TJS, Isaya 29:1–8. Linganisha na Isaya 29:1–8
Ujumbe ambao mwanzo ulihubiriwa Yerusalemu na manabii wa kale utahubiriwa siku za mwisho kutoka Kitabu cha Mormoni, kilichopatikana “kutoka ardhini.”
1 Ole kwa Arieli, kwa Arieli, jiji ambamo Daudi aliishi! Ongeza mwaka kwa mwaka; waache watoe kafara za kuteketeza.
2 Bado nitautesa Ariel, kutakuwapo na maombolezo na kilio; kwani hivyo ndivyo Bwana alivyoniambia, Itakavyokuwa kwa Ariel;
3 Kwamba Mimi Bwana nitapanga majeshi kuzunguka pande zote, na nitauzingira mji kwa mlima, na nitajenga ngome dhidi yake.
4 Na atashushwa na atasema kutoka ardhini, na maneno yake yatakuwa ya chini kutoka mavumbini; na sauti yake itakuwa kama ya mtu mwenye pepo, kutoka ardhini, na maneno yake yatanongʼona kutoka mavumbini.
5 Aidha wingi wa adui zake utakuwa kama vumbi jembamba, na wingi wa watishao utakuwa kama makapi yapitayo; ndiyo na utakuja bila kukawia na kwa ghafla.
6 Kwani watatembelewa na Bwana wa majeshi kwa ngurumo za radi na kwa tetemeko la ardhi, na sauti kuu, na chamchela na tufani, na mwali wa moto uteketezao.
7 Na wingi wa mataifa yote ambayo yanapigana dhidi ya Ariel, hata yale yote yanayopigana dhidi yake na silaha zake, na hiyo inamtesa, itakuwa kama ndoto ya maono ya usiku.
8 Tena, itakuwa kwao kama mtu mwenye njaa anayeota, na tazama anakula, lakini anapoamka, nafsi yake bado ina njaa; au kama mtu mwenye kiu anaye ota, na tazama, anakunywa lakini anapoamka, na tazama anazimia, na nafsi yake inatamani. Tena, hata hivyo ndivyo itakavyokuwa huo wingi wa mataifa ambayo yanapigana dhidi ya mlima Sayuni.