2021
Matendo Madogo Madogo ya Kujali na Upendo Huimarisha maisha Yetu
Februari 2021


UJUMBE WA KIONGOZI WA UKUHANI

Matendo Madogo Madogo ya Kujali na Upendo Huimarisha maisha Yetu

“Kama vile mjane wa Sarepta ambaye unga wake haukupunguka, na mafuta hayakuisha, akiba yetu ndogo nyumbani haikuisha.Tulipata hisia ya faraja na utulivu—na kwamba yote yangekuwa sawa kwa familia yetu.”

Janga la ulimwengu la COVID-19 limeathiri ulimwengu mzima, likitusukuma kubadili tabia fulani, na hata mtindo wetu wa maisha. Hata hivyo, kuna mambo halikuweza kubadili. Halingeweza kubadili upendo wetu na kujitolea kwetu kwa Mungu vilevile utayari wetu kwenye kupendana, kutumikiana, na kuhudumiana. Zaidi, hitaji letu la kupendana, kutumikiana na kuhudumiana halijawahi kuwa la lazima na muhimu kiasi hiki.

Siku zote nimekuwa nikishangazwa na mfano mkamilifu wa huduma iliyotolewa na Bwana wetu Yesu Kristo. Wakati Mwokozi anapowatembelea Wanefi baada ya ufufuko Wake, anakutana na kundi la watu elfu mbili na mia tano pale. Katika 3 Nefi mlango wa 17, hata hivyo, tunasoma kwamba—licha ya idadi kubwa ya watu—Mwokozi anafanikiwa kumhudumia kila mtu mmoja mmoja. Acha kwa ufupi tuchanganue mistari michache kutoka kwenye mlango huu:

Katika mstari wa 2, anagundua kwamba wao ni wadhaifu. Katika mstari wa 5, anagundua kwamba wanalia na anaelewa hitaji lao la kumwomba Yeye akae nao. Katika mstari wa 7, anauliza wale wote wenye mahitaji maalum au matatizo—na anaomba kwamba waletwe kwake kwa ajili ya uponyaji. Mstari wa 9 unaeleza kwamba anawaponya kila mmoja wao. Katika mstari wa 11, anaamuru kwamba watoto wadogo waletwe kwake; na katika mstari wa 21, tunasoma “. . . Akachukua watoto wao wachanga, mmoja mmoja, na kuwabariki, na kuomba kwa Baba juu yao.”

Kutoka kwenye mistari hii michache, tunaweza kuelewa na kujifunza mambo mengi kuhusu huduma kutoka kwa Mwokozi mwenyewe:

  • Huduma inafokasi kwa “watoto” na wale ambao ni wadhaifu.

  • Wakati tunapokuwa na tamanio la kuhudumu, Roho Mtakatifu anaweza kutuwezesha kujua mahitaji ya wengine hata kama hayakuelezewa kwa maneno.

  • Huduma inajumuisha kuwatafuta wenye mahitaji.

  • Huduma humaanisha kumsaidia mtu, kwa sababu hata katika kila familia, kila mwanafamilia anaweza kuwa na mahitaji maalum.

Ninakumbuka muda kitambo uliopita, mimi na mwenza wangu tulikuwa tukihudumu katika familia yenye watu wa umri tofauti (wakati huo ilikuwa ikiitwa Mafundisho ya Nyumbani). Mwenza wangu angetoa somo kutoka kwenye ujumbe wa Urais wa Kwanza wa kila mwezi, na ili niweze kuongezea alichokisema, ningefokasi kwa watoto, nikifungamanisha masomo kwenye mahitaji na kiwango chao ili kuhakikisha uwezo wa kufahamu. Siku moja mwishoni mwa moja ya matembezi, mmoja wa wazazi alielezea shukrani zake kwa uhalisia ambao matembezi haya yalikuwa na maana tofauti kwa watoto wao—na hata maana zaidi kwa wazazi kwa sababu tulikuwa tunakidhi mahitaji ya kila mmoja katika nyumba yao.

Akizungumza juu ya wakati wa janga la ulimwengu la COVID-19, Mzee D. Todd Christofferson, wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, alisema ulikuwa ni wakati ambao ulihitaji kuwa na “ufahamu endelevu wa ustawi wa watu wanaokuzunguka.”1 Wengi wetu tulipitia hofu na huzuni kutokana na mashaka yaliyosababishwa na ugonjwa wa COVID-19. Zuio lilitulazimisha kusalia nyumbani kuzuia migusano yote ya kimwili na wengine. Kwa kuongezea, hii ilileta fursa kubwa kwa familia yetu kuelezea upendo wetu, kutumikia na kuhudumu. Na tuna shukrani kwamba wakati mwingine tuliweka azimio, kama familia, kusahau kuhusu sisi kwa manufaa ya watu wengine. Tulihudumu kupitia teknolojia, tukiwapigia watu ambao tuliwafikiria walikuwa wameathiriwa zaidi na janga ili kuwapa faraja na kusikia kuhusu mahitaji yao. Nyakati zingine, ilikuwa ni arafa ya maneno machache tu au ujumbe mfupi wa mitandao ya kijamii.

Ili kujiandaa kwa ajili ya karantini, kama ilivyo kwa watu wengi, tuliweka akiba ya vitu muhimu, na hata kiasi cha pesa taslimu. Lakini tulijifunza kwamba tamanio letu la kuhudumu lilituwezesha kuwafikia wengine iwe kwa juhudi zetu wenyewe au kupitia kuomba kwao. Japokuwa hatukujua zuio lingedumu kwa muda gani, hatukusita kujitolea chakula na nyakati zingine pesa kutoka kwenye akiba yetu ndogo kwa familia chache na watu ambao walikua kwenye uhitaji (ndiyo, huku tukichukua tahadhari muhimu za afya). Maelekezo ya Mwokozi yaliyotolewa kwa wanafunzi Wake wapya aliokuwa Amewachagua na kuwaita kati ya Wanefi yalitupa faraja: “. . . Kwani tazama, ni nyinyi ambao nimewachagua kuwahudumia hawa watu . . . msisumbukie maisha yenu, ni nini mtakula, au ni nini mtakunywa” (3 Nefi 13:25).

Hakuna maneno yanayoweza kuelezea tuzo tuliyoipata. Kama vile mjane wa Sarepta ambaye unga wake haukupunguka, na mafuta hayakuisha (ona 1 Wafalme 17:16); akiba yetu ndogo nyumbani haikuisha. Tulipata hisia za faraja na utulivu wakati wa kipindi hiki kigumu na hisia ya ujasiri kwamba yote yangekuwa sawa kwa familia yetu. Kaka mmoja alituandikia punde baadaye: “Nimekuwa nikiwafikiria leo tangu asubuhi. Ninatambua jinsi matendo yenu madogo madogo ya kujali na upendo yanavyoimarisha maisha yetu na kutupatia nguvu ya kuendelea kwa moyo wa furaha. Hilo linatambulika. Asanteni kwa njia hizi ndogo ndogo ambazo maisha yenu yamejikita juu yake wakati wa huduma yenu. Mnasikiliza. Tafadhali fahamuni kwamba matendo yenu madogo madogo yanaleta tofauti. Asanteni.”

Ninashuhudia kwamba nyakati zingine neno rahisi, ujumbe mfupi, tabasamu la upendo, kipande cha mkate au jicho lenye kujali kwa wengine huleta tofauti kubwa. Upendo na matokeo yake, huduma, ni kiini hasa cha injili ya Yesu Kristo.

Eustache Ilunga aliitwa kama Sabini wa Eneo mnamo Aprili 2018. Yeye na mke wake, Mamie, ni wazazi wa watoto wanne. Mzee na Dada Ilunga wanaishi Kinshasa, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.

MUHTASARI

  1. Sarah Jane Weaver, “Chungeni Ustawi wa Waseja, Mzee Christofferson Anasema wakati Anaposhiriki Njia za Kunusurika Upweke wa COVID-19,” Mei 7, 2020, newsroom.churchofjesuschrist.org.