2023
Daniel na Thérèse Kola: ‘Tulikuwa na hiyo shangwe mioyoni mwetu’
Juni 2023


Hadithi Kutoka Historia Yetu ya Kiafrika

Daniel na Thérèse Kola: ‘Tulikuwa na hiyo shangwe mioyoni mwetu’

Mnamo 1989 wakati Daniel na Thérèse Kola walipojifunza kuhusu injili iliyorejeshwa, kipato chao kikubwa kilitokana na uuzaji wa kahawa, tumbaku na pombe kwenye mgahawa wao. Baada ya kukubali Neno la Hekima, walijiuliza kama ilikuwa sahihi kuuza vitu walivyohitaji kuviepuka. Walijadili nini cha kufanya mpaka siku ya ubatizo wao ilipofika. Waliamua kuachana na maisha yao ya kale, kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa kale wa Kristo.

“Ilipofika asubuhi, uamuzi ulifanywa,” Daniel Kola anakumbuka. Waliuza duka lao na wakabatizwa, kwa ujasiri walifanya kile Bwana angewataka wao kukifanya. “Tulikuwa na hiyo shangwe mioyoni mwetu kwa sababu tulihisi kitu.”

Kwa miaka saba iliyofuatia, Daniel na Thérèse walitumikia kwa uaminifu wakati Kanisa likikua nchini mwao. Kama ilivyokuwa kwa wengine ambao walikuwa ni uzao wa kwanza wa Watakatifu wa Siku za Mwisho huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, walijifunza hatua kwa hatua. Mnamo 1996 viongozi wa Kanisa wa Kongo walipewa changamoto ya kupiga hatua katika ukuaji wao. Ingawa Kinshasa ilikuwa takribani kilometa 4,000 kutoka hekalu la Johannesburg, Afrika Kusini, ambalo ndilo lilikuwa karibu, kundi la zaidi ya viongozi 20 walialikwa kusafiri kwenda hekaluni kwa pamoja ili kupokea endaumenti kupitia nguvu toka mbinguni na kuunganishwa na wenza wao kwa milele yote. Lilikuwa ni kundi la kwanza la safari ya hekaluni katika historia ya Kongo.

Miaka baada ya safari ya hekaluni ilikuwa ya muhimu kwa Kanisa huko Kongo. Mwishoni mwa miaka ya 1990, kigingi baada ya kingingi vilianzishwa huko Kongo. Wengi wa wanaume walioitwa kama marais wa kigingi, akiwemo Daniel Kola, walikuwa wameshiriki katika safari ile ya hekaluni.

Mnamo 2007 Daniel Kola aliitwa kama Sabini wa Eneo. Mwaka uliofuata alisafiri kwenda Utah kuhudhuria mkutano mkuu na alibarikiwa kushiriki hekaluni mara tano zaidi ili kufanya ibada za awali, endaumenti na kuunganishwa kwa ajili ya mababu zake, ikijumuisha yeye kuunganishwa na wazazi wake. “Wakati nilipopokea endaumenti yangu, kuna mengi sikuyaelewa,” Kola anakumbuka. “Lakini leo, ninaelewa na ufahamu wangu ni mkubwa zaidi.”

Wakati akionyesha shukrani za dhati kwa sababu ya hekalu, Kola pia alikuza hamu kubwa juu ya historia ya familia. Pamoja na wengine wengi, alitambua kwamba aliishi katika wakati muhimu sana, wakati majina na hadithi za mababu wengi zilikuwa bado zinapatikana lakini zikiwa hatarini kupotea kama hazingewekewa kumbukumbu. Mnamo 2018 Shirika lisilo la kibiashara la Daniel Kola liliingia mkataba na FamilySearch ili kusafiri kuzunguka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kurekodi hadithi simulizi, kwa lengo la kukusanya majina 400,000 kwa miezi 12.