“Ishara za Kuzaliwa kwa Yesu,” Hadithi za Kitabu cha Mormoni (2023)
Ishara za Kuzaliwa kwa Yesu
Imani katika mafundisho ya nabii
Ilikuwa karibia miaka mitano tangu Samweli nabii alipowafundisha watu kuhusu ishara za kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Watu wengi waliamini na walitazamia ishara hizo. Watu wengine walisema Samweli hakuwa sahihi na wakati wa ishara hizo tayari ulikuwa umepita. Waliwadhihaki walioamini na kusema Yesu hangekuja.
Waaminio walikuwa na wasiwasi, lakini walikuwa na imani. Wao waliendelea kutazamia ishara. Ishara moja ilikuwa usiku ambao hakungekuwa na giza. Ungekuwa angavu kama vile mchana baada ya jua kutua. Usiku usio na giza ungekuwa ishara kwamba Yesu angekuwa anazaliwa siku iliyofuata katika nchi nyingine.
Watu ambao hawakuamini walifanya mpango. Walichagua siku na kusema kwamba kama ishara haingetokea kufikia siku hiyo, waaminio wangeuawa.
Mtu aliyeitwa Nefi alikuwa nabii wakati huu. Alikuwa na huzuni sana kwamba baadhi ya watu walitaka kuwaua waaminio.
Nefi aliinama chini ardhini na kusali kwa Mungu kwa ajili ya waaminio ambao walikuwa karibu kufa kwa sababu ya imani yao. Alisali siku nzima.
Kama jibu la sala yake, Nefi alisikia sauti ya Yesu. Yesu alisema ishara ingetokea usiku ule na kisha Yeye angezaliwa siku iliyofuata.
Usiku ule kulikuwa hakuna giza ingawa jua lilikuwa limetua. Watu ambao walikuwa hawajaamini maneno ya Samweli walishangaa sana kiasi kwamba walianguka ardhini. Waliogopa kwa sababu walikuwa hawaamini. Watu ambao walikuwa wanaamini hawangeuawa.
Siku iliyofuata, jua lilichomoza tena na anga likabaki kuwa angavu. Watu walijua kwamba hii ilikuwa ile siku ambayo Yesu angezaliwa.
Watu waliona ishara nyingine. Nyota mpya ilichomoza angani. Ishara zote ambazo Samweli alikuwa amesema juu yake zilikuja kutokea kweli. Watu wengi zaidi waliamini katika Yesu na wakabatizwa.