TJS, Zaburi 14:1–7. Linganisha na Zaburi 14:1–7
Mtunga Zaburi anaona upotevu wa ukweli katika siku za mwisho na anatazamia kuanzishwa kwa Sayuni.
1 Mpumbavu amesema moyoni mwake, Hakuna mtu ambaye amemwona Mungu. Kwa sababu yeye hajionyeshi kwetu, kwa hiyo hakuna Mungu. Tazama, wameharibika; wamefanya machukizo, na hakuna kati yao atendaye mema.
2 Kwa maana toka mbinguni Bwana aliwachungulia wanadamu, na kwa sauti yake akawaambia watumishi wake, Tafuteni ninyi miongoni mwa wanadamu, kuona kama yupo mtu yeyote ambaye anamfahamu Mungu. Naye akafungua kinywa chake kwa Bwana, na kusema, Tazama, hawa wote husema wao ni wako.
3 Bwana akajibu, na kusema, Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, huwezi kumwona yeyote kati yao atendaye mema, la, hata mmoja.
4 Wote walio nao kama walimu wao ni watenda maovu, na hakuna maarifa ndani yao. Wao ndiyo wale, walao watu wangu. Wao hula mkate na hawamlingani Bwana.
5 Wao wapo katika hofu kubwa, kwa maana Mungu hukaa katika kizazi cha wenye haki. Yeye ni mshauri wa maskini, kwa sababu wanaaibishwa na uovu, na kukimbilia kwa Bwana, maana ni kimbilio lao.
6 Wao wanaaibika kwa sababu ya shauri la mnyonge kwa sababu Bwana ndiyo kimbilio lake.
7 Laiti Sayuni ingeanza kutoka mbinguni, huo wokovu wa Israeli. Ee Bwana, ni lini utaianzisha Sayuni? Bwana awarudishapo wafungwa wa watu wake, Yakobo atashangilia, na Israeli atafurahi.