“Nabii Etheri,” Hadithi za Kitabu cha Mormoni (2023)
Nabii Etheri
Onyo la Bwana kwa taifa
Bwana alimleta kaka wa Yaredi na familia yake kwenye nchi ya ahadi. Walikuwa wanyenyekevu na walitii amri za Mungu. Kundi lao lilikua kwa miaka mingi na walitaka mfalme wa kuwaongoza. Kaka ya Yaredi aliwaonya kwamba kuwa na mfalme kungewaletea matatizo, lakini yeye aliwaacha wamchague mfalme.
Kwa mamia ya miaka, Wayaredi waliishi katika nchi ya ahadi. Wakati mwingine wafalme wao waliwaongoza kufanya mema, lakini nyakati zingine hawakufanya hivyo. Manabii wa Mungu wangewaonya watu ili watubu. Watu waliposikiliza na kutii amri za Mungu, Yeye aliwabariki. Nabii wa mwisho wa Wayaredi aliitwa Etheri.
Etheri 7:23–27; 9:26–30; 10:16–17, 28; 11:1–8, 12–13, 20–22; 12:2
Watu walikuwa hawamtii Mungu. Lakini Roho wa Bwana alikuwa na Etheri. Aliwafundisha kutoka asubuhi hadi usiku. Aliwaambia waamini katika Mungu na watubu au wangeangamizwa. Kama wangekuwa na imani, wangekuwa na tumaini la kuishi na Mungu tena na kupata nguvu za kufanya mambo mazuri. Watu hawakuamini.
Etheri alitazama kile watu walichofanya. Etheri alijificha pangoni mchana na kuandika kile alichokiona. Watu hawakutubu na walianza kupigana wao kwa wao.
Etheri aliona kwamba mfalme Myaredi, Koriantumuri, ilimbidi kupigana na watu wengi ambao walikuwa wanataka kuwa mfalme. Koriantumuri alitumia jeshi lake kujilinda.
Siku moja, Bwana alimwambia Etheri kumuonya Koriantumuri na watu wake ili watubu. Kama wangefanya hiivyo, Bwana angewasaidia watu na angemruhusu Koriantumuri kuendelea kuwa na ufalme wake. Kama sivyo, watu wangeangamizana wao kwa wao. Koriantumuri angeishi muda mrefu vya kutosha kuona maneno ya Bwana yakitimia. Kisha na yeye angekufa pia.
Koriantumuri na watu wake hawakutubu. Watu walijaribu kumuua Etheri, lakini Etheri alitoroka hadi kwenye pango lake. Mtu mmoja aliyeitwa Shizi alipigana dhidi ya Koriantumuri. Watu walichagua kujiunga na jeshi la Shizi au jeshi la Koriantumuri. Majeshi haya mawili yalikuwa na vita vingi. Watu wengi walikufa.
Etheri 13:22–25; 14:17–20; 15:2
Koriantumuri alikumbuka kile Etheri alichokuwa amesema. Alikuwa na huzuni kwamba watu wengi sana walikuwa wamekufa. Alikumbuka kwamba manabii wote walionya hili lingetokea. Alianza kutubu na kutuma barua kwa Shizi. Alisema angeachia ufalme kama watu wake wangeokolewa. Lakini Shizi alitaka kupigana.
Watu wa Koriantumuri walikuwa wamekasirika na walitaka kupigana. Watu wa Shizi walikuwa wamekasirika pia na walitaka kupigana. Hakuna aliyetaka kutubu. Etheri aliona kwamba kila mtu alienda vitani. Watu wengi zaidi walikufa.
Koriantumuri alitaka kusitisha vita. Alimuomba Shizi achukue ufalme na asiwaumize watu wake. Kila mtu alikuwa amekasirika. Hawakuwa na Roho wa Bwana. Etheri aliona kwamba kila mtu aliendelea kupigana mpaka pale Koriantumuri alipokuwa Myaredi mwingine pekee aliyekuwa hai. Kisha Koriantumuri alizimia.
Etheri aliona kwamba kila kitu Bwana alichosema kilikuja kuwa kweli. Etheri alikamilisha kuandika kile kilichokuwa kimetokea. Kisha alihakikisha watu wangeweza kupata maandishi yake baada ya yeye kuwa amekufa. Etheri alimtumainia Mungu na kutazamia kuwa pamoja Naye siku moja.