“Mei 17–23. Mafundisho na Maagano 51–57: ‘Mwaminifu, Mwenye haki na Mtumishi mwenye Hekima,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)
“Mei 17–23. Mafundisho na Maagano 51–57,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2021
Mei 17–23
Mafundisho na Maagano 51–57
“Mwaminifu, Mwenye haki na Mtumishi mwenye Hekima”
Kujifunza maandiko kunakusaidia kutambua sauti ya Bwana, kwani maandiko yalitolewa na Yeye kupitia Roho Wake (ona Mafundisho na Maagano 18:34–36).
Andika Misukumo Yako
Kwa waumini wa Kanisa mnamo miaka ya 1830, kuwakusanya Watakatifu na kuujenga mji wa Sayuni ilikuwa kazi ya kiroho vilevile ya kimwili, ikiwa na maswala mengi ya kiufundi ya kushughulikia: Mtu alihitajika kununua na kugawa ardhi ambapo Watakatifu wangeweza kukaa. Mtu alihitajika kuchapisha vitabu na machapisho mengine. Na mtu alihitajika kusimamia ghala ili kutoa bidhaa kwa wale waliokuwa Sayuni. Kwenye ufunuo ulioandikwa katika Mafundisho na Maagano 51–57, Bwana aliwateua na kuwaelekeza watu kushughulikia majukumu haya, na Yeye alipendekeza Independence, Missouri, kama “eneo la katikati” la Sayuni (Mafundisho na Maagano 57:3).
Lakini wakati ujuzi katika mambo kama ya ununuzi wa ardhi, uchapishaji, na usimamizi wa ghala ni yenye thamani kwenye kazi ya kimwili ya kuijenga Sayuni, ufunuo huu pia unafundisha kwamba Bwana anakusudia Watakatifu Wake wawe wenye kustahili kiroho kuitwa watu wa Sayuni. Anatuita kila mmoja wetu kuwa “Mwaminifu, Mwenye haki, na Mtumishi mwenye Hekima,” tukiwa na roho iliyopondeka, “tukisimama imara” katika majukumu yetu tuliyopewa (ona Mafundisho na Maagano 51:19; 52:15; 54:2). Ikiwa tunaweza kufanya hivyo—licha ya ujuzi wetu wa kimwili—Bwana anaweza kututumia kuijenga Sayuni, na Yeye “atauhimiza mji katika wakati wake”(Mafundisho na Maagano 52:43).
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi
Bwana ananitaka niwe mwaminifu, mwenye haki na mtumishi mwenye Hekima.
Ikiwa ungekua muumini wa Kanisa mnamo 1831, ungeweza kuwa umealikwa kuishi sheria ya uwekaji wakfu kwa kutoa mali zako kwa Kanisa kupitia askofu. Kisha yeye angerejesha kwako, mara nyingi, kile ulichotoa, wakati mwingine kikiwa na ziada. Lakini ilikuwa si tena mali yako—ilikuwa utumishi wako.
Leo taratibu ziko tofauti, lakini kanuni za uwekaji wakfu na utumishi bado ni muhimu kwenye kazi ya Bwana. Zingatia maneno haya kutoka kwa Mzee Quentin L. Cook: “Tunaishi katika nyakati za hatari ambapo wengi wanaamini hatuwajibiki kwa Mungu na kwamba hatuna wajibu binafsi au utumishi kwa ajili yetu au kwa ajili ya wengine. Wengi ulimwenguni wamefokasi kwenye kujiridhisha wenyewe … [na] hawaamini kwamba wao ni walinzi wa kaka zao. Ndani ya Kanisa, hata hivyo, tunaamini kwamba utumishi huu ni uaminifu mtakatifu” (“Utumishi—Uaminifu Mtakatifu,” Ensign au Liahona, Nov. 2009, 91).
Unaposoma sehemu ya 51, fikiria kuhusu kile ambacho Mungu amekikabidhi kwako. Ni nini maneno “mtumishi” (mstari wa 19) na “iliyowekwa wakfu” (mstari wa 5) humaanisha, na ni nini maneno hayo hudokeza kuhusu matarajio ya Mungu juu yako? Ni kanuni zipi unapata katika sehemu ya 51 na katika maneno ya Mzee Cook ambazo zinakufundisha kile inachomaanisha kuwa mtumishi? (Ona hasa mistari 9, 15–20).
Ona pia Mathayo 25:14–30; “The Law of Consecration,” video, ChurchofJesusChrist.org.
Mafundisho na Maagano 52:14–19
Mungu alitoa utaratibu kwa ajili ya kuepuka udanganyifu.
Kukiwa na watu wengi waliodai madhihirisho ya kiroho, Watakatifu wa mwanzo walikuwa na wasiwasi kuhusu kudanganywa. Ni kwa jinsi gani wangeweza kujua nani alikua “amekubaliwa na [Mungu]”? (mstari wa 15). Katika Mafundisho na Maagano 52:14–19, Bwana alitoa utaratibu wenye msaada. Ni kwa jinsi gani unaweza kutumia utaratibu huu ili kugundua ujumbe wa uongo ulimwenguni? Ungeweza pia kutumia utaratibu huu kujitathmini mwenyewe: fikiria kutumia vifungu vya maneno kutoka kwenye mistari hii kuandika maswali kama vile “Wakati ninapozungumza, je, roho yangu imepondeka?”
Ninaweza kumgeukia Bwana wakati ninapoumizwa na chaguzi za wengine.
Kama sehemu ya kukusanyika huko Ohio, kundi la Watakatifu likiongozwa na Newel Knight liliwasili kutoka Colesville, New York, na kuhitaji mahala pa kuishi. Leman Copley alikua na shamba kubwa karibu na Kirtland, na alifanya agano kuruhusu Watakatifu kukaa kwenye ardhi yake. Hata hivyo, muda mfupi baada ya kuanza makazi huko, Copley aliyumba katika imani yake, akavunja agano lake, na kuwafukuza Watakatifu kutoka kwenye ardhi yake (ona Watakatifu, 1:125–28).
Kama ilivyoandikwa katika sehemu ya 54, Bwana alimwambia Newel Knight kile ambacho Watakatifu walipaswa kufanya kuhusu hali yao. Ni nini unachopata katika ufunuo huu ambacho kinaweza kukusaidia wakati misimamo iliyovunjwa ya mtu mwingine au chaguzi mbaya za mtu mwingine zinapokuathiri?
Mafundisho na Maagano 56:14–20
Heri wenye moyo safi.
Katika mistari hii, Bwana alizungumza kwa wote matajiri na masikini; ingeweza kuwa ya kuvutia kulinganisha ushauri Wake kwa makundi haya mawili. Ni nini katika mistari hii kinaonekana kuhusika kwako binafsi? Ni kwa jinsi gani kufokasi kwenye utajiri “kunaharibu” roho yako? (mstari wa 16). Inamaanisha nini kwako kuwa “maskini aliye safi moyoni” (mstari wa 18) kuhusiana na mali za dunia?
Ona Yakobo 2:17–21.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Nyumbani
-
Mafundisho na Maagano 51:9.Mngeweza kucheza mchezo ambao familia inaufurahia na kisha zungumzeni kuhusu jinsi ambavyo mchezo ungekuwa tofauti ikiwa mtu angefanya udanganyifu. Kwa nini ni muhimu “kufanya haki” kwa kila mmoja? Ni kwa jinsi gani uaminifu hutusaidia “kuwa na umoja”?
-
Mafundisho na Maagano 52:14–19.Unapojadili utaratibu ulioelezwa katika mistari hii, familia yako ingeweza kufurahia kuangalia taratibu zingine unazotumia—kama vile utaratibu wa kushona nguo au kutengeneza chombo. Mngeweza kufanya kazi pamoja kutengeneza kitu kutoka kwenye utaratibu wakati mkizungumza kuhusu utaratibu Bwana aliotoa ili kuepuka udanganyifu.
-
Mafundisho na Maagano 53:1.Fikiria kushiriki na familia yako uzoefu wakati wewe, kama vile Sidney Gilbert, ulimuomba Bwana “juu ya wito wako.”
-
Mafundisho na Maagano 54:2; 57:6–7.Inamaanisha nini “kusimama imara” (Mafundisho na Maagano 54:2) katika kile ambacho Mungu ametutaka kufanya? Ungeweza kuwaalika wanafamilia kusimama na kutaja kitu ambacho Mungu amewataka wafanye.
-
Mafundisho na Maagano 55.Ni kwa jinsi gani Bwana alitumia uwezo wa William Phelps kama mwandishi na mchapishaji? (Kwa mfano, ona kielezo cha mwandishi katika kitabu cha nyimbo za kanisa kwa ajili ya orodha ya nyimbo alizoandika). Pengine wanafamilia wangeweza kuzungumzia talanta na uwezo wanaouona ndani ya kila mmoja. Ni kwa jinsi gani talanta zetu zinachangia kwenye kazi ya Mungu?
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.
Wimbo uliopendekezwa: “‘Give,’ Said the Little Stream,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto,236.