nini kwetu sisi? Alika washiriki wa darasa kuweka mawazo hayo katika akili zao wanaposoma barua ya Paulo kwa Watakatifu wa Rumi.
Nyenzo za Ziada
Kutoa ushuhuda.
Mzee M. Russell Ballard aliongelea kuhusu ushuhuda wa Paulo mbele ya Mfalme Agripa na kufundisha inamaanisha nini kwetu kutoa ushuhuda:
“Mikutano yetu ya kutoa ushuhuda inahitaji kujikita zaidi katika Mwokozi, mafundisho ya injili, baraka za Urejesho, na mafundisho ya maandiko. Tunahitaji kubadilisha hadithi, filamu na mhadhara kwa shuhuda safi. Wale ambao wameaminiwa kuongea na kufundisha katika mikutano yetu wanahitaji kufanya hivyo kwa nguvu za mafundisho ambazo zitasikika na kugusa mioyo, wakiinua roho na kuwajenga watu wetu. …
“… Wakati ni vizuri daima kuonyesha upendo na shukrani, mitazamo hiyo haijumuishi aina ya ushuhuda ambao utawasha moto wa imani katika maisha ya wengine. Kushuhudia ni ‘kutoa ushahidi kwa nguvu ya Roho Mtakatifu; kutoa tamko la dhati juu ya ukweli kulingana na uelewa binafsi au imani’ [Mwongozo wa Maandiko, “Shuhudia,” scriptures.lds.org]. Tamko wazi la ukweli huleta tofauti katika maisha ya watu. Hiki ndicho kinachobadili mioyo. Hiki ndicho ambacho Roho Mtakatifu anaweza kukishuhudia katika mioyo ya watoto wa Mungu” (“Ushuhuda Halisi,” Ensign au Liahona, Nov. 2004, 41).
Kusimama na viongozi wa Kanisa.
Mzee Ronald A. Rasband alifundisha:
“[Viongozi wetu], kwa mwongozo wa kiungu, wameitwa kutufundisha na kutuongoza na … wanatoa wito kwetu kuwa makini na hatari ambazo tunakumbana nazo siku hadi siku—kutoka kutotii sabato kikamilifu, mpaka vitisho kwa familia, mashambulio katika uhuru wa kidini na hata mabishano juu ya ufunuo wa siku za mwisho. Akina kaka na akina dada, je, tunasikiliza ushauri wao? …
“Tunaposonga mbele, tukichagua kufuata ushauri na maonyo ya viongozi wetu, tunachagua kumfuata Bwana wakati ulimwengu ukielekea upande mwingine. Tunachagua, kushikilia fimbo ya chuma, kuwa Watakatifu wa Siku za Mwisho, kuwa upande wa Bwana, na kujazwa “na shangwe kubwa’ [1 Nefi 8:12].
Swali linaloendelea leo lipo wazi: je, unasimama pamoja na viongozi wa Kanisa katika ulimwengu wa giza ili uweze kueneza Nuru ya Kristo?” (“simama na Viongozi wa Kanisa,” Ensign au Liahona, Mei 2016, 47–48).