Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 56


Sehemu ya 56

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Kirtland, Ohio, 15 Juni 1831. Ufunuo huu unamrudi Ezra Thayre kwa kutotii ufunuo wa awali (amri iliyotajwa katika aya ya 8), ambayo Joseph Smith alikuwa amepokea kwa ajili yake, ukimwagiza Thayre kuhusu wajibu wake juu ya shamba la Frederick G. Williams ambamo yeye alikuwa akiishi. Ufunuo ufuatao pia unatengua wito wa Thayre wa kusafiri kwenda Missouri pamoja na Thomas B. Marsh (ona sehemu ya 52:22).

1–2, Watakatifu ni lazima wabebe msalaba wao na kumfuata Bwana ili kupata wokovu; 3–13, Bwana huamuru na hutangua, na wenye kiburi hukatiliwa mbali; 14–17, Ole wake tajiri ambaye hatamsaidia maskini, na ole wao maskini ambao mioyo yao haijapondeka; 18–20, Heri maskini walio safi moyoni, kwani watairithi nchi.

1 Sikilizeni, Enyi watu mliolikiri jina langu, asema Bwana Mungu wenu; kwani tazama, hasira yangu inawaka dhidi ya waasi, na wataujua mkono wangu na uchungu wa hasira yangu, katika siku ya kujiliwa na ya ghadhabu juu ya mataifa.

2 Na yule asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata, na kushika amri zangu, huyo hataokolewa.

3 Tazama, Mimi, Bwana, naamuru; na yule ambaye hatatii atakatiliwa mbali katika wakati wangu mwenyewe, baada ya kuwa nimeamuru na amri imevunjwa.

4 Kwa hiyo Mimi, Bwana, ninaamuru, na kutengua, kama nipendavyo; na hii yote itajibiwa juu ya vichwa vya waasi, asema Bwana.

5 Kwa hiyo, ninateangua amri ambayo ilitolewa kwa watumishi wangu Thomas B. Marsh na Ezra Thayre, na ninatoa amri mpya kwa mtumishi wangu Thomas, kwamba aanze safari yake haraka kwenda nchi ya Missouri, na mtumishi wangu Selah J. Griffin aende pia pamoja naye.

6 Kwani tazama, mimi nitatangua amri ambayo ilitolewa kwa watumishi wangu Selah J. Griffin na Newel Knight, katika matokeo ya kiburi cha watu wangu walioko Thompson, na uasi wao.

7 Kwa hiyo, wacheni mtumishi wangu Newel Knight abaki pamoja nao; na wale wote watakaokwenda na waende, wale walio wanyoofu mbele zangu, na waongozwe naye kwenda kwenye nchi niliyoiteua.

8 Na tena amini ninawaambia, kwamba mtumishi wangu Ezra Thayre ni lazima atubu kwa majivuno, na uchoyo wake, na atii amri zilizopita nilizompa juu ya mahali anapoishi.

9 Na kama atayafanya haya, na pasiwepo na mgawanyo wa ardhi hiyo, bado atateuliwa kwenda katika nchi ya Missouri;

10 Na vinginevyo atarejeshewa fedha alizolipa, na kuondoka mahali hapo, na atakatiliwa mbali kutoka katika kanisa langu, asema Bwana Mungu wa majeshi;

11 Na ingawa mbingu na dunia zitapita, maneno haya hayatapita kamwe, bali yatatimilizwa.

12 Na kama mtumishi wangu, Joseph Smith, Mdogo, itambidi kulipa fedha hizo, tazama, Mimi, Bwana, nitamlipa yeye tena katika nchi ya Missouri, ili kwamba wale ambao atapokea kutoka kwao waweze kupata thawabu tena kulingana na yale wanayofanya;

13 Kwani kulingana na kile ambacho wanakifanya watapokea, hata katika ardhi kwa urithi wao.

14 Tazama, hivyo ndivyo asemavyo Bwana kwa watu wangu—mnayo mambo mengi ya kufanya na kuyatubu; kwani tazama, dhambi zenu zimenifikia, na hazisameheki, kwa sababu ninyi mnashauriana katika njia zenu wenyewe.

15 Na mioyo yenu hairidhiki. Na wala haitii ukweli, bali mnafurahia katika dhuluma.

16 Ole wenu ninyi watu matajiri, ambao hamtatoa vitu vyenu kwa maskini, kwani utajiri wenu utaziharibu roho zenu; na huku kutakuwa kuomboleza kwenu katika siku ya kujiliwa, na ya hukumu, na ya hasira ya uchungu: Mavuno yamepita, na kiangazi kimeisha, na nafsi yangu haikuokolewa!

17 Ole wenu ninyi watu maskini, ambao mioyo yenu haijapondeka, ambao roho zenu siyo nyoofu, na ambao matumbo yenu hayatosheki, na ambao mikono yenu haijizuii kuchukua mali ya watu, ambao macho yenu yamejaa uroho, na ambao hamfanyi kazi kwa mikono yenu wenyewe!

18 Lakini heri maskini walio safi moyoni, ambao mioyo yao imevunjika, na roho zao zimepondeka, kwa kuwa watauona ufalme wa Mungu ukija katika nguvu na utukufu mwingi kwa ukombozi wao; kwani vinono vya nchi vitakuwa vyao.

19 Kwani tazama, Bwana atakuja, na ujira wake utakuwa pamoja naye, na atamlipa kila mtu, na maskini atafurahi;

20 Na vizazi vyao vitairithi dunia kutoka kizazi hadi kizazi, milele na milele. Na sasa nimefika mwisho wa kusema nanyi. Hivyo ndivyo. Amina.