2021
Kigingi cha Kwanza Afrika
Februari 2021


SEHEMU YA HISTORIA YA KANISA

Kigingi cha Kwanza Afrika

“Mwaka huu tunasherehekea kumbukizi ya miaka 50 ya uanzishwaji wa kigingi cha kwanza Afrika.”

Mnamo Aprili 1970, zaidi kidogo ya miaka 50 iliyopita, kichwa cha habari cha Cumorah’s Southern Messenger kilivumisha habari: Afrika Kusini Kuunda Kigingi! Kilikuwa kigingi cha kwanza cha Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kilichoanzishwa katika bara la Afrika na tukio la maana sana na la kukumbukwa kwa waumini wa Kanisa waliokuwa wakiishi ndani ya mipaka ya Misheni ya Afrika Kusini kwa wakati huo.

Cumorah’s Southern Messenger lilikuwa chapisho la kila mwezi la misheni—na lilijumuisha habari ya kila kitu kuanzia ubatizo na baraka kwa watoto mpaka “mikusanyiko,” ya misheni ambayo sasa huitwa mikutano.

Wamisionari walikuwa wametarajia ujio wa Mzee Marion G. Romney (1897–1988), wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, kwenye mkutano wao wa katikati ya mwezi Machi wa mwaka 1970, lakini si hata mmoja wao aliyehudhuria mkutano aliyekuwa amejiandaa kwa ajili ya ujumbe wa ufunguzi wa Rais wa Misheni Howard C. Badger. Alisoma barua kutoka kwa Mzee Spencer W. Kimball (1895–1985), wakati huo akiwa Kaimu Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, ikitangaza kwamba Mzee Romney alikuwa amekuja Johannesburg akiwa na maelekezo ya kuanzisha kigingi cha kwanza.

Mhariri wa Messenger ambaye hakutajwa jina aliandika, “Roho aliongezeka miongoni mwetu sote na tulihisi furaha tele kwa taarifa njema ambayo sote hapa katika Misheni ya Afrika Kusini tumekuwa tukiiwekea juhudi tangu Wamisionari walipokuja kwa mara ya kwanza katika ardhi hii mnamo 1853.”

Louis P. Hefer aliitwa kama rais wa kwanza wa Kigingi kipya cha Transvaal, ambacho kiliundwa eneo la Johannesburg kutoka Wilaya ya Transvaal. Washauri wa Rais Hefer walikuwa Ben de Wet na Olev Taim. Kila mmoja wa viongozi hawa watatu wa ukuhani alikuwa ni muongofu Kanisani wa kati ya miaka 8 na 12, na kila mmoja alikuwa ametumikia katika nyadhifa mbalimbali za uongozi katika kipindi hicho. Wanaume kumi na wawili wengine walioandaliwa na wenye vigezo walichaguliwa kama washauri wakuu.

Matawi matano yaliyokuwa kwenye wilaya ya zamani yalipangiliwa upya kuwa kata na wakati huo huo kigingi kilianzishwa, na marais wa matawi walitawazwa kuwa maaskofu. Kata mpya na maaskofu wapya walikuwa ni pamoja na: Kata ya Krugersdorp (Askofu Daniel Cherrett); Johannesburg 1st Ward, (Askofu George Samuels); Johannesburg 2nd Ward (Askofu Johann Brummer); Kata ya Pretoria, (Askofu Michael Blight); na Kata ya Springs (Askofu Kenneth Armstrong). Kigingi cha Transvaal pia kilijumuisha matawi matano yaliyobakia: Germiston, Vereeniging, East Rand, Klerksdorp na Carletonville.

Wakati wa mkutano wa wamisionari wa mwaka 1970, Rais Badger aliwahakikishia wamisionari wake juu ya ukuaji endelevu ambao ungetokea Kanisani na kuwaasa kumtumikia Mwokozi kwa uwezo wao wote, akili na nguvu, ambavyo wamisionari katika miongo yote iliyofuatia wamefanya pia.

Ni miaka 117 tangu wamisionari wa kwanza kufika Cape Town na habari njema ya injili ya urejesho ya Kristo mpaka kufikia uanzishwaji wa kigingi hiki cha kwanza Afrika. Wakati huo kulikuwa na takriban waumini 6,000 barani kote, wengi wakitoka Afrika Kusini na ijulikanayo leo kama Zimbabwe. Lakini tangu Kigingi cha Transvaal kuanzishwa, Kanisa limeshuhudia ukuaji mkubwa sana. Leo kuna zaidi ya waumini 685,000 katika nchi 34 za Afrika. Wanakutana na kuabudu pamoja katika vigingi 180 na wilaya 98.

Wakati wa mkutano wa wamisionari, Mzee Romney alitoa jumbe ambazo zina manufaa sasa kama zilivyokuwa wakati huo. Aliwaambia wasikilizaji wake kuwa na subira katika mateso, na kujitahidi kumjua Mungu. “Furaha,” alisema, “ni kutafuta njia anayopita Bwana na [kupita] njia hiyo hiyo.”