“Machi 16–22. Yakobo 5–7: ‘Bwana Hufanya Kazi Nasi,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Machi 16–22. Yakobo 5–7,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020
Machi 16–22.
Yakobo 5–7
Bwana Hufanya Kazi Nasi
Kusoma maandiko kunaalika ufunuo. Kwa hiyo unaposoma Yakobo 5–7, tafuta mwongozo kutoka kwa Roho akusaidie wewe pamoja na familia yako. Je, ni jumbe gani Bwana anazo kwa ajili yako?
Andika Misukumo Yako
Kuna watu wengi, wengi mno ambao bado wangali hawajaisikia injili ya Yesu Kristo. Ikiwa kamwe utahisi kushindwa na uzito wa jukumu la kuwakusanya katika Kanisa la Bwana, fumbo la mizeituni katika Yakobo 5 lina ukumbusho wenye kutia moyo: mmiliki wa shamba ni Bwana. Ametupatia kila mmoja wetu sehemu ndogo kusaidia katika kazi Yake—familia yetu, kundi letu la marafiki, sehemu ambapo tuna ushawishi. Na wakati mwingine mtu wa kwanza ambaye tunasaidia kumkusanya ni sisi wenyewe. Lakini kamwe hatuko peke yetu katika kazi hii, kwa maana Bwana mwenye shamba anafanya kazi pamoja na wafanya kazi wake (ona Yakobo 5:72). Mungu anawajua na anawapenda watoto Wake, atatengeneza njia kwa ajili ya kila mmoja wao kusikia injili Yake, hata wale ambao walimkataa kipindi cha nyuma (ona Yakobo 4:15–18). Na kisha, wakati kazi itakapokuwa imekamilika, wale wote ambao wamekuwa “na bidii katika kutumikia pamoja [Naye] … Watapokea shangwe pamoja [Naye] kwa sababu ya matunda ya shamba [Lake] la mizabibu” (Yakobo 5:75).
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi
Fumbo ni nini?
Mafumbo ni hadithi ambazo hufundisha kweli za kiroho kupitia ishara. Katika fumbo la mizabibu, kwa mfano, shamba linawakilisha dunia, mzeituni unawakilisha Israeli (wale waliofanya maagano na Mungu), na michekele inawakilisha nchi za wayunani (wale ambao hawajafanya maagano na Mungu).
Unapojifunza fumbo katika Yakobo 5, tafuta ishara za ziada na utafakari kile ambacho zinaweza kuwa zinamaanisha. Kwa mfano, unafikiri matunda mema yanawakilisha nini? Matunda mabaya yaweza kuwa yanaashiria nini?
Yesu Kristo ndiye Bwana wa shamba.
Kabla haujaanza kujifunza fumbo la mizeituni katika Yakobo 5, inaweza kuwa na manufaa kufanya mapitio ya Yakobo 4:10–18 ili kujifunza ni kwa nini Yakobo alishiriki fumbo hili na watu wake. Katika Yakobo 6:3–5, utapata baadhi ya jumbe za ziada ambazo Yakobo alitaka kuzisisitiza; tafuta jumbe hizi katika fumbo. Ni jumbe zipi unazipata kwa ajili yako katika Yakobo 5?
Yakobo 5 ni mlango mrefu—mrefu zaidi katika kitabu cha Mormoni. Pengine inaweza kuwa busara kuugawa katika sehemu zifuatazo, ambazo zinaelezea nyakati za historia ya dunia:
-
Mistari 3–14:Kutawanyika kwa Israeli kabla ya wakati wa Kristo
-
Mistari 15–28:Huduma ya Kristo na Mitume
-
Mistari 29–49:Ukengeufu Mkuu
-
Mistari 50–76:Kukusanyika kwa Israeli katika siku za mwisho
-
Mistari 76–77:Milenia na mwisho wa dunia
Kwa ajili ya umaizi wa ziada kuhusu fumbo hili, ona kielelezo kinachoambatana na muhtasari huu.
Mungu ananialika nimsaidie kukusanya watoto Wake.
Wale “watumishi wengine” (Yakobo 5:70) ambao waliitwa katika shamba la Bwana ni pamoja na watu kama wewe—kama waumini wa Kanisa, ni wajibu wetu sisi wote kumsaidia Mungu kukusanya watoto Wake. Ni kanuni zipi unazopata katika Yakobo 5, hasa mistari 61–62 na 70–75, kuhusu kufanya kazi katika shamba la Bwana? Umehisi ni kwa njia gani amekuita uhudumu katika shamba Lake? Ni uzoefu gani uliopata wakati ukishiriki katika kazi Yake?
Ona pia “Kazi ya Umisionari,” Mada za Injili, topics.ChurchofJesusChrist.org; “Old Testament Olive Vineyard,” “Help the Church Grow” (video, ChurchofJesusChrist.org).
Ninaweza kusimama imara wakati wengine wanapinga imani yangu.
Tukio la Wanefi na Sheremu mara nyingi linarudiwa siku hizi: kunaweza kuwa na watu wasomi, wenye lugha fasaha ambao wanajaribu kuangamiza imani yako. Lakini Yakobo “hangetetemeshwa” (Yakobo 7:5). Je, Yakobo aliitikia kwa njia gani wakati imani yake iliposhambuliwa? Unajifunza nini kutokana na majibu yake? Utafanya nini sasa ili kujiandaa kwa ajili ya nyakati ambapo imani yako itapingwa?
Ona Pia “Kujibu Maswali ya Injili,” Mada za Injili, topics.ChurchofJesusChrist.org; Jeffrey R. Holland, “Gharama—na Baraka—za Ufuasi,” Ensign au Liahona, Mei 2014, 6–9.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani
Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.
Yakobo 5
Baadhi ya familia zinaonelea kuwa ina manufaa kuchora ishara kutoka katika fumbo la mizeituni wanapolisoma. Familia yako inaweza kufurahia mtazamo huo, au kunaweza kuwa na njia mbadala unayoweza kuwasaidia wanafamilia kupata taswira ya ishara zinazopatikana katika fumbo. Pengine unaweza kuweka alama katika sehemu kwenye meza au sakafuni kuwakilisha shamba (au dunia) na kuonyesha mzeituni (au nyumba ya Israeli) pamoja na kitu, kama vile chemshabongo, ambayo inaweza kugawanywa katika vipande (kuwakilisha kutawanywa kwa Israeli) na kisha kuletwa pamoja tena (kuwakilisha kukusanywa kwa Israeli). Je, fumbo hili linatufundisha nini kuhusu Bwana? kuhusu watumishi Wake?
Yakobo 5:70–77
Unaposoma kuhusu “mara hii ya mwisho” ambayo Bwana atatumika katika shamba Lake, ni kipi kinawatia msukumo wewe pamoja na familia yako kumtumikia Bwana “kwa uwezo wenu”? (Yakobo 5:71). Unaweza ukawaalika wanafamilia wabinafsishe mstari wa 75 kwa kuongeza majina yao katika mstari huu—kwa mfano, “Na heri nyinyi [jina].” Pengine wanaweza kushiriki uzoefu ambapo walihisi shangwe wakati walipokuwa wakimtumikia Bwana wa shamba, kwa mfano kupitia kushiriki injili, kutumikia hekaluni, au kuwaimarisha waumini wa Kanisa. (Ona pia M. Russell Ballard, “Weka Imani Yako Kwa Bwana,” Ensign au Liahona, Nov. 2013, 43–45.)
Yakobo 6:4–7
Je, ni kwa njia gani Bwana ametunyoshea mkono Wake wa huruma? Je, neno “mjishikilie” lina maana gani katika mistari hii? Je, Bwana anatushikilia kwa namna gani? Je, ni namna gani tunaweza kujishikilia Kwake?
Yakobo 7:1–12
Tunajifunza nini kutoka kwenye mistari hii kuhusu jinsi watu wanavyojaribu kuwapotosha wengine? Ni jinsi gani tunaweza kuiga mfano wa Yakobo na kuwa imara katika imani yetu katika Kristo?
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.