“Alma na Korihori,” Hadithi za Kitabu cha Mormoni (2023)
Alma na Korihori
Imani kwamba Mungu kweli yupo
Mtu mmoja aliyeitwa Korihori alikuja kwenye nchi ya Zarahemla. Aliwaambia watu kwamba Mungu na Yesu Kristo hawapo.
Korihori aliwaambia watu wangeweza tu kujua kitu kama wangekiona. Aliwadhihaki watu ambao waliamini katika Yesu.
Korihori aliwaambia watu hawakuhitaji amri za Mungu. Alisema watu wangeweza kufanya cho chote walichotaka. Watu wengi walimwamini yeye. Waliamua kufanya mambo mabaya.
Korihori alijaribu kuwafundisha Waanti-Nefi-Lehi, lakini hawakumuamini. Walimfunga kamba na kumpeleka mbali. Alienda nchi ya Gidioni badala yake. Watu huko pia walimfunga kamba. Walimpeleka kwa Alma.
Korihori alimwambia Alma kwamba hakuna Mungu. Alisema Alma na makuhani wengine walikuwa wanadanganya watu. Korihori alisema walikuwa wanawafanya watu wafuate tamaduni za kipumbavu. Alisema pia walikuwa wanatwaa fedha kutoka kwa watu. Alma alijua hii haikuwa kweli. Aliamini katika Mungu na Yesu.
Alma alisema manabii na kila kitu ulimwenguni huwasadia watu kujua kwamba yuko Mungu. Korihori alitaka ushahidi zaidi. Alma alisema angempa Korihori ushahidi. Alisema kwamba Mungu angemfanya Korihori asiweze kuzungumza. Punde Alma aliposema hivi, Korihori hakuweza kuzungumza.
Korihori aliandika kwamba alijua Mungu yupo. Daima amekuwa akijua hivyo. Aliandika kwamba ibilisi alikuwa amemdanganya. Ibilisi alimwambia Korihori kufundisha uongo juu ya Mungu na Yesu. Wakati watu walipojua ukweli huu kuhusu Korihori, hawakuamini mafundisho yake. Walitubu na kuanza kumfuata Yesu tena.