2021
Ukuu wa Mungu
Februari 2021


SAUTI ZA WAUMINI

Ukuu wa Mungu

“Katika hali mbaya sana, upotevu wa maisha hutokea, na mama na mtoto wangeweza kupotezwa. Japokuwa hili lilinipa hofu, nilijua kwamba Mungu alikuwepo kwenye kila kitu. Nilijua kwamba Bwana angetenda mapenzi Yake kwa mke na mtoto wangu.”

Mnamo tarehe 29 Novemba 2018, mke wangu kipenzi, Ruth, alipata uchungu wa mtoto wetu wa nne. Japokuwa huu ulikuwa wakati wa kufurahisha na wa shangwe kwetu kama familia, kulikuwa na wasiwasi mkubwa. Ujauzito ulikuwa wa wiki 32 na matarajio ya kujifungua yalipaswa kuwa mwisho wa Januari 2019. Hii ilikuwa takriban wiki nane kabla. Wazo—na uhalisia wa ushahidi wa sasa—wa kumpata mtoto wetu mapema ulikuwa wa kuvuruga.

Kabla ya kuharakisha hospitali ya Aga Khan iliyoko Nairobi usiku ule, nilisema sala ya kimya na kumsihi Bwana ili kwamba wote mama na mtoto waweze kulindwa. Tulipowasili hospitali madaktari walinitahadharisha juu ya matokeo yamkini ya hatari ya kujifungua mapema. Walidokeza kwamba maendeleo ya mtoto yangeweza kuathiriwa kutokana na muda kutokamilika tumboni. Katika hali mbaya sana, upotevu wa maisha hutokea, na mama na mtoto wangeweza kupotezwa. Japokuwa hili lilinipa hofu, nilijua kwamba Mungu alikuwepo kwenye kila kitu. Nilijua kwamba Bwana angetenda mapenzi Yake kwa mke na mtoto wangu. Hakikisho hili lilinipa amani tele. Nilikuwa nimeomba mara nyingi kwa ajili ya mambo yenye shinikizo hapo awali, na nilikuwa nimeuona mkono wa Bwana. Yeye alikuwa amejibu maombi yangu tangu siku za ujana wangu. Nilijua Yeye asingetuacha hata katika suala hili licha ya kuonekana gumu.

Katika muda huu wa jaribu, kata yangu, Zimmerman, ilikuwa imegawanywa na nilipokea wito wa kuwa askofu wa moja ya kata mbili mpya zilizoundwa. Huu ulikuwa wakati wenye changamoto kwangu, lakini nilijua kwamba Mungu angetengeneza njia ya kufanikisha jukumu hili kubwa sana. Ningefanya hili na lile kati ya wito wangu mpya, nikiwatunza watoto watatu nyumbani—wote kati yao walikuwa bado wadogo—nikifanya matembezi ya mara kwa mara hospitalini, na kutoa nguvukazi ya uaminifu kwa mwajiri wangu. Kutokana na kujumuika kwangu na maaskofu wengine, ilikuwa dhahiri kwamba wito wa kuwa askofu ulichukuliwa kama moja ya miito yenye changamoto ndani ya kanisa—ukiogopwa na kupendwa kwa kiwango sawa. Hata hivyo, nilijua kwa ujasiri kwamba yeye ambaye Bwana humwita basi Bwana humstahilisha na kwamba Yeye angetoa njia kwa ajili yangu kuwa askofu mwenye mafanikio na vilevile kutimiza majukumu mengine yote yaliyowekwa mabegani mwangu. Kama vile Nefi alivyoeleza: “Na ikawa kuwa mimi, Nefi, nilimwambia baba yangu: Nitaenda na kutenda vitu ambavyo Bwana ameamuru, kwani ninajua kwamba Bwana hatoi amri kwa watoto wa watu, isipokua awatayarishie njia ya kutimiza kitu ambacho amewaamuru” (1 Nefi 3:7).

Mambo yalikwenda vizuri na mtoto wetu David alizaliwa akiwa na uzito wa kg 1.5 (takriban paundi 3.3). Madaktari walisema alionekana vizuri kwa umri wake na kwamba hakuwa kwenye hatari kubwa. Aliwekwa kwenye sadaruki ya watoto wachanga na aliitikia vyema matunzo aliyopewa na madaktari pamoja na manesi. Kama vile kwenye nyakati zingine kabla, niliuona mkono wa Bwana na baraka Zake maalum kwenye maisha ya mke wangu na mwana wangu. Uzoefu huu ulinisaidia kuwa na shukrani kwenye teknolojia kubwa ya tiba na matendo yasiyo ya ubinafsi ya wafanyakazi wa hospitali. David ana afya na anastawi sasa na amekuwa ongezeko kubwa kwenye familia yetu.Yeye ni chanzo cha furaha kwetu sote. Ndugu zake Payson, Precious, na Natasha wanampenda kwa dhati. Yeye ni ukumbusho endelevu wa ukuu wa Mungu.

Joshua M. Njoroge kwa sasa anahudumu kama Mshauri wa 2 katika Kigingi cha Mashariki Nairobi Kenya.