“Juni 7–13. Mafundisho na Maagano 63: ‘Kile Ambacho Huja kutoka Juu Ni Kitakatifu,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)
“Juni 7–13. Mafundisho na Maagano 63,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2021
Juni 7–13
Mafundisho na Maagano 63
“Kile Ambacho Huja kutoka Juu Ni Kitakatifu”
Bwana alisema, “Mnampokea Roho kwa njia ya sala” (Mafundisho na Maagano 63:64). Fikiria kusali kwa ajili ya Roho kuongoza kujifunza kwako.
Andika Misukumo Yako
Eneo kwa ajili ya mji wa Sayuni lilikuwa limechaguliwa. Viongozi wa Kanisa walikuwa wametembelea eneo hili na kuliweka wakfu kama eneo la kukusanyika kwa ajili ya Watakatifu. Kulingana na historia ya Joseph Smith, “nchi ya Sayuni ilikuwa ndicho kitu kilichokuwa cha maana zaidi usoni” (Mafundisho na Maagano 63, kichwa cha habari cha sehemu). Lakini mitazamo juu ya Sayuni ilikuwa mingi. Watakatifu wengi walikuwa na shauku ya kuanza kukusanyika Missouri. Kwa upande mwingine, watu kama Ezra Booth walikuwa wamekatishwa tamaa na ardhi ya Sayuni na waliweka wazi mitazamo yao. Kwa kweli, wakati Joseph aliporejea Kirtland kutoka Missouri, alikuta kwamba mabishano na ukengeufu vilikuwa vimenyemelea Kanisani wakati alipokuwa hayupo. Ilikuwa ni katika mazingira haya kwamba ufunuo katika Mafundisho na Maagano 63 ulipokelewa. Hapa Bwana alizungumzia ununuzi wa ardhi na kuwahamishia Watakatifu Missouri. Lakini kati ya maswala hayo ya kiutendaji ilikuwa ni ukumbusho wa mara kwa mara: “Mimi, Bwana, naitoa sauti yangu, na mtaitii” (mstari wa 5). Sauti Yake, mapenzi Yake, amri Yake—vyote ambavyo “[huja] kutoka juu havipaswi kuchukuliwa kwa ubeuzi au kawaida. Ni “kitakatifu, na ni lazima kitamkwe kwa uangalifu” (mstari wa 64).
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi
Mafundisho na Maagano 63:1–6; 32–37
Hasira ya Bwana inawaka dhidi ya waovu na waasi.
Wakati ufunuo huu ulipopokelewa, Joseph Smith alikuwa akipitia ukosoaji wa kikatili kutoka kwa waumini kadhaa wa Kanisa ambao walikuwa wamemuasi (ona “Ezra Booth na Isaac Morley,” Ufunuo katika Muktadha, 130–36). Ni maonyo gani Bwana alitoa katika Mafundisho na Maagano 63:1–6, 32–37 kuhusu “waovu na waasi”? Ni kwa jinsi gani maonyo kama hayo ni ushahidi wa upendo wa Mungu?
Ishara huja kwa imani na mapenzi ya Mungu.
Ishara au miujiza pekee havileti imani ya kudumu. Mapema mnamo 1831 Ezra Booth, mtumishi wa Kimethodist huko Kirtland, aliamua kubatizwa baada ya kumwona Joseph Smith kimiujiza akiponya mkono wa rafiki wa Booth Elsa Johnson.
Na bado, ndani ya miezi michahce, Booth alipoteza imani yake na kuwa mkosoaji wa Nabii. Hili lingewezekanaje, ukizingatia muujiza aliokuwa ameshuhudia? Fikiria hili unaposoma Mafundisho na Maagano 63:7–12. Ungeweza pia kufikiria kwa nini baadhi ya watu hupokea ishara “kwa faida ya wanadamu kwa utukufu wa [Mungu]” (mstari wa 12) na wengine huzipokea “kwa … maangamizo” (mstari wa 11). Kwa kuzingatia kile ulichosoma, ni jinsi gani unafikiri Bwana anakutaka ufikirie na kuhisi kuhusu ishara?
Ona pia Mathayo 16:1–4; Yohana 12:37; Mormoni 9:10–21; Etheri 12:12, 18.
Mafundisho na Maagano 63:13–23
Usafi wa kimwili humaanisha kuyaweka mawazo yangu na matendo kuwa safi.
Watu wengi wangetambua kwamba uzinzi ni kitu kibaya. Lakini katika Mafundisho na Maagano 63:13–19, Mwokozi aliweka wazi kwamba mawazo ya kutamani pia yana madhara ya kufisha ya kiroho. “Kwa nini kutamani ni dhambi mbaya kiasi hicho?” Mzee Jeffrey R. Holland aliuliza. “Basi, pamoja na kuwa na athari ya kuharibu kabisa Roho tuliyonayo mioyoni mwetu, ninafikiri ni dhambi kwa sababu inachafua uhusiano mkuu na mtakatifu ambao Mungu hutupatia katika maisha ya muda—upendo ambao mume na mke wanao kila mmoja kwa mwingine na hamu ambayo wenzi huo unao kuleta watoto katika familia inayokusudiwa kuwa ya milele” (“Hakuna Nafasi Tena kwa Adui wa Nafsi Yangu,” Ensign au Liahona, Mei 2010, 44).
Ni madhara gani Bwana anayataja katika Mafundisho na Maagano 63:13–19 ambayo yatawajia wale ambao hawatubu kwa mawazo na matendo machafu? Gundua baraka Mwokozi anazoahidi katika mstari wa 20 na 23 kwa wale ambao ni waaminifu. Ni baraka zipi zimekuja maishani mwako kutokana na kutii sheria ya usafi wa kimwili? Ni jinsi gani Mwokozi anakusaidia kubaki au kuwa msafi?
Ona pia Mafundisho na Maagano 121:45; Linda S. Reeves, “Ustahiki kwa Baraka Zetu Zilizoahidiwa,” Ensign au Liahona, Nov. 2015, 9–11.
Mafundisho na Maagano 63:24–46
Bwana anaongoza maswala ya kiroho na kimwili ya Watakatifu Wake.
Baada ya Bwana kuonesha wapi Sayuni itajengwa, Watakatifu huko Ohio bado walihitaji mwongozo kuhusu lini waanze kuhama na wapi pa kupata pesa ya kununua ardhi. Unaposoma Mafundisho na Maagano 63:24–46, tafuta mwongozo wa kiroho na kimwili Bwana aliotoa kuhusu Sayuni. Ni mwongozo upi wa kiroho na kimwili Bwana anakupatia?
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Nyumbani
-
Mafundisho na Maagano 63:7–12.Hadithi ya Ezra Booth kuacha Kanisa licha ya kushuhudia uponyaji wa Elsa Johnson (ona maelezo mafupi katika “Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi” na kielelezo ambacho kinaambatana na muhtasari huu) vinaweza kuchochea mjadala kuhusu miujiza. Pengine wanafamilia wako wangeweza kuzungumzia miujiza ambayo imeimarisha imani yao, ikijumuisha uzoefu kutoka kwa familia yako au historia ya familia yako. Ni kwa namna gani walionesha imani inayohitajika kupokea miujiza hii? Ni nini Mafundisho na Maagano 63:7–12) inafundisha kuhusu uhusiano kati ya imani na miujiza?
-
Mafundisho na Maagano 63:13–19.Ni kwa jinsi gani tunaweza kujilinda kutokana na ushawishi usiostahili, ikiwa ni pamoja na ponografia? (Unaweza kupata nyenzo nyingi zenye msaada kwa ajili ya familia kwenye AddressingPornography.ChurchofJesusChrist.org.) Ni zipi baraka za kuishi sheria ya usafi wa kimwili?
-
Mafundisho na Maagano 63:23.Ni kwa jinsi gani unaweza kuisaidia familia yako kuelewa jinsi “siri za ufalme,” au kweli za injili, ni kama “chemchemi ya maji ya uzima”? Kwa mfano, ungeweza kusafiri kwenda kwenye chemchemi au mto ulio karibu (au onesha video au picha ya vitu hivyo). Ni kwa jinsi gani kweli za injili ni kama maji?
-
Mafundisho na Maagano 63:58.Ni maonyo gani tunayapata katika sehemu ya 63? Ni nini baadhi ya maonyo tunasikia kutoka kwa viongozi wetu wa Kanisa leo?
-
Mafundisho na Maagano 63:58–64.Ioneshe familia yako hazina ya thamani ya familia. Ni kwa jinsi gani tunakichukulia kitu hiki tofauti na vitu vingine ambavyo si vya thamani? Ni nini Mafundisho na Maagano 63:58–64 inatufundisha kuhusu kile tunachoweza kufanya ili kuvipa heshima vitu vitakatifu?
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.
Wimbo uliopendekezwa: “Reverence Is Love,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto,31.