“Kuhusu Kitabu cha Mormoni,” Hadithi za Kitabu cha Mormoni (2023)
Kuhusu Kitabu cha Mormoni
Yesu Kristo na watu Wake Katika Mabara ya Amerika
Kitabu cha Mormoni ni maandiko.matakatifu. Kinatufundisha kuhusu Bwana Yesu Kristo na ziara Yake katika Mabara ya Amerika miaka mingi iliyopita. Kutoka katika Kitabu cha Mormoni, tunaweza kujifunza kuhusu injili ya Yesu. Kinatufundisha jinsi ya kuwa na amani sasa na jinsi tunavyoweza kuishi pamoja na Mungu na Yesu tena siku moja.
Ukurasa wa jina la Kitabu cha Mormoni; utangulizi wa Kitabu cha Mormoni; 3 Nefi 11
Kitabu cha Mormoni kiliandikwa na manabii wa Mungu. Waliandika kwenye kurasa za mabati yaliyoitwa mabamba. Hadithi na shuhuda zao zinatusaidia kuwa na imani katika Yesu. Waliandika kuhusu makundi mengi ya watu walioishi katika Mabara ya Amerika miaka mingi iliyopita.
Ukurasa wa jina la Kitabu cha Mormoni; utangulizi wa Kitabu cha Mormoni
Kundi moja lilikuja kutoka Yerusalemu kwenda Mabara ya Amerika takribani miaka 600 kabla Yesu hajazaliwa. Wakawa mataifa mawili yalioitwa Walamani na Wanefi.
Utangulizi wa Kitabu cha Mormoni; 1 Nefi 1:4
Mapema zaidi, kundi lingine lilitoka kutoka kwenye Mnara wa Babeli kwenda kwenye haya Mabara ya Amerika Hawa waliitwa Wayaredi.
Utangulizi wa Kitabu cha Mormoni; Etheri 1:33–43
Manabii wa Mungu waliwafundisha watu. Watu waliposikiliza na kutii amri za Mungu, Yeye aliwasaidia. Manabii walifundisha kuhusu Yesu na walisema kwamba atazaliwa Yerusalemu. Wanefi na Walamani walijifunza kwamba Yesu angewatembelea baada ya kifo Chake.
2 Nefi 1:20; 25:12–14; 26:1, 3, 9; Mosia 3:5–11; Alma 7:9–13; Helamani 32
Yesu alikuja kama vile manabii walivyosema. Baada ya Yesu kufa na kufufuka, Aliwatembelea watu. Aliacha kila mtu aguse alama za misumari katika mikono na miguu Yake. Walijua Yesu alikuwa Mwana wa Mungu. Alifundisha injili Yake, na watu waliiandika. Walizungumza kuhusu ziara ya Yesu kwa miaka mingi.
3 Nefi 11:7–15, 31–41; 16:4; 4 Nefi 1:1-6, 13–22
Mormoni alikuwa nabii aliyeishi takribani miaka mia moja baada ya ziara ya Yesu. Wakati wa maisha ya Mormoni, watu waliacha kumfuata Bwana. Mormoni alikuwa na maandiko ya manabii walioishi kabla yake. Aliweka mengi ya maandiko yao katika seti moja ya mabamba. Mabamba haya yakawa Kitabu cha Mormoni.
Utangulizi wa Kitabu cha Mormoni; Maneno ya Mormoni 1:2–9; Mormoni 1:2–4, 13–17
Kabla ya Mormoni kufa, alimkabidhi mabamba hayo mwanawe Moroni. Wakati wa maisha ya Moroni, watu walikuwa wanafanya mambo mabaya sana. Walitaka kumuua mtu ye yote ambaye aliamini katika Yesu. Moroni alitaka kuwasaidia watu katika siku za baadaye, kwa hiyo aliandika zaidi kwenye mabamba na kuyazika ili yawe salama.
Utangulizi wa Kitabu cha Mormoni; Maneno ya Mormoni 1:1–2; Mormoni 8:1–4, 14–16; Moroni 1
Miaka mingi baadaye, katika mwaka 1823, Moroni alikuja kama malaika kwa Nabii Joseph Smith. Moroni alimwambia Joseph wapi pa kuyapata yale mabamba. Kwa msaada wa Mungu, Joseph alitafsiri kile kilichoandikwa kwenye hayo mabamba.
Utangulizi wa Kitabu cha Mormoni; Joseph Smith—Historia ya 1
Mungu humtuma Roho Mtakatifu.kukusaidia wewe ujue wakati kitu fulani ni cha kweli. Unaposoma Kitabu cha Mormoni, unaweza kusali na kumwuliza Mungu kama ni cha kweli. Katika njia hiyo hiyo, unaweza kujua kwamba Yesu ni Mwokozi wako na kwamba Yeye anakupenda.