2023
Baraka za Kufanya na Kutunza Maagano ya Hekaluni
Juni 2023


Ujumbe wa Kiongozi wa Eneo

Baraka za Kufanya na Kutunza Maagano ya Hekaluni

Mnamo Septemba 2022, nilipata fursa adhimu ya kuzuru Hekalu la Ghana- Accra nikiwa na wana wangu wawili, wenzi wao na wajukuu watatu. Mmoja wa wana wangu alikuwa akiunganishwa kwa mke wake na watoto watatu. Sote tukiwa tumevalia nyeupe, nilipata taswira katika macho ya akili zangu ya familia ya milele ikiwa sote tungetunza maagano yetu.

Sisi sote ni watoto wa Baba yetu wa Mbinguni na anatupenda sana. Hata hivyo, uhusiano wa kutuunganisha zaidi pamoja Naye ni kupitia kufanya na kutunza maagano. Utiifu kwa maagano yaliyofanywa ndani ya makanisa yetu na nyumba za kuabudu husaidia kutukaribisha kwenye maagano ya juu ya hekaluni. Kwa hivyo kama waumini wa kanisa lengo letu linapaswa kuwa kwenda hekaluni kufanya maagano na Baba wa Mbinguni na kutunza maagano ili tuweze kufurahia uhusiano huo wa kuunganisha.

Malaki katika agano la kale alitoa unabii kuhusu kuja kwa Eliya kabla haijaja ile siku iliyo kuu na ya kuogofya ya Bwana ili kuigeuza mioyo ya akina baba iwaelekee watoto na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, unabii huohuo ulinukuluwa na Malaika Moroni wakati alipomtokea Joseph Smith. (Ona Mafundisho na Maagano 2.) Unabii huu ulitimizwa wakati Eliya alipokuja ndani ya hekalu la Kirtland kurejesha funguo za ukuhani. (Ona Mafundisho na Maagano 110:14–15.) Kupitia funguo hizi mioyo yetu si tu inawageukia mababu zetu bali pia kwenye ahadi Mungu alizofanya kwa Ibrahimu. Waumini wa Kanisa moja kwa moja wanakuwa wanufaika wa ahadi hizo kama aidha watoto halisi wa Ibrahimu kwa kuzaliwa au kuasiliwa. (Ona Ibrahimu 5:10–11.)

Nefi alitufunza vyema kwamba Bwana anatualika sote tuje kwake tupokee wema wake na hamkatazi yeyote, mweusi na mweupe, wafungwa na walio huru, mwanamume na wanamke, wote Wayahudi na Wayunani. (Ona 2 Nefi 26:33.) Kwa wale ambao hawajazuru hekaluni, hebu tujiandae vyema kwa kutunza maagano kwa uaminifu ambayo mpaka sasa tumeyafanya ili kwamba tuwe wenye kustahili kuingia kwenye nyumba ya Bwana.

Kwa wanaume watu wazima kuweni wenye kustahili kutawazwa kwenye Ukuhani wa Melkizedeki ambao bila huo hamuwezi kuingia kwenye nyumba ya Bwana. Pata kibali cha hekaluni kupitia mahojiano na Askofu wako pamoja na Rais wa Kigingi. Jiunge na hudhuria madarasa ya maandalizi ya kwenda hekaluni na andaa nyaraka za kusafiria kama vile pasi ya kusafiria, cheti cha homa ya manjano na cheti cha chanjo ya Uviko-19 ikiwa kitahitajika.

Ninashuhudia kwamba hekalu ni nyumba ya Bwana ambamo tunaweza kuwasiliana Naye ili kutafuta mwongozo wa kiungu kwa ajili ya maisha yetu, kuhisi upendo wake, shangwe na amani. Ni mahala pa kujifunza ambapo uelewa wetu wa mpango wa wokovu unaongezeka. Ni mahala ambapo tunahudumu kama vile mwokozi alivyohudumu juu ya Mlima Sayuni kwa kusimama kwa niaba ya mababu zetu waliofariki na wengine ambao hata hatuwafahamu. Ni mahala pa kuweka msimamo unaojirudia wa kutunza maagano.

Katika mkutano Mkuu wa Oktoba 2022 Rais Russell M. Nelson alituahidi kwamba kufanya maagano kwenye visima vya ubatizo na hekaluni na kuyatunza kunaongeza kufikia kwetu nguvu ya Yesu Kristo.1

Na tuendelee kutunza maagano ya hekaluni na turejee kuabudu hekaluni mara nyingi kadiri fursa zinavyojitokeza.

Muhtasari

  1. Ona Russell M. Nelson, “Ushinde Ulimwengu na Upate Pumziko”, Liahona, Nov. 2022, 96.

Chapisha