Maandiko Matakatifu
Etheri 11


Mlango wa 11

Vita, mafarakano, na uovu unatawala maisha ya Wayaredi—Manabii watabiri kuangamizwa kabisa kwa Wayaredi wasipotubu—Watu wanakataa maneno ya manabii.

1 Na kulitokea pia katika siku za Komu manabii wengi, na walitoa unabii wa uharibifu wa wale watu wakuu isipokuwa watubu, na kumgeukia Bwana, na kuacha mauaji yao na uovu.

2 Na ikawa kwamba manabii walikataliwa na watu, na walimkimbilia Komu kwa ulinzi, kwani watu walitaka kuwaangamiza.

3 Na walitoa unabii wa vitu vingi kwa Komu; na alibarikiwa kwa siku zake zote zilizosalia.

4 Na aliishi kwa umri mzuri wa uzee, na alimzaa Shiblomu; na Shiblomu akatawala badala yake. Na kaka wa Shiblomu aliasi dhidi yake, na kukaanza kuwa na vita vikubwa katika nchi yote.

5 Na ikawa kwamba kaka wa Shiblomu alisababisha kwamba manabii wote waliotoa unabii wa uharibifu wa watu wauawe;

6 Na kulikuwa na msiba mkubwa katika nchi yote, kwani walikuwa wameshuhudia kwamba laana kubwa ingekuja kwenye nchi, na pia juu ya watu, na kwamba kungekuwa na uharibifu mkuu miongoni mwao, mkubwa kuliko yote iliyowahi kuwa usoni mwa dunia, na mifupa yao ingekuwa kama mafungu ya mchanga usoni mwa nchi isipokuwa watubu uovu wao.

7 Na hawakusikiliza sauti ya Bwana, kwa sababu ya makundi yao maovu; kwa hivyo, kulianza kuwa na vita na mabishano katika nchi yote, na pia njaa nyingi na maradhi ya kuambukiza, mpaka kwamba kukawa na uharibifu mkuu, ambao haujawahi kujulikana usoni mwa dunia; na haya yote yalikuja kutimia katika siku za Shiblomu.

8 Na watu walianza kutubu uovu wao; na kadiri walivyofanya hivyo, Bwana alikuwa na huruma kwao.

9 Na ikawa kwamba Shiblomu aliuawa, na Sethi akaletwa kwenye utumwa, na aliishi kwenye utumwa siku zake zote.

10 Na ikawa kwamba Aha, mwana wake, alichukua ufalme; na akawatawala watu siku zake zote. Na alifanya aina yote ya uovu katika siku zake, ambamo kwake alisababisha umwagaji wa damu nyingi; na siku zake zilikuwa chache.

11 Na Ethemu, akiwa wa ukoo wa Aha, alichukua ufalme; na pia alifanya yale yaliyokuwa maovu katika siku zake.

12 Na ikawa kwamba katika siku za Ethemu kulitokea manabii wengi, na wakatoa unabii tena kwa watu; ndiyo, walitabiri kwamba Bwana angewaharibu kabisa kutoka kwa uso wa dunia isipokuwa watubu uovu wao.

13 Na ikawa kwamba watu walishupaza mioyo yao, na hawangesikiliza maneno yao; na manabii waliomboleza na kujitoa miongoni mwa watu.

14 Na ikawa kwamba Ethemu alitoa hukumu katika uovu siku zake zote; na alimzaa Moroni. Na ikawa kwamba Moroni alitawala badala yake; na Moroni alifanya yale ambayo yalikuwa maovu mbele ya Bwana.

15 Na ikawa kwamba kulitokea uasi miongoni mwa watu, kwa sababu ya lile kundi ovu la siri ambalo lilianzishwa kupata uwezo na faida; na kulitokea mtu mkubwa wa uovu miongoni mwao, na akapigana na Moroni, ambamo kwake alipindua nusu ya ufalme; na akashika nusu ya ule ufalme kwa miaka mingi.

16 Na ikawa kwamba Moroni alimpindua, na kupata ufalme tena.

17 Na ikawa kwamba kulitokea mtu mwingine mwenye nguvu; na alikuwa uzao wa kaka wa Yaredi.

18 Na ikawa kwamba alimwondoa Moroni na kuchukua ufalme; kwa hivyo, Moroni aliishi katika utumwa siku zake zote zilizosalia; na alimzaa Koriantori.

19 Na ikawa kwamba Koriantori aliishi katika utumwa siku zake zote.

20 Na katika siku za Koriantori kulitokea manabii wengi, na wakaagua vitu vikubwa na vya ajabu, na kuhubiri toba kwa watu, na isipokuwa watubu Bwana Mungu angetoa hukumu dhidi yao hadi watakapoharibiwa kabisa.

21 Na kwamba Bwana Mungu angewatuma au kuwaleta mbele watu wengine kumiliki nchi, kwa uwezo wake, kwa njia sawa ambayo aliwaleta babu zao.

22 Na walikataa maneno yote ya manabii, kwa sababu ya kundi lao la siri na machukizo yao maovu.

23 Na ikawa kwamba Koriantori alimzaa Etheri, na akafariki, akiwa ameishi katika utumwa siku zake zote.