Scripture Stories
Bendera ya Uhuru


“Bendera ya Uhuru,” Hadithi za Kitabu cha Mormoni (2023)

Alma 46–50

Bendera ya Uhuru

Kutetea haki ya kuamini katika Mungu

Picha
Amalikia ananyosha mikono mbele ya watu wake na wanashangilia

Amalikia alikuwa Mnefi mkubwa, mwenye nguvu. Alitaka kuwa mfalme. Aliahidi kuwapa nguvu watu waliomsaidia. Watu wengi walimpenda na walijaribu kuwafanya wengine wamfuate. Amalikia aliwaongoza watu kutenda mambo mabaya. Yeye na wafuasi wale walitaka kuwaua watu ambao walifundisha kuhusu Yesu Kristo.

Alma 45:23–24; 46:1–10

Picha
Kapteni Moroni anaondoka mbali na Amalikia na watu wake

Kapteni Moroni, kiongozi wa majeshi ya Wanefi, aliamini katika Yesu. Alijua Wanefi walikuwa wamebarikiwa kwa sababu walitii amri za Mungu. Alikuwa amekasirishwa sana na Amalikia kwa kuwa anawaongoza watu mbali na Mungu, akijaribu kuwa mfalme, na akijaribu kuwaumiza watu.

Alma 46:9–11, 13–15, 18

Picha
Kapteni Moroni ananyanyua juu bendera ya uhuru

Moroni alichana koti lake. Aliandika juu yake kwamba watu wanapaswa kumkumbuka Mungu wao, uhuru wao, na familia zao. Kisha akafunga kwenye mlingoti na kuiita bendera ya uhuru. Moroni alisali kwa ajili ya baraka za Mungu. Aliwaonyesha Wanefi bendera ya uhuru na kuwaomba kujiunga naye katika kupigana na Amalikia.

Alma 46:12–20, 23–24, 28

Picha
Kapteni Moroni anasimama mbele ya jeshi na familia zao

Watu wanavalia silaha zao na kumkimbilia Moroni. Walikuwa tayari kupigana kwa ajili ya Mungu na nyumba zao, familia zao na uhuru wao. Walifanya agano, au ahadi maalumu na Mungu kwamba wangemfuata Yeye daima. Kisha wakajiweka tayari kupigana na Amalikia.

Alma 46:21–22, 28

Picha
Amalikia na baadhi ya askari wake wanakimbilia

Jeshi la Moroni lilikuwa kubwa. Amalikia alikuwa anaogopa. Alijaribu kukimbilia mbali pamoja na wafuasi wake. Lakini wengi wao walikuwa na wasiwasi kwamba Amalikia alikuwa anapigana kwa sababu zisizo sahihi. Wengi hawangeweza kumfuata yeye tena. Jeshi la Moroni liliwazuia wale ambao bado walimfuata Amalikia, lakini Amalikia na baadhi ya wachache walitoroka.

Alma 46:29–33

Picha
Amalikia anazungumza na Walamani

Amalikia alienda kwenye nchi ya Walamani. Aliwataka Walamani wamsaidie yeye kupigana dhidi ya Wanefi. Ndipo angekuwa na jeshi kubwa, lenye nguvu zaidi. Aliwafanya Walamani wengi kuwakasirikia Wanefi. Mfalme wa Walamani aliwaambia Walamani wote wajiandae kupigana na Wanefi.

Alma 47:1

Picha
Amalikia anapiga magoti mbele ya mfalme Mlamani kwa ajili ya taji

Mfalme alimpenda Amalikia. Alimfanya Amalikia kuwa mmoja wa viongozi wa jeshi la Walamani. Lakini Amalikia alitaka uwezo zaidi.

Alma 47:1–3

Picha
Amalikia anavalia taji

Amalikia alifanya mpango wa kuwatawala Walamani. Alilitwaa jeshi lote la Walamani. Kisha aliwafanya watumishi wake wamuue mfalme na kudanganya kuhusu yule aliyefanya hivyo.

Alma 47:4–26

Picha
Amalikia anakunja ngumi mbele ya askari Walamani hali wanashanglia

Amalikia alijifanya amekasirika kwa mfalme kuuawa. Walamani walimpenda Amalikia. Alimuoa malkia na kuwa mfalme mpya. Alitaka pia kuwatawala Wanefi. Alizungumza vibaya kuwahusu Wanefi ili kwamba Walamani waweze kuwakasirikia. Punde, Walamani wengi walitaka kupigana na Wanefi.

Alma 47:25–35; 48:1–4

Picha
Kapteni Moroni na askari wake wakijenga kuta

Wakati Amalikia akipata nguvu kwa kudanganya, Moroni aliwaandaa Wanefi kumtumainia Mungu. Moroni aliweka bendera ya uhuru katika kila mnara katika nchi ili kuwakumbusha watu ahadi yao. Majeshi ya Moroni pia yaliiandaa miji ya Wanefi kwa ajili ya vita. Walijenga kuta na kuchimba mitaro ili kuifanya miji kuwa salama na imara.

Alma 46:36; 48:7–18

Picha
Askari wa Amalikia wanatupa mishale kwenye mji wa Wanefi

Wakati Walamani walipokuja kupigana, hawangeweza kuingia ndani ya miji ya Wanefi. Walizuiwa na kuta na mitaro ambayo majeshi ya Moroni yalijenga. Walamani wengi walikufa wakati walipowashambulia Wanefi. Amalikia alikasirika sana. Aliahidi kumuua Moroni.

Alma 49:1–27

Picha
Kapteni Moroni anazungumza na Wanefi baada ya mapigano

Wanefi walimshukuru Mungu kwa kuwasaidia na kuwalinda. Waliifanya miji yao kuwa salama zaidi na kujenga miji mingine zaidi. Vita na Walamani viliendelea, lakini Mungu alimsaidia Moroni na majeshi yake kuendelea kuwafanya Wanefi kuwa salama. Wanefi walikuwa na furaha. Walimtii Mungu na kubakia waaminifu Kwake.

Alma 49:28–30; 50:1–24

Chapisha