“Alma kwenye Maji ya Mormoni,” Hadithi za Kitabu cha Mormoni (2023)
Alma kwenye Maji ya Mormoni
Kuwa watu wa Mungu
Alma alikuwa kuhani wa mfalme aliyeitwa Nuhu. Alma alijaribu kumwokoa Abinadi, nabii wa Mungu, kutokana na kuuawa na Nuhu. Lakini Nuhu alimkasirikia Alma na alitaka kumuua Alma pia. Alma alimkimbia Nuhu ili kuwa salama. Wakati wa mchana, Alma alijificha karibu na mahali palipoitwa Maji ya Mormoni.
Alma aliamini kile ambacho Abinadi alifundisha kuhusu Yesu Kristo. Alimwomba Mungu amsamehe dhambi na makosa yake.
Alma alikutana na watu kwenye faragha na kuwafundisha kuhusu Yesu. Alimfundisha kila mtu ambaye angemsikiliza.
Watu wengi walimwamini Alma. Walienda kwenye Maji ya Mormoni kumsikiliza Alma akifundisha.
Waaminio walitaka kuitwa watu wa Mungu, kuwasaidia wengine wenye uhitaji, na kuwaambia watu kuhusu Mungu. Kwa hiyo Alma aliwaalika wabatizwe. Kwa kubatizwa, wangefanya agano, au ahadi, na Mungu ya kumtumikia Yeye na kushika amri Zake. Matokeo yake, Mungu angewabariki wao na Roho Wake.
Watu walikuwa na furaha sana. Walipiga makofi na kusema kwamba walitaka kubatizwa. Alma alimbatiza kila mmoja wao katika Maji ya Mormoni. Wote walijawa na Roho wa Mungu na kuhisi upendo wa Mungu kwa ajili yao. Wakawa waumini wa Kanisa la Kristo.
Nuhu aliona kwamba baadhi ya watu wake walikuwa wanaondoka kutoka kwenye nchi yake. Aliwatuma watumishi kwenda kuwatazama. Watumishi waliona watu walienda kwenye nchi ya Mormoni ili kusikiliza mafundisho ya Alma. Nuhu alikasirika sana. Alituma jeshi lake ili kumuua Alma na watu wa Alma aliokuwa anawafundisha.
Mungu alimwonya Alma kuhusu jeshi lile. Kwa msaada wa Mungu, Alma na watu wake kwa usalama waliondoka nchi ile. Jeshi halikuweza kuwakamata. Walitembea kwa siku nane nyikani na kufika kwenye nchi nzuri sana. Wakafanya makazi mapya humo. Alma aliwafundisha watu, na wao walishika ahadi yao kwa Mungu.