“Januari 8–14: ‘Nitaenda na Kutenda.’ 1 Nefi 1–5,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2024)
“Januari 8–14. 1 Nefi 1–5,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2024)
Januari 8–14: “Nitaenda na Kutenda”
1 Nefi 1–5
Kitabu cha Mormoni kinaanza na historia halisi ya familia iliyokuwa ikipitia changamoto halisi. Ilitokea mnamo miaka 600 K.K, lakini kuna mambo kuhusu historia hii ambayo yanaweza kuonekana yanafahamika kwa familia leo. Familia hii ilikuwa ikiishi katika dunia yenye uovu uliokithiri, lakini Bwana aliwaahidi ya kwamba kama wangemfuata, angewaongoza hadi mahali palipo salama. Katika safari walikuwa na nyakati nzuri na nyakati mbaya, baraka kubwa na miujiza, lakini pia walikuwa na mabishano na ugomvi. Ni nadra katika maandiko kupata historia ndefu kama hii kuhusu familia ambayo inajaribu kuishi injili: wazazi wakihangaika kuchochea imani katika familia yao na kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wao, watoto wakiamua ikiwa watawaamini wazazi wao, na vijana wakikabiliana na wivu na ugomvi—na wakati mwingine wakisameheana. Katika yote, kuna nguvu kwenye mifano ya imani katika familia hii isiyo kamilifu.
Mawazo kwa ajili ya kujifunza Nyumbani na Kanisani
Maneno ya Mungu ni “ya thamani kuu” kwangu.
Ujumbe mmoja mashuhuri katika Kitabu cha Mormoni ni “thamani kubwa” ya neno la Mungu (1 Nefi 5:21). Unaposoma 1 Nefi 1–5, tafuta njia ambazo neno la Mungu moja kwa moja au kwa njia tofauti liliibariki familia ya Lehi (kwa mfano, ona 1:11–15; 3:19–20; 5:10–22). Milango hii inakufundisha nini kuhusu neno la Mungu? Ni kitu gani umekipata kinachokushawishi uyachunguze maandiko?
Ona pia “Nisomapo Maandiko,” Nyimbo za Dini, na. 159; “Scriptures Legacy” (video), Gospel Library.
Ninaweza kuimarisha ushuhuda wangu wakati ninapomgeukia Bwana.
Nefi anajulikana kwa imani yake yenye nguvu kwa Bwana, lakini alitakiwa kufanya kazi ili kupata ushuhuda wake—kama vile sote tufanyavyo. Ni kipi unachokisoma katika 1 Nefi 2 ambacho kinaonesha kwa nini Nefi aliweza kupata ushahidi kwamba maneno ya baba yake yalikuwa ya kweli? Ni kwa nini Lamani na Lemueli hawakupata ushahidi huo? (Ona pia 1 Nefi 15:2–11). Ni wakati gani umehisi Bwana akiulainisha moyo wako?
Ona pia “The Lord Commands Lehi’s Family to Leave Jerusalem” (video), Gospel Library.
Mungu ataandaa njia kwa ajili yangu ili niweze kutenda mapenzi Yake.
Wakati Bwana alipowaamuru wana wa Lehi wakachukue mabamba ya shaba, hakutoa maelekezo bayana kuhusu jinsi ya kufanya hivyo. Hii mara nyingi huwa kweli kwenye mwongozo tunaopokea kutoka kwa Mungu, na ingeweza kuhisiwa kwamba Yeye amehitaji “kitu kigumu” (1 Nefi 3:5). Ni kipi kinakushawishi wewe kuhusu jibu la Nefi kwa amri ya Bwana, katika 1 Nefi 3:7, 15–16?
Unaposoma 1 Nefi 3–4, tafuta mambo magumu tofauti tofauti ambayo Nefi alikumbana nayo. Ni kwa namna gani Bwana “aliandaa njia” kwa Nefi “kutimiza vitu [alivyomwamuru]”? Kwa nini ni muhimu kwako kujua kile ambacho Bwana alikifanya kwa ajili ya Nefi?
Njia mojawapo yenye nguvu sana ambayo Mungu ametuandalia ili tutimize amri Zake ni kwa kumtuma Yesu Kristo kuwa Mwokozi wetu. Fikiria kusoma ujumbe wa Rais Dallin H. Oaks “Ni Kitu Gani Mwokozi Wetu Alikifanya kwa ajili Yetu Sisi?” (Liahona, Mei 2021, 75–77). Je, ni kwa namna gani Yesu Kristo ameandaa njia kwa ajili ya kila mmoja wetu? Kwa kujua kwamba Ameshinda vyote kwa ajili yako, unapata msukumo wa “kwenda na kufanya nini”?
Ona pia “Nephi Is Led by the Spirit to Obtain the Plates of Brass” (video), Gospel Library; Mada za Injili, “Utii,” Gospel Library.
Kukumbuka kazi za Mungu kunaweza kunipa imani ya kutii amri Zake.
Wakati Lamani na Lemueli walipohisi kutaka kulaumu au kunung’unika, siku zote walikuwa na Nefi na Lehi karibu kuwatia msukumo na kuwasaidia. Unapohisi kunung’unika, inaweza kusaidia kusoma maneno ya Nefi na Lehi. Ni kwa namna ipi Nefi na Lehi walijaribu kuwasaidia wengine kujenga imani kwa Mungu? (ona 1 Nefi 4:1–3; 5:1–8; ona pia 1 Nefi 7:6–21). Unajifunza nini kinachoweza kukusaidia wakati unapojaribiwa kunung’unika au kulaumu?
“Niliongozwa na Roho.”
Katika 1 Nefi 4:5–18, ni kipi kinachokuvutia kuhusu uwezo wa Nefi wa kutambua na kumfuata Roho? Ungeweza kujifunza ujumbe wa Rais Russell M. Nelson “Ufunuo kwa Ajili ya Kanisa, Ufunuo kwa Ajili ya Maisha Yetu” (Liahona, Mei 2018, 93–96) ili kujifunza zaidi kuhusu kupokea ufunuo kutoka kwa Bwana.
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Ninaweza kuwa na ushuhuda wangu binafsi.
-
Ni kwa namna gani Nefi aliweza kujua kwamba kile kilichofundishwa na baba yake kilikuwa cha kweli? Wasaidie watoto wako wapate majibu ya swali hili katika 1 Nefi 2:16, 19. Wangeweza pia kufurahia kuandika matendo ya Nefi kwenye matofali au vitu vingine na kisha kujenga kitu kwa kutumia vitu hivyo. Hii ingeweza kuwapeleka kwenye mazungumzo kuhusu jinsi ambavyo matendo haya hutusaidia kujenga ushuhuda.
-
Ungeweza kuwaonesha watoto wako picha au maumbo ambayo yanawakilisha vitu ambavyo wangeweza kutafutia ushuhuda juu yake, vitu kama vile nakala ya Kitabu cha Moromoni au picha ya Yesu Kristo, hekalu au nabii aliye hai. Waalike wachague kimoja na washiriki shuhuda zao juu ya kitu hicho. Ungeweza pia kuwaambia watoto wako jinsi wewe ulivyoweza kupata ushuhuda wako. Je, ni kwa nini tunahitaji ushuhuda wetu wenyewe?
Mungu atanisaidia nishike amri Zake.
-
Fikiria kutumia nyenzo moja au zaidi ya hizi ili kuwasaidia watoto wako wazungumze kuhusu jinsi Mungu alivyomsaidia Nefi kupata mabamba ya shaba: 1 Nefi 3–4; ukurasa wa shughuli ya wiki hii; “Nephi’s Courage” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 120–21); na “Mlango wa 4: Mabamba ya Shaba” (katika Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 8–12).
-
Wewe pamoja na watoto wako mngeweza kufurahia kuigiza 1 Nefi 3:2–7. Pengine ungeweza kujifanya wewe ni Lehi na kuwataka watoto wako warudi Yerusalemu kuchukua mabamba ya shaba. Waalike kuitikia katika maneno yao wenyewe kama vile ambavyo wao wangekuwa Lamani na Lemueli au Nefi. Ni baadhi ya mambo yapi Mungu ametuamuru sisi tufanye? (ona picha 103–15 katika Kitabu cha Sanaa za Injili au Mosia 18:8–10 kwa ajili ya mawazo). Ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa kama Nefi?
Maandiko ni hazina kuu.
-
Maandiko yalikuwa ya muhimu kwa familia ya Lehi. Ili kuonesha mfano, ungeweza kuwaalika watoto wako wasaidie kukwambia au kuigiza kile Nefi na kaka zake walichokifaya ili kupata bamba za shaba: Walisafiri umbali mrefu, walitoa vitu vyao vya dhahabu na vya fedha na walijificha kwenye pango la mwamba ili kuhifadhi maisha yao. Kisha ungeweza kusoma 1 Nefi 5:21 na kuzungumza kuhusu kwa nini maandiko yalikuwa ya thamani sana kwa familia ya Lehi. Kwa nini ni ya thamani kwetu sisi? Ni kwa jinsi gani tunaweza kuchukulia maandiko kama hazina?
Roho Mtakatifu ataniongoza wakati nitafutapo kutenda mapenzi ya Bwana.
-
Baada ya kupitia pamoja 1 Nefi 3 jinsi Nefi na kaka zake walivyojaribu kupata mabamba ya shaba, soma pamoja na watoto wako 1 Nefi 4:6 ili kupata kile ambacho Nefi alikifanya ambacho kilimruhusu hatimaye kufanikiwa. Kisha watoto wako wangeweza kutengeneza orodha ya kile ambacho Mungu anawataka wakifanye. Je, Roho Mtakatifu anatusaidiaje katika hali kama hizi?