“Oktoba 3–9. Isaya 58–66: “Mkombozi Atakuja Sayuni,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: Agano la Kale 2022 (2021)
“Oktoba 3–9. Isaya 58–66,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: 2022
Oktoba 3–9
Isaya 58–66
“Mkombozi Atakuja Sayuni”
Unapojifunza mafundisho mazuri katika sura hizi, mwalike Roho akuongoze kwenye ujumbe ambao utakuwa na maana zaidi kwa washiriki wa darasa.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Ungeweza kuwaalika washiriki wa darasa kuandika ubaoni marejeo ya mistari ambayo imewagusa wakati wa kujifunza kwao kwa maandiko wiki hii. Kama darasa, unaweza kisha kuangalia mistari hii na kuzungumza kuhusu ukweli unaopatikana humo. Umaizi huu unaweza kuongoza hata kwenye mazungumzo ya kina ya kanuni moja au zaidi zilizoorodheshwa hapa chini.
Fundisha Mafundisho
Mfungo huleta baraka.
-
Ili kuwasaidia washiriki wa darasa kujadili kwa nini na jinsi Bwana ametuamuru sisi kufunga, unaweza kutengeneza safu mbili ubaoni zilizoandikwa “Hamfungi Kama Mfanyavyo Siku Hii ya Leo” na “Saumu Niliyoichagua Mimi.” Kisha washiriki wa darasa wanaweza kusoma Isaya 58:3–7, kujaza safu ya kwanza na maelezo ya jinsi Waisraeli walivyokuwa wakifunga na safu ya pili maelezo ya kufunga kama vile Bwana anavyodhamiria. Ni kwa jinsi gani maelezo haya yanaathiri jinsi tunavyoona kufunga? Washiriki wa darasa wanaweza kushiriki jinsi, katika uzoefu wao, kufunga kunavyotuongoza kwenye baraka alizoahidi Bwana katika mstari wa 8–12.
-
Baadhi ya washiriki wa darasa wanaweza kuwa walipata uzoefu katika kuelezea wengine kwa nini tunafunga. Waalike kuelezea kile wao walichosema. Ungeweza pia kumwalika mshiriki wa uaskofu kuzungumzia kuhusu jinsi matoleo ya mfungo yanavyotumika. Au unaweza kushiriki mojawapo ya mifano kutoka katika ujumbe wa Rais Henry B. Eyring “Je, Saumu Niliyoichagua, Siyo ya Namna Hii?” (Liahona, Mei 2015, 22–25). Je, kufunga na kulipa matoleo ya mfungo husaidiaje “kuzilegeza kamba za nira” zetu wenyewe na wengine? (Isaya 58:6).
Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wetu.
-
Wakati Yesu Kristo alipotangaza kwa watu wa Nazareti kwamba Yeye alikuwa Masiya, Yeye alinukuu kutoka katika Isaya 61:1–3 (ona Luka 4:16–21; ona pia video “Jesus Declares He Is the Messiah,” ChurchofJesusChrist.org). Labda washiriki wa darasa wangeweza kusoma Isaya 61:1–3 na kuzungumzia kuhusu kwa nini mistari hii ni maelezo mazuri ya huduma ya Mwokozi. Unaweza kuorodhesha ubaoni kila kitu ambacho Mwokozi alipakwa mafuta ili kufanya na jadili kila kimoja kinamaanisha nini. Je, Mwokozi alitimizaje vipengele vya huduma Yake wakati wa maisha Yake duniani? Je, Yeye amevitimizaje katika maisha yetu?
-
Washiriki wa darasa kisha wanaweza pia kusoma Isaya 63:7–9 na kushiriki jinsi Yesu Kristo alivyowabariki wao katika njia hizi.
-
Isaya 61:1–3 hutumia lugha nzuri na ya kishairi kuelezea nguvu za Yesu Kristo za kukomboa kile kinachoonekana kuharibiwa. Ili kusaidia kutoa kielelezo cha mistari hii, fikiria kushiriki hadithi kuhusu kitu ambacho kilidhaniwa kupotea au kuharibika lakini kiligeuzwa kuwa kitu kizuri zaidi. Kwa mfano, tazama video “Provo City Center Temple” (ChurchofJesusChrist.org; ona pia “Nyenzo za Zaida”) au hadithi ya mwanzoni mwa ujumbe wa Rais Dieter F. Uchtdorf “Atakubeba Mabegani Mwake na Kukupeleka Nyumbani” (Liahona, Mei 2016, 101–4). Washiriki wa darasa wanaweza kuzungumza kuhusu namna ambavyo wameona Bwana akiwapa watu kitu kizuri wakati walikuwa wanadhani maisha yao yameharibika.
Katika Ujio wa Pili, Bwana “atatengeneza mbingu mpya na dunia mpya.”
-
Isaya 65:17–25 huelezea hali duniani baada ya Ujio wa Pili wa Mwokozi. Unaweza kuwaalika washiriki wa darasa kupitia tena mistari hii wakitafuta majibu ya maswali kama haya: Je, maisha katika “dunia mpya” yatakuwaje tofauti na maisha yalivyo katika dunia ya sasa? Unapata nini katika mistari hii ambacho kinakusababisha ufurahie?
Nyenzo za Ziada
Bwana “hatuachi katika majivu.”
Baada ya kusimulia jinsi moto karibu uharibu Tabenakulo la Provo, kuwezesha kujengwa tena baadaye kama Hekalu la Provo City Center, Dada Linda S. Reeves alisema: “Mungu huruhusu tujaribiwe na kupimwa, wakati mwingine ili kufikia uwezo wetu wa juu. Tumeona maisha ya wapendwa wetu—na pengine yetu wenyewe—kistiari yakiteketezwa na tumejiuliza ni kwa nini Baba wa Mbinguni mwenye upendo na mwenye kujali angeruhusu mambo kama haya kufanyika. Lakini Yeye hatuachi katika majivu; Anasimama na mikono iliyo wazi, akitualika kwa shauku kuja Kwake. … Yeye anajenga maisha yetu kuwa mahekalu mazuri kabisa mahali ambapo Roho Wake anaweza kukaa milele” (“Dai Baraka za Maagano Yako,” Liahona, Nov. 2013,119).