“Agosti 12- 18: ‘Simama Imara Katika Imani ya Kristo.’ Alma 43–52,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2023)
“Agosti 12–18. Alma 43–52,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2023)
Agosti 12–18: “Simama Imara Katika Imani ya Kristo”
Alma 43–52
Wakati tunaposoma maneno haya mwanzoni mwa Alma mlango wa 43—“Na sasa narejea historia ya vita kati ya Wanefi na Walamani”—ni kawaida kujiuliza kwa nini Mormoni alijumuisha historia hizi za vita wakati alikuwa amebakiza nafasi ndogo kwenye mabamba (ona Maneno ya Mormoni 1:5). Ni kweli kwamba tuna fungu letu la vita katika siku za mwisho, lakini kuna umuhimu katika maneno yake zaidi ya maelezo ya mkakati na huzuni ya vita. Maneno yake pia yanatuandaa kwa ajili ya vita ambayo “sote ni askari” (Nyimbo za Dini, na. 143), vita tunavyopigana kila siku dhidi ya nguvu za uovu. Vita hivi ni halisi, na matokeo yanaathiri maisha yetu ya milele. Kama vile Wanefi, sisi “tukitiwa moyo na nia takatifu—“Mungu wetu, dini yetu, na uhuru wetu na amani yetu, wake zetu, na watoto wetu—kitu ambacho Moroni alikiita “nia ya Wakristo” (Alma 46:12, 16).
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Yesu Kristo anaweza kunisaidia kwenye vita vyangu vya kiroho.
Unaposoma Alma 43–52, gundua kitu ambacho Wanefi walikifanya ambacho kiliwafanya wawe na mafanikio (au wakose mafanikio). Kisha tafakari jinsi unavyoweza kutumia kile unachojifunza ili kikusaidie ushinde vita vyako vya kiroho. Andika mawazo yako hapa chini:
-
Alma 43:19: Wanefi walijiandaa kwa silaha. (Ninaweza kujitahidi kujiandaa kwa silaha za kiroho.)
-
Alma 43:23–24: Walitafuta mwongozo wa nabii.
Pia, ona kile unachoweza kujifunza kutokana na juhudi za maadui wa Wanefi. Tafakari jinsi Shetani anavyoweza kukushambulia katika njia sawa na hizo:
-
Alma 43:8: Zerahemna alitaka kuwakasirisha watu wake ili aweze kuwa na nguvu juu yao. (Shetani anaweza kunijaribu nitende kwa hasira.)
Ona pia Russell M. Nelson, “Kumbatia Siku za Usoni kwa Imani,” Liahona, Nov. 2020, 73–76; “Mlinzi ni Mungu Wetu,” Nyimbo za Dini, na. 28.
“Simama imara katika imani ya Kristo.”
Je, unataka kupunguza nguvu za adui katika maisha yako? Njia moja ni kufuata ushauri katika Alma 48:17 wa kuwa “kama Moroni.” Fikiria kutengeneza orodha ya maneno ambayo yanamuelezea Moroni unaposoma Alma 46:11–28; 48:7–17. Unajifunza kipi kutoka kwa Moroni kuhusu kusimama imara katika imani ya Kristo? (Alma 46:27).
Ungeweza pia kujifunza jinsi Moroni alivyowavutia wengine katika “nia ya Wakristo” (ona Alma 46:11–22). Ni kwa jinsi gani ungeeleza nia hiyo? Ni kipi unaweza kufanya ili kushiriki katika nia hiyo? Ni kwa jinsi gani wewe unaweza kuwavutia wengine kushiriki pia?
Kitu kimoja Moroni alichofanya ili kuwavutia wengine kilikuwa ni kutengeneza bendera ya uhuru, ambayo ilisisitiza kanuni za kuwavutia Wanefi (ona mstari wa 12). Ni kanuni zipi viongozi wetu wa Kanisa wanasisitiza katika siku zetu? Unaweza kuzitafuta katika Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi (kijitabu, 2022), “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” dhima ya Wasichana na Akidi ya Ukuhani wa Haruni, au jumbe za hivi karibuni za mkutano mkuu. Ungeweza kufanya muhtasari wa kile jumbe hizo zinachofundisha kuwa baadhi ya kauli rahisi za kutengeneza bendera yako mwenyewe ya uhuru—kitu fulani cha kukukumbusha wewe kuwa mkweli kwa Mwokozi na injil Yake.
Ona pia Mada za Injili, “Imani katika Yesu Kristo,” Maktaba ya Injili.
Shetani hutujaribu na hutudanganya kidogo kidogo.
Shetani anajua kwamba hauna uwezekano wa kutenda dhambi kubwa au kuamini uongo ulio wazi. Kwa hiyo, anatumia uongo wenye werevu na majaribu madogo madogo—mengi kadiri anavyodhani utaweza kukubali—kukuongoza mbali na usalama wa kuishi kwa haki.
Tafuta mpangilio huu katika Alma 47, na utafakari jinsi Shetani anavyoweza kuwa anajaribu kukudanganya. Zingatia umaizi huu kutoka kwa Mzee Robert D. Hales:
“Msaliti Amalikia alimhimiza Lehonti ‘ashuke chini’ ili akutane naye katika bonde. Lakini wakati Lehonti alipotoka kwenye uwanda wa juu, alipewa sumu ‘kidogo kidogo’ mpaka akafa, na jeshi lake likaangukia mikononi mwa Amalikia (ona Alma 47). Kwa mabishano na mashitaka, baadhi ya watu wanatutega ili tutoke kwenye sehemu ya juu. Sehemu ya juu ndiko nuru iliko. … Ni mahali pa usalama” (“Ujasiri wa Kikristo: Gharama ya Ufuasi,” Liahona, Nov. 2008, 74).
Unajifunza kipi kutoka katika video ya “Temptation Fades as We Seek Christ in Every Thought” (Maktaba ya Injili) ambacho kinaweza kutusaidia tushinde majaribu?
Ona pia Nehemia 6:3; 2 Nefi 26:22; 28:21–22.
Umoja huleta usalama.
Licha ya silaha na ngome za Wanefi, Walamani waliteka mingi ya miji yao (ona Alma 51:26–27). Ni kwa jinsi gani hili lilitokea? Tafuta majibu unaposoma sura hizi (ona hasa Alma 51:1–12). Tafakari ni maonyo gani tukio hili linaweza kuwa nayo kwa ajili yako na kwa familia yako.
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Alma 43:17–21; 48:7–8; 49:1–5; 50:1–6
Ninaweza kupata ulinzi wa kiroho katika injili ya Yesu Kristo.
-
Fikiria kutumia “Mlango wa 31: Kapteni Moroni Anamshinda Zerahemna” (Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 85–88) kuwaambia watoto wako kuhusu vita kati ya Wanefi na Walamani. Unaposoma kuhusu silaha za Wanefi katika Alma 43:19, ungeweza kulinganisha silaha ambayo hulinda miili yetu na vitu ambavyo Mungu ametupatia kulinda roho zetu. Pengine wewe na watoto wako mngeweza kuchora picha ya mtoto na kuongeza kipande cha silaha kwenye picha kwa ajili ya kila kitu ambacho watoto wako wanaweza kutaja ambacho hutulinda kiroho.
-
Mistari hii inaelezea ngome ambayo Wanefi waliijenga: Alma 48:7–9; 49:1–9; 27:27–6. Baada ya kusoma mistari hii pamoja, watoto wako wangeweza kufurahia kujenga ngome kutokana na vitu kama viti na mablanketi. Video “Elder Stevenson on Fortifying Families” (Maktaba ya Injili) inaweza kukusaidia kujadili jinsi ya kujenga ngome ya kiroho nyumbani kwako.
Alma 46:11–16; 48:11–13, 16–17
Ninaweza kuwa “imara katika imani ya Kristo” kama Kapteni Moroni.
-
Watoto wako wangeweza kuangalia picha katika muhtasari ili kusimulia hadithi ya bendera ya uhuru (ona Alma 46:11–16; “Mlango wa 32: Kapteni Moroni na Bendera ya Uhuru” Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 89–90). Ni kipi Moroni alitaka watu wake wakumbuke? (ona mstari wa 12)? Ni kipi Baba wa Mbinguni anatutaka sisi tukumbuke? Pengine watoto wako wangebuni “bendera zao za uhuru” kwa virai au picha ambazo zitawasaidia wao wakumbuke mambo haya.
-
Ili kuwafundisha watoto wako kuhusu kuwa “imara katika imani ya Kristo” kama vile Moroni (ona Alma 48:13), ungeweza kuwasaidia watafute na waguse kitu kilicho thabiti. Je, inamaanisha nini kwa imani kuwa “imara”? Someni pamoja Alma 48:11–12 ili kutafuta kile kilichomfanya Moroni awe imara katika imani yake kwa Kristo. Mngeweza pia kuimba “I Will Be Valiant” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto,162). Je, tunaweza kufanya nini ili kuwa “imara katika imani juu ya Kristo”?
Shetani hutujaribu na kutudanganya kidogo kidogo.
Someni pamoja mistari iliyochaguliwa kutoka Alma 47:4–19. Nini kingetokea kama Amalikia angemwambia Lehonti kile alichopanga kufanya tangu mwanzo? Mistari hii inafundisha nini kuhusu jinsi Shetani anavyojaribu kutudanganya?