TJS, Mwanzo 50:24–38. Linganisha na Mwanzo 50:24–26; 2 Nefi 3:4–22
Yusufu akiwa Misri anatoa unabii wa Musa akikomboa Waisraeli toka katika utumwa wa Wamisri; juu ya tawi la uzao wa Yusufu likiongozwa hata nchi ya mbali, mahali ambako watakumbukwa katika maagano ya Bwana; juu ya Mungu kumwita nabii wa siku za mwisho aitwaye Joseph ili kuunganisha kumbukumbu ya Yuda naya Yusufu; na juu ya Haruni kutumikia kama msemaji wa Musa.
24 Na Yusufu akawaambia kaka zake, ninakufa, na ninaenda kwa baba zangu; na ninashuka katika kaburi langu kwa shangwe. Mungu wa baba yangu Yakobo na awe pamoja nanyi, kuwakomboa kutokana na mateso katika siku za utumwa wenu, kwa maana Bwana amenijilia, nami nimepata ahadi ya Bwana, kwamba kutoka tunda la viuno vyangu, Bwana Mungu ataliinua tawi lenye haki kutoka viunoni mwangu, na kwenu ninyi, ambao baba yangu Yakobo amewapa jina Israeli, Nabii; (siyo Masiya ambaye anaitwa Shilo;) na nabii huyu atawakomboa watu wangu kutoka Misri katika siku za utumwa wenu.
25 Na itakuwa kwamba watatawanywa tena; na tawi litavunjwa nalo litachukuliwa katika nchi ya mbali; hata hivyo watakumbukwa katika agano la Bwana, wakati Masiya ajapo; kwani atajionesha kwao katika siku za mwisho katika uwezo wa Roho; na atawatoa gizani na kuwaingiza katika nuru; kutoka giza lililofichika, na kutoka kifungo na kuwaweka huru.
26 Mwonaji Bwana Mungu wangu atamwinua, ambaye atakuwa mwonaji bora kwa tunda la viuno vyangu.
27 Hivyo ndivyo asemavyo Bwana Mungu wa baba zangu kwangu, Mwonaji bora nitamwinua kutoka tunda la viuno vyangu, naye ataheshimiwa sana miongoni mwa tunda la viuno vyako; na kwake yeye nitatoa amri ili afanye kazi kwa ajili ya tunda la viuno vyako, ndugu zake.
28 Naye atawafanya wafahamu maagano ambayo nimeyafanya pamoja na baba zako; naye atafanya kazi yoyote nitakayomwamuru.
29 Nami nitamfanya yeye kuwa mkuu machoni mwangu, kwa maana atafanya kazi yangu; na atakuwa mkuu kama yule ambaye nimesema nitamwinua kwenu, ili kuwakomboa watu wangu, Ee nyumba ya Israeli, kutoka nchi ya Misri; maana mwonaji nitamwinua ili kuwakomboa watu wangu kutoka nchi ya Misri; naye ataitwa Musa. Na kwa jina hili yeye atajua kwamba yeye ni wa nyumba yako; kwa maana atatunzwa na binti wa mfalme, naye ataitwa mwana wake.
30 Na tena, mwonaji nitamwinua kutoka tunda la viuno vyako, na kwake yeye nitatoa uwezo wa kulitoa neon langu kwa uzao wa viuno vyako; na siyo kwa kulitoa neno langu tu, asema Bwana, bali hata kuwashawishi wao juu ya neno langu, ambalo litakuwa tayari limeenea miongoni mwao katika siku za mwisho;
31 Kwa sababu hiyo tunda la viuno vyako litaandika, na tunda la viuno vya Yuda litaandika; na kile ambacho kitabaki kwa tunda la viuno vyako, na pia kile kitakachoandikwa na tunda la viuno vya Yuda, vitakuwa pamoja, hata kwa ajili ya kuyashinda mafundisho ya uongo, na kuyaweka chini mabishano, na kusitawisha amani miongoni mwa tunda la viuno vyako, na kuwaleta katika maarifa ya baba zao katika siku za mwisho; na pia katika maarifa ya maagano yangu, asema Bwana.
32 Na kutoka kwenye unyonge atafanywa kuwa mwenye nguvu, katika siku ile ambapo kazi yangu itaanza miongoni mwa watu wangu wote, ambao atawarejesha walio wa nyumba ya Israeli, katika siku za mwisho.
33 Na huyo mwonaji nitambariki, nao wale watafutao kumwangamiza watashindwa; kwa maana ahadi hii ninawapa ninyi; kwani nitawakumbuka ninyi kutoka kizazi hadi kizazi, na jina lake litaitwa Joseph, nalo litakuwa kama jina la baba yake; naye atakuwa kama wewe; kwa maana mambo ambayo Bwana atayafanya kwa mkono wake yatawaleta watu wangu kwenye wokovu.
34 Na Bwana akamwapia Yusufu kwamba yeye atauhifadhi uzao wake milele, akisema, Nitamwinua Musa, na fimbo itakuwa mkononi mwake, naye atawakusanya pamoja watu wangu, na atawaongoza kama kundi, na atayapiga maji ya Bahari ya Shamu kwa fimbo yake.
35 Naye atakuwa na hukumu, na ataandika neno la Bwana. Naye hataongea maneno mengi, kwani nitamwandikia sheria yangu kwa kidole cha mkono wangu mwenyewe. Nami nitamfanyia msemaji, na jina lake ataitwa Haruni.
36 Na itafanyika kwako katika siku za mwisho pia, hata kama vile nilivyoapa. Kwa hiyo, Yusufu aliwaambia ndugu zake, hakika Mungu atawatembelea ninyi, na kuwatoa kutoka nchi hii, kwenda nchi ambayo aliapa kwa Ibrahimu, na kwa Isaka, na kwa Yakobo.
37 Na Yusufu aliyathibitisha mambo mengine mengi kwa ndugu zake, na kufanya kiapo cha wana wa Israeli, akiwaambia, Hakika Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu.
38 Basi Yusufu akafa akiwa na umri wa miaka mia na kumi; na wakampaka dawa, na wakamtia katika jeneza huko Misri; naye hakuzikwa na wana wa Israeli, ili apate kuchukuliwa na kuzikwa katika kaburi pamoja na baba yake. Na hivyo walikumbuka kiapo ambacho waliapa kwake.