Mafundisho na Maagano 2021
Mei 24–30. Mafundisho na Maagano 58–59: “Kujishughulisha kwa Shauku katika Kazi Njema”


“Mei 24–30. Mafundisho na Maagano 58–59: ‘Kujishughulisha kwa Shauku katika Kazi Njema,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)

“Mei 24–30. Mafundisho na Maagano 58–59,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2021

Picha
Mtaa wa Independence Missouri

Independence, Missouri, na Al Rounds

Mei 24–30

Mafundisho na Maagano 58–59

“Kujishughulisha kwa Shauku katika Kazi Njema”

Rais Dallin H. Oaks alifundisha, “Maandiko yatatusaidia kutatua maswali yetu yote kwa sababu kwa kuyasoma tunajialika na kujistahilisha kwa ajili ya uvuvio wa Roho Mtakatifu, ambao utatuongoza kwenye ukweli wote” (katika David A. Edwards, “Je, Majibu Yangu Yako Humo?New Era, Mei 2016, 42).

Andika Misukumo Yako

Wakati wazee wa Kanisa mwanzoni walipoona eneo la jiji la Sayuni—Independence, Missouri—haikuwa kile walichotegemea. Baadhi walifikiri wangekuta jumuiya iliyositawi, yenye bidii pamoja na kundi lenye nguvu la Watakatifu. Badala yake walikuta makazi machache yaliyojitenga, yasiyo na ustaarabu waliouzoea na yaliyokaliwa na wakazi waanzilishi wenye fujo badala ya Watakatifu. Ilionekana kwamba Bwana hakuwaomba tu kuja Sayuni—Yeye aliwataka wao kuijenga Sayuni.

Wakati matarajio yetu hayalandani na uhalisia, tunaweza kukumbuka kile Bwana alichowaambia Watakatifu mnamo 1831: “Hamuwezi kuona kwa macho yenu ya asili, kwa wakati huu, mipango ya Mungu wenu … na utukufu utakaofuata baada ya taabu kubwa.(Mafundisho na Maagano 58:3). Ndiyo, maisha yamejaa mateso, hata uovu, lakini tunaweza “kutekeleza haki nyingi; kwa uwezo ulio ndani [yetu]” (mistari 27–28).

Ona pia Watakatifu, 1:127–33.

Picha
ikoni ya kujifunza kibinafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi

Mafundisho na Maagano 58:1–5, 26–33, 44; 59:23

Baraka huja kulingana na muda wa Mungu na bidii yetu.

Watakatifu waliweka msingi wa Sayuni huko Jackson County, Missouri, ambapo walivumilia majaribu mengi. Hakika walitumaini kwamba wakati wa kipindi cha maisha yao eneo hili lingesitawi kuwa mahala ambapo Watakatifu wote wangeweza kukusanyika. Hata hivyo, Watakatifu walifukuzwa kutoka Jackson County ndani ya miaka michache, na Bwana alifunua kwamba watu Wake walipaswa “kusubiri kwa kipindi kifupi kwa ajili ya ukombozi wa Sayuni” (Mafundisho na Maagano 105:9).

Unaposoma vifungu vifuatavyo, tafuta kwa nini baraka zinaweza kuzuiliwa kwa muda. Maswali yafuatayo yanaweza kukusaidia kutafakari.

Mafundisho na Maagano 58:1–5; 59:23. Ni ujumbe upi katika mistari hii unaimarisha uwezo wako wa kupitia mateso kwa uvumilivu zaidi? Ni baraka zipi umepokea baada ya mateso? Kwa nini unadhani baadhi ya baraka huja tu baada ya mateso.

Mafundisho na Maagano 58:26–33. Ni jukumu lipi ambalo “kujishughulisha kwa shauku katika kazi njema” linalo katika utimizwaji wa ahadi za Mungu? Ni jukumu lipi utiifu wako unalo?

Mafundisho na Maagano 58:44. Kuna uhusiano gani kati ya “sala ya imani” na mapenzi ya Bwana kwetu?

Mafundisho na Maagano 59, kichwa cha habari cha sehemu

Polly Knight alikuwa nani?

Polly Knight na mumewe, Joseph Knight mkubwa, walikuwa baadhi ya waaminio wa mwanzo katika wito wa kinabii wa Joseph Smith. Polly na Joseph walitoa usaidizi muhimu kwa Nabii katika kazi ya kutafsiri Kitabu cha Mormoni. Familia ya Knight iliondoka Colesville, New York, ili kukusanyika pamoja na Watakatifu huko Ohio na baadaye waliamriwa kuhamia Jackson County, Missouri. Walipokuwa wakisafiri, afya ya Polly ilianza kuwa mbaya, lakini alikuwa ameweka msimamo wa kuiona Sayuni kabla ya kifo chake. Alikuwa ameishi Missouri siku chache tu wakati alipofariki (ona Watakatifu, 1:127–28, 132–33). Mafundisho na Maagano 59 ilipokelewa siku ya kifo chake, na mistari 1 na 2 inaonekana kuwa mahususi kwake.

Mafundisho na Maagano 59:9–19

Kuitakasa Sabato kunaleta baraka za kimwili na kiroho.

Baada ya kuahidi kuwabariki Watakatifu katika Sayuni, “kwa amri zisizo haba,” Bwana alitoa msisitizo maalumu kwa amri moja hasa: amri ya kuitakasa “siku yake takatifu” (Mafundisho na Maagano 59:4, 9). Unapojifunza Mafundisho na Maagano 59:9–19, tafakari kwa nini kuitakasa Sabato kungekuwa muhimu sana kwa Watakatifu hawa wakati walipotafuta kuijenga Sayuni.

Ungeweza pia kutafakari maswali kama haya: je, ninatumia siku ya Sabato katika njia ambayo Bwana alikusudia? Ni kwa jinsi gani kuitakasa Sabato kunanisaidia kubaki “bila mawaa ya ulimwengu”? (mstari wa 9). Nini ninaweza kufanya ili kutoa “dhabihu zangu za shukrani kwa Aliye Juu Sana”? (mstari wa 10).

Baada ya kusoma mistari ifuatayo, unapata msukumo wa kufanya nini ili kuitakasa Sabato kikamilifu zaidi? Mwanzo 2:2–3; Kutoka 20:8–11; 31:13, 16; Kumbukumbu la Torati 5:12–15; Isaya 58:13–14; Marko 2:27; Yohana 20:1–19; Matendo ya Mitume 20:7.

Ungeweza pia kunufaika kutokana na moja ya video nyingi au nyenzo zingine kuhusu Sabato zinazopatikana kwenye sabbath.ChurchofJesusChrist.org.

Ona pia Russell M. Nelson, “Sabato Ni ya Kupendeza,” Ensign au Liahona, Mei 2015, 129–32; Kamusi ya Biblia, “Sabato.”

Picha
mkate na vikombe vya sakramenti

Kushiriki sakramenti ni sehemu ya kuitakasa Sabato.

Picha
ikoni ya kujifunza kifamilia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Nyumbani

Mafundisho na Maagano 58:26–29.Pengine wanafamilia wangeweza kutengeneza orodha ya baadhi ya mambo ambayo kwayo “wanajishughulisha kwa shauku”. Je, yote ni “kazi njema”? Kwa nini Bwana anatutaka tufanye “mambo mengi kwa hiari [yetu] wenyewe”? Muombe kila mwanafamilia kufikiria juu ya nini wanaweza kufanya wiki hii ili “kutekeleza haki nyingi.” Baadaye wanaweza kutoa taarifa juu ya kile walichofanya.

Mafundisho na Maagano 58:42–43.Je, nini wanafamilia wanahisi wakati wanaposoma mistari hii? Ni kwa jinsi gani mistari hii ingeweza kumsaidia mtu anayehitaji toba?

Mafundisho na Maagano 59:3–19.Inaweza kumaanisha nini “kuvikwa taji la … amri”? (mstari wa 4). Unaposoma amri katika mistari 5–19, jadili baraka ulizopokea kwa kutii kila moja ya amri hizi.

Ungeweza pia kugundua jinsi maneno kama “shangwe”, “kushangilia,” “moyo mkunjufu,” na “kufurahi” yalivyotumika kuelezea amri ya kuheshimu siku ya Sabato. Unawezaje kuifanya Sabato yako kuwa ya shangwe zaidi? Pengine familia yako ingeweza kutengeneza mchezo wa kulinganisha kwa kutumia kadi ambazo huwakilisha vitu unavyoweza kufanya ili kuitakasa Sabato.

Mafundisho na Maagano 59:18–21.Tuweza kufanya nini ili “kukiri … Mkono wa [Mungu] katika mambo yote”? (mstari wa 21). Fikiria kwenda matembezini au kutazama picha, ukigundua vitu ambavyo “vinaridhisha jicho na … kufurahisha moyo” (mstari wa 18). Ungeweza kuchukua au kuchora picha ya kile unachopata na kisha kuzungumza kuhusu jinsi unavyoweza kuonesha shukrani kwa vitu hivi. Ni kwa jinsi gani tumeuona mkono wa Mungu katika maisha yetu?

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Wimbo uliopendekezwa: “Choose the Right,” Nyimbo za Kanisa, na. 239.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Shiriki maandiko. Wape wanafamilia muda wa kushiriki vifungu vya maandiko walivyopata katika kujifunza kwao binafsi ambavyo vina maana kwao.

Picha
msichana akiomba wakati wa sakramenti

Kielelezo na Marti Major

Chapisha