Mlango wa 46
Amalikia anakula njama kuwa mfalme—Moroni anainua bendera ya uhuru—Anaunganisha watu kulinda dini yao—Waumini wa kweli wanaitwa Wakristo—Baki la Yusufu litahifadhiwa—Amalikia na wakaidi wanatorokea nchi ya Nefi—Wale ambao hawataunga kusudi la uhuru mkono wanauawa. Karibia mwaka 73–72 K.K.
1 Na ikawa kwamba kadiri wengi ambao hawangesikiza maneno ya Helamani na ndugu zake walikusanywa pamoja dhidi ya ndugu zao.
2 Na sasa tazama, walikasirika sana, hata kwamba waliamua kuwaua.
3 Sasa kiongozi wa wale ambao walikasirika dhidi ya ndugu zao alikuwa mtu mkubwa na mwenye nguvu; na jina lake lilikuwa Amalikia.
4 Na Amalikia alitamani kuwa mfalme; na wale watu waliokasirika walitamani kwamba awe mfalme wao; na walikuwa wengi baina yao waamuzi wa vyeo vya chini katika nchi, na waliojitafutia ukubwa.
5 Na walikuwa wameongozwa na udanganyifu wa Amalikia, kwamba ikiwa watamuunga mkono na kumsimamisha kuwa mfalme wao kwamba angewafanya kuwa watawala juu ya watu.
6 Hivyo waliongozwa na Amalikia kwa mafarakano, ijapokuwa kuhubiri kwa Helamani na ndugu zake, ndiyo, ijapokuwa utunzaji wao mkuu juu ya kanisa, kwani walikuwa makuhani wakuu juu ya kanisa.
7 Na kulikuwa na wengi kanisani ambao waliamini maneno ya kusifu uongo ya Amalikia, kwa hivyo walikataa hata kanisa; na hivyo ndivyo mambo ya watu wa Nefi yalikuwa yenye shida nyingi na ya hatari, ijapokuwa ushindi wao mkuu ambao walipata juu ya Walamani, na furaha yao kubwa ambayo walipata kwa sababu ya wokovu wao kupitia mkono wa Bwana.
8 Hivyo tunaona vile watoto wa watu humsahau Bwana Mungu wao haraka, ndiyo, vile hutenda maovu haraka, na kupotoshwa na yule mwovu.
9 Ndiyo, na pia tunaona ule uovu mwingi ambao mtu mmoja aliye mwovu anaweza kusababisha kufanyika miongoni mwa watoto wa watu.
10 Ndiyo, tunaona kwamba Amalikia, kwa sababu alikuwa mtu mjanja na mtu wa maneno mengi ya kusifu ya uongo, kwamba aliongoza mioyo ya watu wengi kufanya maovu; ndiyo, na kutafuta kuangamiza kanisa la Mungu, na kuangamiza msingi wa uhuru ambao Mungu alikuwa amewakabidhi, au baraka ambazo Mungu alituma katika ardhi kwa ajili ya wale walio haki.
11 Na sasa ikawa kwamba wakati Moroni, ambaye alikuwa amiri jeshi mkuu wa majeshi ya Wanefi, aliposikia mafarakano haya, alimkasirikia Amalikia.
12 Na ikawa kwamba alipasua koti lake; na akachukua kipande chake, na kuandika juu yake—Kwa ukumbusho wa Mungu wetu, dini yetu, na uhuru, na amani yetu, wake zetu, na watoto wetu—na akaifunga juu ya mwisho wa mti.
13 Na akajifunga chapeo kwenye kichwa chake, na dirii yake, na ngao yake, na akajifunga silaha yake kiunoni mwake; na akaachukua ule mti, ambao mwisho wake kulikuwa koti lake lililoraruliwa, (na akaiita bendera ya uhuru) na akajiinamisha chini, na akaomba sana kwa Mungu kuwa baraka ya uhuru iwe na ndugu zake, kadiri kundi la Wakristo libaki kumiliki nchi—
14 Kwani ndivyo waumini wa kweli wa Kristo, waliokuwa ndani ya kanisa la Mungu, walivyoitwa na wale ambao hawakuwa wafuasi wa kanisa.
15 Na wale ambao walikuwa wa kanisa walikuwa waaminifu; ndiyo, wale wote ambao waliokuwa waumini wa kweli katika Kristo walijichukulia, kwa furaha, jina la Kristo, au Wakristo vile waliitwa, kwa sababu ya imani yao katika Kristo ambaye angekuja.
16 Na kwa hivyo, kwa wakati huu, Moroni aliomba kwamba nia ya Wakristo, na uhuru wa nchi ungependelewa.
17 Na ikawa kwamba alipokuwa ametoa roho yake yote kwa Mungu, aliita nchi yote iliyo kusini mwa Ukiwa, ndiyo, na kwa ufupi, nchi yote, kaskazini na kusini—Nchi iliyochaguliwa, na nchi ya uhuru.
18 Na akasema: Kwa kweli Mungu hawezi kukubali kwamba sisi, ambao tumedharauliwa kwa sababu tumejichukulia jina la Kristo, tutakanyagwa chini na kuangamizwa, mpaka tujiletee wenyewe maangamizi kwa makosa.
19 Na Moroni aliposema maneno haya, alienda mbele miongoni mwa watu, akipepeza kipande cha vazi lake kilichoraruka hewani, ili wote waone maandishi ambayo aliandika kwenye sehemu iliyoraruka, na akipaza sauti, akisema:
20 Tazama, wowote watakaohifadhi hii bendera katika nchi, hebu waje mbele kwa uwezo wa Bwana, na kufanya agano kwamba watahifadhi haki yao, na dini yao, kwamba Bwana Mungu angewabariki.
21 Na ikawa kwamba wakati Moroni alipokuwa ametangaza maneno haya, tazama, watu walikuja wakikimbia pamoja na silaha zao zikiwa zimefungwa viunoni mwao, wakirarua nguo zao kama ishara, au kama agano, kwamba hawatamwacha Bwana Mungu wao; au, kwa maneno mengine, ikiwa wataasi amri za Mungu, au kuingia kwenye makosa, na wapate aibu kujichukulia jina la Kristo, Bwana angewararua hata kama vile walivyorarua nguo zao.
22 Sasa hili ndilo agano ambalo walifanya, na walitupa nguo zao miguuni mwa Moroni, wakisema: Tunaagana na Mungu wetu, kwamba tutaangamizwa, hata kama vile ndugu zetu katika nchi ya kaskazini, ikiwa tutaingia kwenye makosa; ndiyo, atutupe miguuni mwa maadui zetu, hata vile tumetupa nguo zetu miguuni mwako zikanyagwe chini ya miguu, ikiwa tutaingia kwenye makosa.
23 Moroni akawaambia: Tazama, sisi ni baki la uzao wa Yakobo; ndiyo, ni baki la uzao wa Yusufu, ambaye koti lake liliraruliwa na kaka zake kwa vipande vingi; na sasa tazama, hebu tukumbuke kutii amri za Mungu, au nguo zetu zitararuliwa na ndugu zetu, na tutupwe gerezani, au tuuzwe, au tuuawe.
24 Ndiyo, acha tuhifadhi uhuru wetu kama baki la Yusufu; ndiyo, acha tukumbuke maneno ya Yakobo, kabla ya kifo chake, kwani tazama, aliona kwamba sehemu ya baki la koti la Yusufu ilihifadhiwa na haikuwa imeoza. Na akasema—Hata vile baki la nguo ya mwana wangu limehifadhiwa hata hivyo baki la uzao wa mwana wangu lihifadhiwe kwa mkono wa Mungu, na lirudishwe kwake mwenyewe, wakati baki la uzao wa Yusufu itaangamia, hata vile baki la nguo yake ilikuwa.
25 Sasa tazama, hii inaipatia nafsi yangu huzuni; walakini, nafsi yangu ina shangwe katika mwana wangu, kwa sababu ya sehemu ya uzao wake ambayo itachukuliwa kwa Mungu.
26 Sasa tazama, hii ilikuwa lugha ya Yakobo.
27 Na sasa ni nani anaweza kujua kuwa baki la uzao wa Yusufu, ambalo litaangamia kama nguo yake, ni wale ambao wametukataa sisi? Ndiyo, na hata itakuwa sisi ikiwa hatuwezi kusimama imara katika imani ya Kristo.
28 Na sasa ikawa kwamba Moroni alipokuwa amesema maneno haya alienda mbele, na pia akatuma kwenye sehemu zote za nchi ambako kulikuwa na mafarakano, na akawakusanya watu wote ambao walikuwa wanatamani kuhifadhi uhuru wao pamoja, kusimama dhidi ya Amalikia na wale waliokataa, ambao waliitwa Waamalikia.
29 Na ikawa kwamba wakati Amalikia alipoona kwamba watu wa Moroni walikuwa wengi kuliko Waamalikia—na alipoona pia kwamba watu wake walikuwa na wasiwasi kuhusu haki ya njia ambayo walikuwa wamechukua—kwa hivyo, akiogopa kwamba hatafaulu katika mambo yake, alichukua wale wa watu wake ambao wangekubali na wakaondoka na kwenda kwenye nchi ya Nefi.
30 Sasa Moroni alifikiri haikuwa vyema kwamba Walamani wapate nguvu nyingine; kwa hivyo alifikiri kuwazuia watu wa Amalikia, au kuwachukua na kuwarudisha, na amuue Amalikia; ndiyo, kwani alijua kwamba angewavuruga Walamani kukasirika dhidi yao, na kuwasababisha kuja kwa vita dhidi yao; na hivi alijua kwamba Amalikia angefanya ili apate kufikia lengo zake.
31 Kwa hivyo Moroni alifikiri ilikuwa ya lazima kwamba achukue majeshi yake, ambao walikuwa wamejikusanya wenyewe pamoja, na kujihami wenyewe, na kuingia kwenye agano kuweka amani—na ikawa kwamba alichukua jeshi lake na kwenda taratibu na hema zake kwenye nyika, kuzuia mwendo wa Amalikia nyikani.
32 Na ikawa kwamba alifanya kulingana na tamaa yake, na akaenda taratibu hadi kwenye nyika, na kuuzuia mwendo wa majeshi ya Amalikia.
33 Na ikawa kwamba Amalikia alikimbia na idadi ndogo ya watu wake, na waliosalia waliwekwa kwenye mikono ya Moroni na wakarudishwa katika nchi ya Zarahemla.
34 Sasa, Moroni akiwa ni mtu aliyechaguliwa na waamuzi wakuu na kwa kura ya watu, kwa hivyo alikuwa na uwezo kulingana na hiari yake na majeshi ya Wanefi, kuanzisha na kuwa na uwezo juu yao.
35 Na ikawa kwamba yeyote wa Waamalikia ambaye alikataa kuingia katika agano kuunga mkono njia ya uhuru, kwamba wangehifadhi serikali huru, alisababisha auawe; na kulikuwa tu wachache waliokataa agano la amani.
36 Na ikawa pia, kwamba alisababisha bendera ya uhuru ipeperushwe kwenye kila mnara ambao ulikuwa kote nchini, ambayo ilimilikiwa na Wanefi; na hivyo Moroni alisimika bendera ya uhuru miongoni mwa Wanefi.
37 Na wakaanza kuwa na amani tena nchini; na hivyo wakadumisha amani nchini mpaka karibu mwisho wa mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa waamuzi.
38 Na Helamani na makuhani wakuu pia waliimarisha utaratibu ndani ya kanisa; ndiyo, hata kwa muda wa miaka minne walikuwa na amani nyingi na furaha ndani ya kanisa.
39 Na ikawa kwamba kulikuwa na wengi waliokufa, wakiamini kwa uthabiti kwamba nafsi zao zimekombolewa na Bwana Yesu Kristo; hivyo walitoka duniani wakishangilia.
40 Na kulikuwa na wengi ambao walifariki kwa homa, ambayo kwa misimu fulani mwakani ilikuweko mara kwa mara nchini—lakini sio kwa wingi hivyo na homa, kwa sababu ya ubora wa mimea mingi na mizizi ambayo Mungu alikuwa ametayarisha kutoa mwanzo wa maradhi, ambayo binadamu walikuwa wakishikwa nayo kwa ajili ya hali ya hewa ya nchi—
41 Lakini kulikuwa na wengi waliokufa wakiwa wamezeeka; na wale waliokufa ndani ya imani ya Kristo wanayo furaha ndani yake, vile lazima tuwaze.