Mlango wa 2
Wayaredi wanajiandaa kwa safari kuelekea nchi ya ahadi—Ni nchi iliyochaguliwa ambamo kwake watu lazima wamtumikie Kristo au waangamizwe—Bwana anamzungumzia kaka wa Yaredi kwa masaa matatu—Wayaredi wanajenga boti—Bwana anamwuliza kaka wa Yaredi atoe shauri jinsi boti zitakavyopata mwangaza.
1 Na ikawa kwamba Yaredi na kaka yake, na jamaa zao, na pia marafiki za Yaredi na kaka yake na jamaa zao, walienda chini kwenye bonde ambalo lilikuwa upande wa kaskazini, (na jina la lile bonde lilikuwa Nimrodi, ikiwa liliitwa baada ya yule mwindaji mashuhuri) na wanyama wao ambao walikuwa wamewakusanya pamoja, wa kiume na wa kike, wa kila namna.
2 Na waliweka mitego na kushika ndege wa hewani; na pia walitayarisha chombo, ambamo ndani yake wangebebea samaki wa majini.
3 Na pia walijibebea desereti, ambayo, kwa tafsiri, ni nyuki wa asali; na hivyo walibeba vikundi vya nyuki, na kila aina ya kile kilichokuwako juu ya uso wa nchi, mbegu za kila aina.
4 Na ikawa kwamba baada ya hao kuja chini kwenye bonde la Nimrodi Bwana alikuja chini na kuongea na kaka wa Yaredi; na alikuwa kwenye wingu, na kaka wa Yaredi hakumwona.
5 Na ikawa kwamba Bwana aliwaamuru waende mbele nyikani, ndiyo, katika ile sehemu ambako mtu hajawai kuwa. Na ikawa kwamba Bwana aliwaongoza, na alizungumza nao akiwa katika wingu, na akawaonyesha njia ya kusafiri.
6 Na ikawa kwamba walisafiri nyikani, na walijenga boti, ambazo walivuka maji mengi, wakiongozwa wakati wote na mkono wa Bwana.
7 Na Bwana hangekubali kwamba wasimame mbele ya bahari nyikani, lakini alitaka kwamba waje mbele hata mpaka kwenye nchi ya ahadi, ambayo ilikuwa nzuri kuliko nchi zingine zote, ambayo Bwana Mungu alikuwa amehifadhi kwa watu wenye haki.
8 Na alikuwa ameapa kwenye ghadhabu yake kwa kaka wa Yaredi, kwamba yeyote atakayemiliki nchi hii ya ahadi, kutokea wakati huo na kuendelea milele, lazima amtumikie, yule Mungu wa kweli na wa pekee, au waangamizwe utimilifu wa ghadhabu ya Mungu ukiwajia.
9 Na sasa, tunaweza kuona amri za Mungu kuhusu nchi hii, kwamba ni nchi ya ahadi; na taifa lolote litakaloimiliki litamtumikia Mungu, au wataangamizwa wakati utimilifu wa ghadhabu yake, utakuja juu yao. Na utimilifu wa ghadhabu yake huja juu yao baada ya wao kuwa waovu sana.
10 Kwani tazama, hii ni nchi ambayo ni nzuri kuliko nchi zingine zote; kwa hivyo yule atakayeimiliki atamtumikia Mungu au ataangamizwa; kwani ni amri isiyo na mwisho ya Mungu. Na haitakuwako mpaka utimilifu wa uovu miongoni mwa watu wa nchi hii, ndipo wataangamizwa.
11 Na hii itakuja kwenu, Ee ninyi Wayunani, ili mjue amri za Mungu—kwamba mpate kutubu, na msiendelee mpaka utimilifu wa uovu wenu utakavyotimia, kwamba msilete utimilifu wa ghadhabu ya Mungu juu yenu kama wakazi wa nchi hii walivyofanya.
12 Tazama, hii ni nchi nzuri, na taifa lolote litakaloimiliki litakuwa huru kutoka utumwa, na kutoka kifungo, na kutoka kwa mataifa mengine yote chini ya mbingu, ikiwa watamtumikia Mungu wa pekee katika nchi, ambaye ni Yesu Kristo, ambaye amedhihirishwa na vitu ambavyo tumeviandika.
13 Na sasa ninaendelea na maandishi yangu; kwani tazama, ikawa kwamba Bwana alimleta Yaredi na ndugu zake mbele hata kwenye hiyo bahari kubwa ambayo inagawanya nchi. Na walipokaribia bahari walipiga hema zao; na waliita mahala pale Moriankumeri; na waliishi kwenye hema, na wakaishi katika hema kwenye ukingo wa bahari kwa muda wa miaka minne.
14 Na ikawa katika mwisho wa miaka minne kwamba Bwana alikuja tena kwa kaka wa Yaredi, na akasimama katika wingu na kuongea na yeye. Na kwa muda wa masaa matatu, Bwana aliongea na kaka wa Yaredi, na kumkemea kwa sababu hakukumbuka kulilingana jina la Bwana.
15 Na kaka wa Yaredi alitubu uovu aliofanya, na akalilingana jina la Bwana kwa niaba ya ndugu zake aliokuwa nao. Na Bwana akamwambia: Nitakusamehe na ndugu zako kutoka kwa dhambi zao; lakini hutafanya dhambi mara nyingine, kwani utakumbuka kwamba Roho yangu haitajishughulisha na mwanadamu kila mara; kwa hivyo, kama utafanya dhambi mpaka ufike mwisho, utakatiliwa mbali kutoka kwenye uwepo wa Bwana. Na hizi ndizo fikira zangu juu ya nchi ambayo nitakupatia kwa urithi; kwani itakuwa nchi nzuri kuliko nchi zote.
16 Na Bwana alisema: Nenda ufanye kazi na ujenge, aina ya boti ambazo mmejenga hadi sasa. Na ikawa kwamba kaka wa Yaredi alienda kazini, na pia ndugu zake, na kujenga boti kama aina ambazo walikuwa wamejenga, kulingana na mafundisho ya Bwana. Na zilikuwa madogo, na zilikuwa nyepesi juu ya maji, hata kama wepesi wa ndege arukaye juu ya maji.
17 Na zilijengwa kwa aina moja kwamba zilikuwa zimekazwa sana, kwamba zingeshikilia maji kama vile sahani inavyofanya; na chini yake zilikuwa zimekazwa sana kama sahani; na pande zilikuwa zimekazwa kama sahani; na ncha zilichongoka; na juu yake zilikuwa zimekazwa kama sahani; na urefu wake ulikuwa urefu wa mti; na mlango wake, baada ya kufungwa, ulikazika kama sahani.
18 Na ikawa kwamba kaka wa Yaredi aliomba kwa Bwana, akisema: Ee Bwana, nimefanya kazi ambayo uliniamuru, na nimetengeneza boti kama vile ulivyoniongoza.
19 Na tazama, Ee Bwana, ndani yake hamna mwangaza; tutazielekeza wapi? Na pia tutaangamia, kwani ndani yake hatuwezi kupumua, isipokuwa tu hewa iliyomo ndani yake; kwa hivyo tutaangamia.
20 Na Bwana akamwambia kaka wa Yaredi: Tazama, utatoboa tundu upande wa juu, na pia upande wa chini; na wakati mtakapokosa hewa mtafungua tundu na mpokee hewa. Na ikiwa itakuwa kwamba maji yataingia ndani kwenu, tazama, mtafunga tundu, ili msife katika mafuriko.
21 Na ikawa kwamba kaka wa Yaredi alifanya vile, kulingana na Bwana alivyomwamuru.
22 Na akaomba tena kwa Bwana akisema: Ee Bwana, tazama nimefanya hata vile ulivyoniamuru; na nimetayarisha vyombo kwa watu wangu, na tazama hakuna mwangaza ndani yake. Tazama, Ee Bwana, utakubali tuvuke maji haya mengi kwenye giza?
23 Na Bwana akamwambia kaka wa Yaredi: Ungetaka nifanye nini ili muwe na mwangaza kwenye boti zenu? Kwani tazama, hamwezi kuwa na madirisha, kwani yatavunjwa vipande vipande; wala hamwezi kubeba moto, kwani hamtaenda kwa mwanga wa moto.
24 Kwani tazama, mtakuwa kama nyangumi katikati ya bahari; kwani milima ya mawimbi yatawaangukia. Hata hivyo, nitawarudisha juu tena kutoka kwenye kilindi cha bahari; kwani pepo hutoka katika mdomo wangu, na pia mvua na mafuriko hutolewa na mimi.
25 Na tazama, ninawatayarisha dhidi ya vitu hivi; kwani hamwezi kuvuka hiki kilindi kikubwa isipokuwa niwatayarishe dhidi ya mawimbi ya bahari, na pepo ambazo zimevuma, na mafuriko ambayo yatakuja. Kwa hivyo unataka nikutayarishie nini ili muwe na mwangaza ndani ya kilindi cha bahari?