Maandiko Matakatifu
Alma 48


Mlango wa 48

Amalikia anachochea Walamani dhidi ya Wanefi—Moroni anawatayarisha watu wake kulinda imani ya Wakristo—Anafurahia uungwana na uhuru na ni mtu mkuu wa Mungu. Karibia mwaka 72 K.K.

1 Na sasa ikawa kwamba, Amalikia alipopokea utawala alianza kuvuta mioyo ya Walamani dhidi ya watu wa Nefi; ndiyo, alichagua watu kuzungumzia Walamani kutoka kwa minara yao, dhidi ya Wanefi.

2 Na hivyo akavuta mioyo yao dhidi ya Wanefi, kwa wingi kwamba katika mwisho wa mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa waamuzi, akiwa ametimiza mipango yake hivyo, ndiyo, akishafanywa mfalme juu ya Walamani, alifikiria pia kutawala nchi yote, ndiyo, na watu wote waliokuwa nchini, Wanefi na pia Walamani.

3 Kwa hivyo alikuwa ametimiza kusudi lake, kwani alikuwa ameshupaza mioyo ya Walamani na akawapofusha akilini, na kuwachochea kuwa na hasira, kwa wingi kwamba waende vitani dhidi ya Wanefi.

4 Kwani alikuwa ameamua, kwa sababu ya wingi wa watu wake, kuwashinda Wanefi na kuwaweka kifungoni.

5 Na hivyo aliweka makapteni wakuu wa Wazoramu, hawa wakiwa wamezoea nguvu za Wanefi, na mahali pao pa kawaida, na sehemu dhaifu za miji yao; kwa hivyo aliwaweka kuwa makapteni wakuu wa majeshi yake.

6 Na ikawa kwamba walichukua kambi yao, na kusonga mbele kuelekea nchi ya Zarahemla katika nyika.

7 Sasa ikawa kwamba wakati Amalikia alikuwa anapokea uwezo kwa hila na udanganyifu, Moroni, kwa upande mwingine, alikuwa anatayarisha akili za watu kwa uaminifu kwa Bwana Mungu wao.

8 Ndiyo, alikuwa akiimarisha majeshi ya Wanefi, na kujenga ngome ndogo, au mahali pa usalama; akitupa kuta za ardhi karibu kufunika majeshi yake, na pia kujenga kuta za mawe kuwazunguka, kuzingira miji yao na mipaka ya nchi yao; ndiyo, kila mahali nchini.

9 Na kwa udhaifu wao aliweka idadi kubwa zaidi ya watu; na hivyo aliweka nguvu na kuimarisha nchi ambayo ilimilikiwa na Wanefi.

10 Na hivyo alikuwa akijitayarisha kulinda uhuru wao, nchi yao, wake zao, na watoto wao, na amani yao, na kwamba wangeishi kwa Bwana Mungu wao, na kwamba wangeshikilia ile ambayo iliitwa na maadui wao imani ya Wakristo.

11 Na Moroni alikuwa mtu mwenye nguvu na uwezo; na alikuwa mtu wa kuelewa kikamilifu; ndiyo, mtu ambaye hakufurahia umwagaji wa damu; mtu ambaye nafsi yake ilijawa shangwe kwa ajili ya uungwana na uhuru wa nchi yake, na wa ndugu zake kutoka kifungo na utumwa;

12 Ndiyo, mtu ambaye moyo wake ulijaa shukrani kwa Mungu wake, kwa maendeleo mengi na baraka ambazo aliwapa watu wake; mtu ambaye alifanya kazi sana kwa ustawi na usalama wa watu wake.

13 Ndiyo, na alikuwa mtu ambaye alikuwa imara katika imani ya Kristo, na aliapa na kiapo kuwa atawalinda watu wake, haki zake, na nchi yake, na dini yake, hata kwenye kumwaga damu yake.

14 Sasa Wanefi walifundishwa vile wanavyoweza kujilinda wenyewe dhidi ya maadui zao, hata kwenye kumwaga damu ikiwa ilihitajika; ndiyo, na walifundishwa kutodhuru, ndiyo, na kutoinua upanga isipokuwa dhidi ya adui, isipokuwa wawe wanahifadhi maisha yao.

15 Na hii ilikuwa imani yao, kwamba kwa kufanya hivyo Mungu angewafanikisha nchini, au kwa maneno mengine, wakiwa waaminifu kwa kutii amri za Mungu kwamba angewafanikisha katika nchi; ndiyo, kuwaonya watoroke, au kuwaandaa kwa vita, kulingana na hatari iliyopo;

16 Na pia, kwamba Mungu angewawezesha kujua wangeenda wapi kujilinda dhidi ya maadui zao, na kwa kufanya hivyo, Bwana angewaokoa; na hii ilikuwa imani ya Moroni, na moyo wake ulifurahi ndani yake; sio kwa kumwaga damu lakini kwa kutenda mema, kwa kuhifadhi watu wake, ndiyo, kwa kutii amri za Mungu, na kuzuia uovu.

17 Ndiyo, kweli, kweli ninavyowaambia, ikiwa watu wote walikuwa, na wako, na ikiwa watakuweko daima, kama Moroni, tazama, hizo nguvu za jehanamu zingetingizika milele; ndiyo, ibilisi hangekuwa na uwezo juu ya mioyo ya watoto wa watu.

18 Tazama, alikuwa mtu kama Amoni, mwana wa Mosia, ndiyo, na hata wana wengine wa Mosia, ndiyo, na pia Alma na wanawe, kwani walikuwa wote watu wa Mungu.

19 Sasa tazama, Helamani na ndugu zake hawakufanya kazi ndogo kwa watu kuliko Moroni; kwani walihubiri neno la Mungu, na walibatiza ubatizo wa toba watu wote ambao wangesikiliza maneno yao.

20 Na hivyo wakaendelea na watu walijinyenyekeza kwa sababu ya maneno yao, kwamba walipendelewa sana na Bwana, na hivyo wakawa huru kutokana na vita na mabishano miongoni mwao, ndiyo, hata kwa muda wa miaka minne.

21 Lakini, vile nimesema, kwenye mwisho wa mwaka wa kumi na tisa, ndiyo, ijapokuwa amani yao miongoni mwao, walilazimishwa bila kupenda kupigana na wenzao, Walamani.

22 Ndiyo, kwa kifupi, vita vyao havikukoma kamwe kwa muda wa miaka mingi na Walamani, ijapokuwa kutopendelea kwao.

23 Sasa, walihuzunika kuchukua silaha dhidi ya Walamani, kwa sababu hawakupendelea umwagaji wa damu; ndiyo, na hii sio yote—walihuzunika kuwa njia ya kuondoa wengi wa ndugu zao nje ya ulimwengu huu hadi kwenye ulimwengu wa milele, kabla ya kujitayarisha kukutana na Mungu wao.

24 Walakini, hawangekubali kuweka chini maisha yao, kwamba wake zao na watoto wao wachinjwe kuuwawa kinyama kwa ukatili na ujeuri wa wale ambao walikuwa siku moja ndugu zao, ndiyo, na walioasi kutoka kanisa lao, na waliwaacha na kujaribu kuwaangamiza kwa kuungana na Walamani.

25 Ndiyo, hawangevumilia kwamba ndugu zao wafurahi juu ya damu ya Wanefi, mradi kuwe na yeyote atakayetii amri za Mungu, kwani ahadi ya Bwana ilikuwa, kama watatii amri zake watafanikiwa nchini.